Dar es Salaam. Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, imemhukumu muosha magari, John Mpali (35), kifungo cha nje cha miezi miwili, baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa fedha taslimu Sh110,000 ziizokuwa ndani ya gari, mali ya Mohamed Ango.
Mpali aliiba fedha hizo, wakati akiosha gari la Ango.
Pia Mahakama hiyo imemwamuru mshtakiwa huyo, kumrudishia mlalamikaji wa kesi hiyo, kiasi hicho cha fedha alichoiba, ifikapo Mei 13, 2026.
Hukumu hiyo ilitolewa leo Aprili 14, 2026 na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Mpoki Mwabela, baada ya mshtakiwa kukiri shtaka hilo, aliposomewa kwa mara ya kwanza.
“Kwa sababu mshtakiwa amekiri mwenyewe na hakutaka kuisumbua mahakama, hivyo ninamhukumu adhabu ya kifungo cha nje cha miezi mwili na kiasi cha fedha alichoiba anatakiwa amrudishie mlalamikaji ifikapo Mei 13, 2026” alisema Hakimu Mwabela.
Hata hivyo, kabla ya kutolewa adhabu hiyo mshtakiwa aliomba mahakama impunguzie adhabu kwani ni kosa lake la kwanza na yuko tayari kumrudishia mlalamikaji kiasi hicho cha fedha.
Hakimu Mpoki, baada ya kusikiliza hoja hiyo, alimhukumu mshtakiwa kifungo cha nje miezi miwili.
Katika kesi ya msingi, mshitakiwa alitenda kosa hilo Aprili 1, 2026 eneo la Posta, Mtaa wa Azikiwe, Dar es Salaam.
Mshtakiwa aliiba Sh110,000 zilizokuwa ndani ya gari la Ango, alipopewa kuliosha.
