Dar es Salaam. Katika kipindi cha hivi karibuni, kumekuwa na mjadala unaozidi kushika kasi miongoni mwa wadau wa demokrasia kuhusu mwenendo wa vyama vya upinzani nchini na namna vinavyoelekeza nguvu zao katika kujijenga kisiasa.
Badala ya kuelekeza nguvu kwa chama tawala ili kuhakikisha wananchi wanakuwa na maisha bora, baadhi ya wadau wanaona vyama hivyo vinaonekana kukiandama zaidi Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), hali inayozua maswali kuhusu mwelekeo na mshikamano wa upinzani nchini.
Kihistoria, vyama vya upinzani hujipambanua kwa kujenga hoja na sera mbadala dhidi ya chama kilicho madarakani. Hata hivyo, katika mazingira ya sasa, uhalisia unaonyesha kuwepo kwa migongano ya ndani miongoni mwa vyama hivyo, ikichangiwa na tofauti za kiitikadi, ushindani wa kisiasa na harakati za kutafuta umaarufu.
Wadau wa demokrasia wanasema Chadema, kama chama kikubwa cha upinzani chenye ushawishi mkubwa, kimekuwa kikilengwa zaidi kutokana na nafasi yake hiyo.
Vyama vidogo vinaweza kuona ni rahisi kujijenga kisiasa kwa kukikosoa Chadema badala ya kukabiliana moja kwa moja na chama tawala chenye rasilimali na mtandao mpana wa kisiasa, na kinachowajibika kuboresha maisha ya wananchi.
Wapo wanaohisi pengine mgawanyiko huo unaweza kudhoofisha juhudi za upinzani kwa ujumla, kwani kukosekana kwa sauti ya pamoja kunapunguza nguvu ya hoja dhidi ya sera za serikali, na hivyo kutoa mwanya kwa chama tawala kuendelea kutawala bila upinzani wenye mshikamano wa kutosha.
Kwa wapiga kura, hali hiyo inaweza kuleta mkanganyiko na hata kupunguza imani kwa vyama vya upinzani, ingawa wapo wanaoona hali hiyo kama sehemu ya ukuaji wa demokrasia ambapo vyama vinaruhusiwa kukosoana na kujipima nguvu.
Msingi wa mjadala huo unatokana na ujumbe aliouandika kwenye mitandao ya kijamii Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi (Bara), Joseph Selasini, aliyewataka wananchi kukichangia Chadema kwa kile alichodai kuwa kina nia ya kweli ya kuwapigania Watanzania.
Mwananchi ilimtafuta Selasini ili kupata ufafanuzi wa ujumbe wake huo. Amesema msingi wa hoja hiyo unatokana na matokeo ya kilichojiri kwenye Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD), kilichofanyika hivi karibuni baada ya yeye kuwasilisha hoja binafsi ya kutaka mabadiliko ya kanuni ili Chadema ijumuishwe.
Amesema chombo hicho kinajumuisha vyama vyenye uwakilishi katika vyombo vya uamuzi, lakini yeye alitaka Chadema kijumuishwe kwa kuwa kina ushawishi mkubwa katika kubadili sheria, kama ambavyo kanuni hizo ziliwahi kubadilishwa na kukijumuisha NCCR-Mageuzi kilipokuwa na madiwani pekee.
“Baada ya kuwasilisha hoja hiyo, mapokeo ya wadau wenzangu katika kikao hicho yalikuwa ya kupinga, wakitaka Chadema ibaki nje. Huo ndiyo ulikuwa msingi wa kuandika ujumbe huo kwenye mitandao,” amesema.
Amesema vyama vingi vya upinzani havikipendi Chadema kwa sababu ya wivu usio na hoja, akieleza kuwa lengo lake katika kikao hicho lilikuwa kukijumuisha chama hicho ili kujenga sauti moja ya upinzani, lakini wenzake walimpinga.
“Ni ukweli usiopingika kuwa Chadema imekuwa sauti ya wananchi kwa sasa. Hata tukizungumzia maridhiano, huwezi kuiepuka Chadema. Kinapitia misukosuko mingi; viongozi wake wamekamatwa, lakini hakuna namna ya kukiepuka,” amesema.
Amesema anachozungumza ni ukweli, na licha ya kuwa yeye ni kiongozi wa NCCR-Mageuzi, hajali atachukuliwaje. Ameongeza kuwa Chadema inachukiwa zaidi kwa sababu ina mtandao mpana kuliko vyama vingine.
“Ukubwa wao unatokana na kuzungumzia ajenda za wananchi. Kwa mfano, katika kipindi ambacho walikuwa wamefungiwa, hakuna chama cha upinzani kilichotoka kuzungumzia shida za wananchi zaidi ya Chadema, ambayo hata ikiwa mafichoni iliendelea kuzungumza,” amesema.
Katika kujenga hoja yake, Selasini amesema hata mgombea urais wa CCM, baada ya kushinda kwa kishindo, alieleza kuwa moja ya sababu za ushindi huo ni kwamba wapiga kura wa chama kikubwa kilichotarajiwa kuleta ushindani walimpigia kura.
“Kama CCM wenyewe wanakubali, inakuwaje sisi vyama vya upinzani tugawanyike na kukitenga Chadema, wakati Watanzania wenyewe wanakipenda na kinafanya mikutano nchi nzima?” amehoji.
Hata hivyo, hoja ya Selasini imepingwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) Bara, Benson Kigaila, ambaye anadai kuwa wao walikuwa wanapinga hoja aliyosema ilikuwa dhaifu, na si kwamba walikuwa wanakipinga Chadema.
“Vyama 14 havipo; unataka kutengeneza sheria ziruhusu Chadema iingie, halafu vile vinavyobakia unavipeleka wapi? Haikubaliki kutunga sheria kwa sababu ya chama kimoja; hiyo si demokrasia,” amesema.
Kigaila amesema kuwa Selasini kuwasilisha hoja hiyo hakumfai kuwa kiongozi wa chama, wala hata kiongozi wa genge la mboga, kwa kuwa haiwezekani kutunga sheria au kanuni kwa ajili ya kukiwezesha chama fulani kuingia TCD; kuingia humo kunategemea sifa.
“TCD unaingia kwa sifa na kufuzu; suala la Chadema kuingia TCD haliwezekani kwa kuwa hakina sifa. Badala yake, kinaweza kuingia kwenye majukwaa mengine kama Baraza la Vyama vya Siasa, ambalo kila chama kina haki ya kuingia,” amesema.
Kuhusu kubadilisha kanuni ili NCCR-Mageuzi ijumuishwe, Kigaila amesema awali TCD ilikuwa inahusisha vyama vyenye wawakilishi Bungeni. Hata hivyo, idadi ya vyama vyenye wabunge ilipopungua, walikubaliana kurekebisha kanuni ili kujumuisha vyama vyenye angalau madiwani watatu.
“Baada ya mabadiliko hayo, NCCR-Mageuzi ilipata sifa, lakini lengo halikuwa kubadili kanuni kwa ajili ya chama kimoja. Itakuwa ni jambo lisilo la busara kutunga sheria ili kiingie chama kimoja,” amesema.
Amesema ndiyo maana, baada ya Selasini kuwasilisha hoja hiyo, waliipinga kwa kuwa Chadema haina sifa za kufuzu kuingia.
Kuhusu hoja kwamba vyama haviungani, Kigaila amesema hilo haliwezekani kwa kuwa kila chama kimesajiliwa kivyake. Ameongeza kuwa kama NCCR-Mageuzi haina sera mbadala za kukabiliana na CCM, basi haifai kulinganisha na vyama vingine vya upinzani.
“Nashangaa anaposema Chadema ni chama kikubwa—huo ukubwa unapimwaje? Ukubwa wa chama hupimwa kwa uwakilishi katika vyombo vya maamuzi. Miaka ya nyuma kilikuwa chama kikubwa kwa sababu kilikuwa na wabunge na madiwani,” amesema.
Amesema kuwa Chaumma haijawahi kuipinga Chadema, kwani walishafunga mjadala huo. Ameeleza kuwa ni Chadema wanaoendelea kujadili Chaumma bila sababu za msingi, huku wao wakijikita katika kukijenga chama chao.
Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na Mwenyekiti wa TCD, Dorothy Semu, amesema hawezi kumjibu Selasini kwa kuwa hoja aliyoieleza inahusu masuala ya vikao.
“ACT-Wazalendo tumekuwa mstari wa mbele kutafuta muungano na vyama vingine vya upinzani ili kuwa na sauti moja, na tumekuwa tukigonga milango lakini haifunguliwi,” amesema.
Amesema kuwa wanaendelea kujifunza kutoka mataifa mbalimbali, ikiwemo Kenya, na wanaamini kuwa siku zijazo watafanikiwa kukamilisha mpango huo, japokuwa kwa sasa wanakabiliwa na changamoto.
Katibu wa Muungano wa vyama 13 vya upinzani nchini, Doyo Hassan Doyo, amesema Tanzania ni nchi ya demokrasia, hivyo kutoa mitazamo yao kwa umma haina maana kwamba wanakiandama Chadema.
“Huo ni mtazamo wake, lakini huwezi kukubaliana na kila jambo kama mbuzi. Sisi ni binadamu, tuna uwezo wa kufikiri. Kama yeye anawaza kukilinda Chadema, ni uhuru wake wa mawazo,” amesema.
Ameongeza kuwa si kweli kwamba vyama vya upinzani vinakisakama Chadema, bali vinakipinga kutokana na misimamo yake, ikiwemo ile ya “kukinukisha”.
“Hatukisakami Chadema; msimamo wetu uko wazi. Wakati mwingine hatukubaliani na ajenda zao na maneno yao kwamba wanataka kuchukua nchi kwa kukinukisha,” amesema.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Lugete Mussa, amesema suala hilo ni mjadala mpana unaotokana na sababu za kihistoria na ushindani wa kisiasa, akibainisha kuwa Chadema ilianza kupata nguvu mwaka 2010 baada ya kubeba ajenda ya ufisadi.
Amesema vyama visivyo na uwakilishi Bungeni mara nyingi huunda miungano yao, ambayo wakati mwingine huegemea upande wa dola.
“Vyama vikubwa kama Chadema mara nyingi havipendi kusikia viongozi wa vyama vidogo wakizungumza,” amesema, na kuongeza: “Hiyo ni saikolojia yao ya ushindi. Vyama vingine vinajua Chadema vinavidharau, ndiyo maana hawawezi kukubali kuwa kitu kimoja. Kinachotokea ni ushindani wa kimkakati,” amesema.
Amesema Chadema, “Wamejijengea saikolojia ya ushindi kwamba jambo lolote jema lazima litoke kwao. Si kwamba Chadema inachukiwa, isipokuwa Chadema imekuwa chanzo cha chuki kwa wengine.”
Amesema Chadema huvituhumu vyama vingine kwa umma kuwa ni wasaliti, jambo linalofanya kushindwa kwao kushirikiana kwa ufanisi dhidi ya CCM.
Akijibu baadhi ya hoja hizo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Bara), Aman Golugwa, amesema chama hicho kinaamini katika ushirikiano na vyama vingine.
“Tupo tayari kushirikiana na chama chochote ambacho mbele ya Watanzania kinaonekana kutetea maslahi ya wananchi. Tumekuwa na uzoefu na vyama ambavyo vimebebwa na dola,” amesema.
Amesema kuwa baadhi ya vyama hivyo vimetumika kuhalalisha mambo ya serikali, na hata mwaka jana viliposhiriki mijadala ya mabadiliko ya mifumo ya uchaguzi vilionekana kuunga mkono ajenda ya chama tawala.
“Walijitengenezea wenyewe jina la ‘vyama vikaragosi’. Si Chadema tunawaita hivyo, bali ni taswira waliyojijengea mbele ya hadhira wanapopambana na vita ya chama tawala dhidi yetu,” amesema.
