Baba aliyefungwa maisha kwa kumbaka, kumlawiti mwanaye aachiwa

Arusha. Mahakama Kuu, Masijala Ndogo ya Tanga, imebatilisha hukumu ya kifungo cha maisha jela aliyokuwa amehukumiwa baba baada ya kukutwa na hatia ya kumbaka na kumlawiti mtoto wake wa kike aliyekuwa na umri wa miaka tisa.

Baba huyo, mkazi wa eneo la Kilole wilayani Korogwe, Tanga, alidaiwa kumbaka na kumlawiti binti yake aliyekuwa na umri wa miaka tisa kwa nyakati tofauti katika kipindi cha miaka miwili, kati ya mwaka 2023 hadi Mei 4, 2025.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi huo baada ya kubaini ushahidi wa mashtaka ulikuwa wa mashaka na wenye upungufu mkubwa, ikiwa ni pamoja na ushahidi wa mwathirika ambao haukuwa wa kuaminika na haukuweza kuthibitisha hatia bila shaka yoyote.

Uamuzi uliomuachia huru baba huyo mkazi wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga umetolewa Aprili 10, 2026 na Jaji Hapiness Ndesamburo, aliyekuwa akisikiliza rufaa hiyo iliyokatwa na baba huyo akipinga uamuzi wa Mahakama ya Wilaya ya Korogwe.

Jaji Ndesamburo amesema Mahakama inamuachia huru mrufani huyo baada ya kuridhika kuwa ushahidi uliotolewa dhidi yake haukuthibitisha makosa ya ubakaji na ulawiti kama inavyotakiwa kisheria. Pia ilibatilisha fidia ya Sh milioni moja aliyopaswa kumlipa mwathirika wa tukio hilo.

Baba huyo alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Korogwe akikabiliwa na makosa mawili; la kwanza likiwa ni ubakaji kinyume na kifungu cha 130(1) na (2)(e) vikisomwa kwa pamoja na kifungu cha 131(3) cha Kanuni ya Adhabu.

Kosa la pili lilikuwa ni ulawiti kinyume na kifungu cha 154(1)(a) na (2) vya Kanuni hiyo, ambapo alidaiwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2023 hadi Mei 4, 2025, katika eneo la Kilole wilayani Korogwe, alitenda makosa hayo.

Katika kuthibitisha kesi hiyo, upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi watano akiwemo mwathirika mwenyewe (shahidi wa tatu), ambaye alidai kuwa mrufani alimfanyia vitendo vya ubakaji na ulawiti mara kwa mara kwa kipindi cha takribani miaka miwili.

Alidai kuwa baba yake alikuwa akimvuta chumbani kwake na kumpa vinywaji vyenye dawa za kulevya, kisha kuzima taa na kumfanyia vitendo hivyo huku akimtishia kumuua iwapo angemweleza mama yake.

Alidai Mei 4, 2025, mrufani na rafiki zake walimbaka na kumlawiti, hali iliyomfanya ashindwe kutembea vizuri. Ndipo alilazimika kumweleza Mwenyekiti wa Mtaa huo, ambaye alikuwa shahidi wa tano katika kesi hiyo, aliyeshuhudia usaha katika sehemu za siri za mtoto huyo na kuamua kuripoti tukio hilo.

Mwathirika huyo alipelekwa Kituo cha Afya Majengo, ambapo shahidi wa pili, ambaye ni ofisa kliniki, alishuhudia kuwa alibaini michubuko katika sehemu za siri za mtoto huyo pamoja na sehemu ya haja kubwa, ambayo misuli yake ilikuwa imelegea, huku akiwa na magonjwa ya zinaa.

Shahidi wa nne, ambaye ni bibi mkubwa wa mtoto huyo, alidai kuwa Mei 5, 2025 alimwona mjukuu wake akikimbilia chooni mara kwa mara, ndipo alipomuuliza na kumweleza kuwa amebakwa na kulawitiwa.

Katika kesi hiyo, mrufani pekee ndiye alikamatwa huku washukiwa wengine wakidaiwa kukimbia.

Katika utetezi wake, baba huyo alidai kesi hiyo ilikuwa ya uongo na kuwa chanzo chake kilikuwa ni mgogoro wa kifamilia ulihusisha fedha baada ya kutengana na mkewe.

Licha ya utetezi huo, mahakama hiyo ya chini ilimkuta na hatia na kumhukumu adhabu ya kifungo cha maisha jela.

Katika rufaa hiyo, mrufani alikuwa na sababu tatu, ikiwemo kuwa Hakimu alikosea kumtia hatiani na kumhukumu bila kuzingatia utetezi wake; alikosea kumtia hatiani kwa msingi wa ushahidi unaokinzana; na alifanya makosa kumtia hatiani kwa makosa ambayo hayajathibitishwa bila kuacha shaka.

Wakili wa mrufani alidai kuwa kesi hiyo ilikuwa ya kubuniwa kutokana na migogoro ya kifamilia kati ya mrufani na mama wa mwathirika. Alisisitiza kuwa hapakuwa na ushahidi wa moja kwa moja wala shahidi huru aliyemuunganisha mrufani na tukio hilo.

Kwa upande wake, Wakili wa Serikali alipinga rufaa hiyo akieleza kuwa mahakama ya awali ilifanya uchambuzi wa kina wa ushahidi na kufikia uamuzi sahihi. Alisisitiza kuwa ushahidi wa mwathirika uliungwa mkono na vielelezo vya kitabibu, hivyo kuthibitisha kuwepo kwa makosa hayo.

Jaji Ndesamburo amesema baada ya kuzingatia hoja za pande zote mbili na kumbukumbu zilizoko mahakamani, masuala yaliyozingatiwa ni iwapo makosa hayo yalithibitishwa, iwapo ushahidi ulikuwa dhaifu na unaokinzana, na iwapo mahakama haikuzingatia utetezi wa mrufani.

Jaji amesema hoja kuu ilikuwa kama upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha vipengele muhimu vya makosa hayo, ambavyo ni umri wa mwathirika, uwepo wa kupenya, na utambulisho wa mtuhumiwa.

Mahakama ilikubaliana kuwa umri wa mwathirika ulithibitishwa ipasavyo kuwa alikuwa na miaka tisa wakati wa tukio. Pia ilikiri kuwa kulikuwa na ushahidi wa kitabibu unaoashiria uwepo wa kupenya.

Hata hivyo, Jaji Ndesamburo alionyesha mashaka makubwa kuhusu uaminifu wa ushahidi wa mwathirika, hasa kutokana na kuwepo kwa maelezo yanayokinzana na yasiyoendana na hali halisi.

Katika uchambuzi wake, Jaji alieleza kuwa mwathirika alidai kupoteza fahamu baada ya kupewa dawa za kulevya, lakini bado aliweza kutoa maelezo ya kina kuhusu matukio yaliyotokea, jambo lililozua shaka juu ya ukweli wa ushahidi wake.

Aidha, mahakama ilibaini mkanganyiko katika ushahidi kuhusu iwapo mwathirika aliwahi kumweleza mtu yeyote kuhusu tukio hilo, kwani kwa upande mmoja alidai hakusema chochote kutokana na vitisho, lakini pia alidai alimweleza mama yake.

Mahakama pia iliona kuwa baadhi ya maelezo yaliyotolewa na mwathirika yalikuwa ya kushangaza na yasiyoendana na uhalisia, ikiwemo madai ya kubakwa na watu saba kwa wakati mmoja bila kuonyesha dalili kubwa za majeraha au kutoa taarifa kwa watu waliokuwa karibu.

“Ni msimamo uliowekwa kisheria kwamba katika makosa ya ngono, ushahidi wa mwathirika unachukuliwa kuwa wa kuaminika zaidi, ambapo mahakama inaweza kubaini uaminifu wa shahidi kwa kutathmini uthabiti wa ushahidi wake na kuuzingatia pamoja na ushahidi wa mashahidi wengine,” alisema Jaji.

Jaji Ndesamburo alieleza kuwa katika mazingira ya kawaida, tukio la aina hiyo lingetarajiwa kuacha athari kubwa zaidi za kimwili na kihisia tofauti na ilivyoonekana katika ushahidi uliowasilishwa.

Pia ilibainika kuwa mwathirika alidai kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa usiku peke yake licha ya madai kuwa alikuwa akinyanyaswa mara kwa mara, jambo ambalo mahakama iliona halina mantiki kwa mtoto wa umri huo.

“Ushahidi huu unaacha maswali fulani bila majibu na kutilia shaka uaminifu wa shahidi; kwa mfano, ni vigumu kuelewa jinsi mwathirika angeweza kukumbuka na kuelezea matukio yaliyodaiwa kutokea alipokuwa amepoteza fahamu kutokana na kupewa dawa za kulevya,” alisema Jaji.

“Kuhusu yaliyotangulia, naona upande wa mashtaka uliacha mapengo mengi muhimu bila kutatuliwa, jambo ambalo lilidhoofisha kesi yake na hivyo sioni haja ya kushughulikia sababu nyingine.

“Ni kanuni ya msingi katika sheria ya jinai kuwa endapo kuna shaka yoyote katika ushahidi wa upande wa mashtaka, shaka hiyo lazima itafsiriwe kwa faida ya mshtakiwa,” alisema Jaji katika hukumu hiyo.

Kutokana na hitimisho hilo, mahakama iliamua kuruhusu rufaa, kufuta hukumu na adhabu zote zilizotolewa na mahakama ya awali, pamoja na amri ya fidia, na kuamuru mrufani aachiliwe huru.