Morogoro. Amani na utulivu ni msingi mkuu wa ustawi wa jamii yoyote inayotamani kufikia maendeleo ya kweli na endelevu. Katika mazingira yenye uvumilivu na kuheshimiana, shughuli za kiuchumi, kijamii na kisiasa hupata nafasi ya kustawi kwa ufanisi.
Taifa lisilo na amani hukosa dira, hupoteza rasilimali zake na kudhoofisha matumaini ya wananchi wake. Ndiyo maana Tanzania imeendelea kujivunia urithi wa amani tangu enzi za waasisi wake, urithi unaopaswa kulindwa na kuendelezwa kizazi hadi kizazi.
Katika mfumo wa vyama vingi, tofauti za kisiasa ni jambo la kawaida. Hata hivyo, namna ya kusimamia tofauti hizo ndiyo kipimo halisi cha ukomavu wa kisiasa.
Kauli, vitendo na mienendo ya viongozi pamoja na wananchi vina nafasi kubwa katika kulinda au kuvuruga hali ya amani. Ni muhimu kutambua kuwa jukumu la kulinda amani si la vyombo vya dola pekee, bali ni la kila mwananchi. Kuanzia katika familia hadi ngazi ya taifa, misingi ya uvumilivu, haki na usawa inapojengwa imara, huimarisha mshikamano wa kitaifa.
Katika nyakati nyeti za kisiasa, viongozi wanabeba wajibu mkubwa wa kuwa mfano wa kuigwa. Kauli zao zinapaswa kujenga matumaini badala ya kuchochea taharuki.
Vivyo hivyo, wananchi wanapaswa kushiriki kwa uwajibikaji katika michakato ya kidemokrasia bila kuvunja misingi ya amani na utulivu.
Akizungumzia nafasi ya amani katika maendeleo ya Tanzania alipozungumza na Mwananchi hivi karibuni, mwanasiasa mkongwe nchini, Hamad Rashid Mohammed anasisitiza kuwa ustawi wa jamii hauwezi kujengwa bila kuwapo kwa hali ya utulivu.
Anabainisha kuwa amani si anasa, bali ni hitaji la msingi katika maisha ya kila siku ya binadamu. Anasema bila amani, haiwezekani kutekeleza shughuli yoyote yenye tija kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Kwa mtazamo wake, hata mataifa yaliyoendelea yamefanikiwa kufikia hatua hiyo kutokana na kujenga misingi imara ya utulivu kwa muda mrefu. Hivyo, Tanzania inapaswa kuendelea kujifunza na kulinda mafanikio yake katika eneo hilo.
Anaonya kuwa kukosekana kwa amani kunaathiri siasa na uchumi kwa kiwango kikubwa, kwa sababu wananchi hukosa mazingira ya kufanya kazi na kujiongezea kipato, hali inayolikosesha taifa uwezo wa kusonga mbele.
Kwa mujibu wa kiongozi huyo, mataifa yaliyokumbwa na migogoro mara nyingi hupoteza mwelekeo wa maendeleo, huku wananchi wake wakibaki katika hali ngumu ya maisha. Hali hiyo inaonyesha wazi kuwa gharama ya kukosekana kwa amani ni kubwa mno kwa taifa lolote.
Aidha, anatahadharisha dhidi ya kuichukulia amani kama ajenda ya msimu, hasa wakati wa uchaguzi. Anasisitiza kuwa amani inapaswa kupewa kipaumbele wakati wote.
Anakumbusha kuwa matukio ya vurugu yaliyowahi kutokea yameacha majeraha makubwa kwa wananchi, yakiwamo kupoteza maisha na mali, hali inayopaswa kuepukwa kwa gharama yoyote.
Anasisitiza kuwa migogoro haiwezi kutatuliwa kwa njia za vurugu, bali kupitia mazungumzo na maridhiano. Kwa mtazamo wake, busara ni kuanza na majadiliano kabla ya hali haijawa mbaya, badala ya kusubiri madhara yatokee ndipo hatua zichukuliwe.
Akirejea matukio ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, anabainisha kuwa katika michakato mikubwa, makosa hayaepukiki.
“Hata hivyo, kinachohitajika ni utayari wa kuyatambua na kuyarekebisha kwa wakati kwa sababu kurudia makosa bila kuyatafutia ufumbuzi kunaweza kusababisha wananchi wakakata tamaa na kupunguza imani yao kwa mifumo ya kidemokrasia nchini,” anasema Hamad.
Kwa mantiki hiyo, anasisitiza umuhimu wa uwajibikaji kwa kila mhusika na haja ya kurejesha imani ya wananchi kwa taasisi za umma kupitia uwazi na haki. Huu ndiyo msingi wa kudumisha amani na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Kwa jumla, amani na utulivu si tu nguzo ya maendeleo, bali pia ni dhamana ya pamoja inayohitaji ushirikiano wa kila mmoja. Taifa linapolinda amani yake, linajenga mazingira thabiti ya ustawi wa wananchi wake na kufungua milango ya maendeleo endelevu. Tanzania ina kila sababu ya kuendelea kuithamini na kuilinda tunu hii adhimu kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.
Kwa upande wake, Magdalena Sakaya aliyewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF) kwa muda mrefu, anaweka bayana kuwa amani ni sharti lisiloepukika katika safari ya maendeleo ya taifa lolote lile. Anasisitiza kuwa hakuna taifa linaloweza kusonga mbele bila uwepo wa utulivu wa kisiasa na kijamii.
Akitoa mifano ya baadhi ya nchi za Afrika zilizokumbwa na migogoro ya muda mrefu, Sakaya anabainisha kuwa hali hiyo imeathiri kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wao.
Kwa mujibu wake, mazingira yasiyo na amani huondoa fursa muhimu za kiuchumi, ikiwamo uwekezaji na utalii, huku rasilimali nyingi zikielekezwa katika kushughulikia migogoro badala ya kuendeleza sekta za uzalishaji. “Hakuna uwekezaji, hakuna utalii bila amani. Uchumi unakwenda kwenye vita badala ya maendeleo,” anasisitiza.
Akizungumzia uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 29, 2025, Sakaya ambaye aliwania ubunge jimbo la Kaliua mkoani Tabora, anaeleza wasiwasi wake kuhusu mwenendo wa mchakato wa kidemokrasia.
Anadai kuwa kasoro zilizojitokeza zilichangia kuzalisha hali ya sintofahamu na hasira miongoni mwa wananchi.
Kwa mtazamo wake, kukosekana kwa ushindani wa haki na huru kunadhoofisha misingi ya demokrasia na kunaweza kuchochea migogoro kwa wananchi.
Anasisitiza kuwa mamlaka ya uongozi hutokana na ridhaa ya wananchi, hivyo ni muhimu kwa viongozi kuheshimu sauti na maoni yao. “Utawala unatoka kwa wananchi, si kitu cha kushushwa kutoka mbinguni,” anasema, akitoa wito kwa viongozi kuepuka kiburi na kujenga utamaduni wa kusikiliza.
Aidha, anasisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa wananchi katika uamuzi wa kisera na kiutawala. Kwa mujibu wake, kukosekana kwa utamaduni huo kunazalisha makundi yenye hisia za kutengwa na chuki, hali ambayo ni hatari kwa mshikamano wa kitaifa. Anasisitiza kuwa amani ya kudumu haiwezi kupatikana bila kuwapo kwa haki na usawa ndani ya mifumo ya uongozi, ambayo ndiyo msingi wa kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za taifa.
Akichambua mizizi ya migawanyiko ya kisiasa, Coster Kibonde, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia Makini, anasema mara nyingi migogoro huanzia kwenye maslahi binafsi na ukosefu wa ushirikishwaji katika vyama vya siasa.
Kwa mujibu wake, viongozi wanaposhindwa kushirikiana katika kufanya uamuzi, hujenga mazingira ya mpasuko unaoweza kuathiri hata mshikamano kwa ujumla.
Hivyo, anatoa wito kwa viongozi kuwa makini na lugha wanazotumia, akisisitiza kuwa wanapaswa kuwaunganisha wananchi badala ya kuwagawa. Anaonya kuwa wananchi huamini kauli za viongozi, hivyo ni lazima wachuje maneno yao ili yasichochee vurugu.
Aidha, anaona maridhiano ya kitaifa kuwa hatua muhimu katika kuponya majeraha ya kisiasa na kurejesha imani ya wananchi.
Kwa upande mwingine, Mwanajuma Noty anaangazia uhusiano wa moja kwa moja kati ya amani na ukuaji wa uchumi, akibainisha kuwa maendeleo hayawezi kupatikana katika mazingira ya migogoro.
Anasisitiza kuwa athari za vurugu huwakumba zaidi wananchi wa kawaida, hasa wanawake na watoto ambao mara nyingi huwa waathirika wakubwa. Hivyo, anahimiza utolewaji wa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda amani na kuenzi utaifa, huku akionya dhidi ya kuruhusu tofauti za kisiasa kuvuruga mshikamano wa kitaifa.
Kwa mtazamo wake, wanawake wanayo nafasi muhimu katika kujenga maridhiano kutokana na mchango wao wa kihistoria katika harakati za kijamii.
Akitoa mtazamo wa kijinsia katika siasa, Dorith Semu Kiongozi wa ACT-Wazalendo anasema wanawake bado wanakabiliwa na changamoto nyingi katika ushiriki wa kisiasa, hasa katika mazingira yenye migogoro.
Anasema mifumo mingi haijawa rafiki kwao hali inayosababisha sauti zao kutosikika ipasavyo. Anasisitiza kuwa ushiriki wa wanawake katika uamuzi ni muhimu si tu kwa usawa wa kijinsia, bali pia kwa kuimarisha amani na mshikamano wa jamii.
Kwa mtazamo wa mwananchi wa kawaida, Yusuf Kitogota anasema kulinda amani ni jukumu la kila mmoja.
Kitogota anasisitiza umuhimu wa viongozi kutenda haki kwa kuzingatia katiba na sheria, huku wananchi wakionyesha uvumilivu na kuepuka kushawishika na propaganda za kisiasa. Anaongeza kuwa vijana wanapaswa kupewa elimu ili kuepuka kutumika katika vurugu, kwa kuwa mustakabali wa taifa unategemea ushirikiano wa jamii nzima.
Katika muktadha wa dini, Sheikh Mussa Kundecha anasisitiza kuwa viongozi wa dini pia wana nafasi muhimu katika kuzuia migogoro. Kupitia mahubiri na mawaidha, wanaweza kuwaandaa waumini kukabiliana na tofauti za kiitikadi na hivyo kuimarisha umoja wa kitaifa. Sheikh Kundecha anasema taasisi za dini zinapaswa kuzingatia zaidi hatua za kinga kwa kushughulikia vyanzo vya migogoro mapema. Kwa mtazamo wake, hali ya amani iliyopo nchini inaridhisha, lakini bado kuna haja ya kuendelea kuielimisha jamii ili kuifanya iwe imara na endelevu zaidi.
Kwa upande wake, Askofu mstaafu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Method Kilaini ameeleza wazi kuwa viongozi wa dini wanayo nafasi muhimu katika kuzuia na kuzima migogoro kabla haijachukua mawanda mapana. Anasisitiza kuwa jukumu la kwanza la kiongozi wa dini ni kupunguza munkari na kuwapa waumini utulivu wa fikra wanapokabiliwa na changamoto mbalimbali za kijamii na kisiasa. Kwa mtazamo wake, viongozi hao wanapaswa kuhakikisha waumini wao hawachukuliwi na jazba katika kushughulikia masuala nyeti.
Aidha, ameongeza kuwa viongozi wa dini wanatakiwa kuwa na uwezo wa kubaini viashiria vya migogoro mapema na kuchukua hatua za haraka kutafuta suluhu.
Anasisitiza umuhimu wa kushughulikia chanzo cha tatizo kabla halijakua na kuleta madhara makubwa kwa wananchi. Kwa mujibu wake, hatua za mapema zinaweza kuzuia hali inayoweza kuvuruga mshikamano wa kijamii na kuathiri amani ya taifa.
Askofu Kilaini pia ameweka mkazo katika ushirikishwaji wa wananchi katika kutafuta suluhu za changamoto zinazowakabili.
Anasema majibu ya kudumu hayawezi kupatikana kwa uamuzi wa mtu mmoja, bali yanahitaji ushiriki wa wale wanaoathirika moja kwa moja. Ushirikishwaji huo, anasema hujenga uelewa mpana na kuongeza uwezekano wa kupatikana kwa suluhu endelevu.
Akizungumzia matumizi ya mitandao ya kijamii, ameonya kuwa majukwaa hayo yameanza kutumika vibaya na baadhi ya watu, hali inayochochea upotoshaji wa taarifa na kuzalisha hofu miongoni mwa wananchi.
Amebainisha kuwa matumizi ya majina bandia na usambazaji wa taarifa zisizo na uhakika ni hatari kwa utulivu wa jamii.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa suluhisho si kupiga marufuku mitandao hiyo, bali kuwawajibisha wale wanaoitumia vibaya ili iwe fundisho kwa wengine.
