RAIS SAMIA AKABIDHI MITUNGI YA GESI YA ORYX KWA BABA, MAMA LISHE

******

Na  Mwandishi Wetu

KAMPUNI ya Oryx Gas Tanzania imetoa seti 200 za mitungi ya Oryx kwa Serikali kupitia Wizara ya Nishati ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono

Mpango wa kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Oryx imekabidhi mitungi hiyo kwa Wizara ya Nishati leo Aprili 21,2026 katika kongamano la Mama na Baba Lishe lililofanyika jijini Dar es Salaam ambapo mgeni rasmi alikuwa Rais Dk.Samia Suluhu Hassan.

Katika kongamano hilo Rais Samia alikabidhi mitungi hiyo ya Oryx kwa Mama na Baba Lishe ikiwa ni ishara ya kuhamasisha mabadiliko kutoka matumizi ya nishati za jadi kama mkaa na kuni kwenda kwenye matumizi ya gesi safi na yenye ufanisi zaidi.

Katika hotuba yake Rais Dk.Samia pia alisisitiza muhimu wa nafasi ya mama lishe na baba lishe katika kukuza uchumi wa nchi na kuhakikisha upatikanaji wa chakula bora kwa  wananchi.

Rais Samia aliwapongeza wadau wote walioshiriki katika kongamano hilo wakiwemo Oryx Gas kwa kuendeleza matumizi ya teknolojia safi za kupikia nchini Tanzania.

Hata hivyo Oryx Gas Tanzania Limited awali katika kongamano hilo imeendesha mafunzo ya matumizi sahihi, matumizi bora ya gesi ya LPG ,viwango vya ubora, faida za kiuchumi, kimazingira pamoja na kiafya.Washiriki 5000 wamepatiwa mafunzo hayo wakati wa kongamano.

Mafunzo hayo yaliendeshwa na Meneja wa Mafunzo wa Oryx Gas Tanzania Limited, Bw. Peter Ndomba,

ambapo ametumia nafasi hiyo kueleza kuwa Oryx inajisikia fahari kuratibu mafunzo hayo makubwa na kuthibitisha kuendelea kutekeleza mipango kama hiyo nchi nzima. 

“Kampuni inalenga kuendelea kusaidia wauza chakula kutumia nishati safi, kuboresha maisha yao, na kuchangia katika malengo ya kitaifa ya uhifadhi wa mazingira na maendeleo endelevu.

“Tukio hili la kihistoria linaonesha dhamira ya Tanzania katika kukuza uchumi shirikishi, kuboresha afya ya jamii, na kuharakisha mpito kuelekea matumizi ya nishati endelevu.”

Mwisho.