BoT yawapa elimu ya fedha wachimbaji wadogo

Mwanza. Licha ya wachimbaji wadogo wa madini kuingiza kipato kikubwa, imebainika kuwa sehemu kubwa ya fedha wanazopata huishia kwenye matumizi yasiyo na tija, hali inayochangia wengi wao kushindwa kupiga hatua za kimaendeleo.

Imeelezwa kuwa wachimbaji wengi hutumia mapato yao katika anasa, zikiwemo ulevi na starehe nyingine, badala ya kuweka akiba au kuwekeza katika miradi ya muda mrefu inayoweza kuwainua kiuchumi.

Wakizungumza leo Jumanne, Aprili 14, 2026 jijini Mwanza, baada ya kupatiwa elimu ya fedha na uwekezaji wa hati fungani (bondi) kutoka Benki Kuu ya Tanzania (BoT), baadhi ya wachimbaji wadogo wamesema changamoto kubwa inayowakabili ni ukosefu wa uelewa wa masuala ya kifedha na uwekezaji.

Mchimbaji mdogo, Ally Omary, amesema wachimbaji wengi hawana elimu ya matumizi sahihi ya fedha, hali inayosababisha wanapopata kipato hutumia sehemu kubwa katika matumizi yasiyo ya lazima.

“Wengi wetu hatuna elimu ya fedha. Tunapopata kipato, badala ya kuwekeza au kuweka akiba, tunatumia kwenye anasa, jambo linalotufanya tushindwe kupiga hatua,” amesema Omary.

Amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutolewa kwa elimu ya kifedha kwa wachimbaji wadogo ili kuwasaidia kubadili mtazamo na kutumia vizuri mapato yao kwa maendeleo endelevu.

“Sanasana kwenye ulevi, uzinzi ndio maana unakuta asilimia kubwa hawatoki…wanapopewa mshahara wote unaishia katika mambo ya starehe unakuta wachimbaji wadogo wadogo wenyewe ni wachache kutoka kimaisha,”ameeleza.

Mchimbaji mdogo wa madini wilayani Misungwi, Flora Maswe amesema wachimbaji wengu hutumia fedha bila mpangilio wakiamini watapata tena.

“Mchimbaji akishapata pesa anaitumia bila mpangilio akijua kesho atapata tena….anakaa siku moja au mbili fedha imeisha, kisha anarudi tena migodini kutafuta upya. Hii inafanya wengi wetu kubaki kwenye hali ileile kila wakati,” amesema.

Mchimbaji mwingine, Neema Tambi amesema jamii ya wachimbaji imegawanyika katika makundi tofauti kulingana na namna wanavyotumia kipato chao, wapo wanaotumia kwenye starehe na wengine kwenye maendeleo.

“Kuna wanaoponda raha na kuna wanaofanya maendeleo, mafunzo haya yametusaidia kuona umuhimu wa kupanga bajeti na kutumia fedha kwa malengo maalumu, unaamini tutakapokwenda kuwaelimisha wengine, kutakuwa na mabadiliko chanya,” amesema.

Mwenyekiti wa wachimbaji Mkoa wa Mwanza, Sabana Salinja amewahimiza wachimbaji kubadili mtazamo na kuanza kuheshimu fedha wanazozipata kwa kuzielekeza kwenye uwekezaji.

“Ni muhimu wachimbaji wakaweka akiba kwenye benki na pia, kuwekeza katika biashara nyingine, kama walivyowekeza kwenye migodi wanapaswa pia kuwekeza kwenye sekta tofauti ili kujihakikishia usalama wa maisha yao ya baadaye,” amesema.

Akizungumza katika mafunzo hayo, mchambuzi mwandamizi mkuu wa masuala ya fedha kutoka BoT, Fidelis Mkatte amesema wameamua kutoa elimu hiyo baada ya kubaini kuwa wachimbaji wengi wana kipato kikubwa, lakini hawana uelewa wa namna ya kukisimamia.

“Wengi wanaingia migodini na kupata fedha nyingi kwa wakati mmoja, lakini maarifa yao yanaishia kwenye uchimbaji pekee. Madini yanaweza kuisha, hivyo ni muhimu kuwa na uwekezaji mbadala utakaosaidia hata baada ya shughuli za uchimbaji kupungua au kusimama,” amesema.

Ameeleza kuwa miongoni mwa fursa wanazowahamasisha wachimbaji ni uwekezaji kwenye dhamana za Serikali, ikiwemo hati fungani na dhamana za muda mfupi, ambazo zina usalama mkubwa.

“Huu ni uwekezaji salama kwa sababu hauhusiani na hatari kubwa…unamwezesha mtu kuweka akiba na kupata faida kwa muda mrefu huku akiwa na uhakika wa fedha zake,” ameongeza.

Kwa upande wake, mchambuzi wa masuala ya fedha kutoka Kurugenzi ya masoko ya fedha BoT, Kennedy Mwasanga amesema benki hiyo pia inaendelea kuhamasisha wachimbaji kuuza madini yao, hususan dhahabu, kupitia mifumo rasmi.

Amesema BoT inanunua dhahabu kutoka kwa wachimbaji wakubwa na wadogo kupitia viwanda vya kuchakata, na malipo hufanyika ndani ya saa 24 baada ya taratibu kukamilika.

“Faida ya kuuza dhahabu BoT ni pamoja na punguzo la kodi ya mrabaha kutoka asilimia sita hadi nne, pamoja na kutolipia baadhi ya gharama nyingine kama VAT na inspection fee. Hii ni fursa muhimu kwa wachimbaji kuongeza kipato chao halali,” amesema.

Aidha, amesema hatua hiyo inalenga pia kudhibiti utoroshaji wa madini kwa kuhakikisha wachimbaji wanapata bei nzuri inayolingana na soko la kimataifa.

Kaimu Ofisa Madini Mkazi Mkoa wa Mwanza, Elinami Kimaro amesema elimu hiyo ni muhimu katika kuwasaidia wachimbaji kuelewa thamani ya rasilimali walizonazo na namna ya kuzitumia kwa maendeleo endelevu.

Amesema Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ya uchimbaji, ikiwemo kutoa elimu kwa wachimbaji pamoja na kuwahamasisha taasisi za kifedha kuielewa sekta ya madini ili iwe rahisi kutoa mikopo.

Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya fedha na uwekezaji kwa wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Mwanza.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Amir Mkalipa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda amesema mkoa huo una jumla ya leseni ndogo za uchimbaji 1,552, ambapo kati ya hizo 846 ni za madini ya dhahabu.

Amesema madini yanayochimbwa mkoani humo ni pamoja na dhahabu, almasi, madini ya viwandani na madini ya ujenzi, akisisitiza umuhimu wa wachimbaji kutumia vyema fursa hiyo kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.