Matumaini ahueni gharama za maisha mikononi mwa Dk Mwigulu

Dodoma. Matumaini ya wananchi kusikia hatua zitakazochukuliwa na Serikali kuwapunguzia gharama za maisha baada ya kupanda kwa bei ya mafuta, yanaelekezwa kwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kesho.

Mzigo wa matumaini hayo kwa Dk Mwigulu, unatokana na ukweli kwamba, Jumatano ya Aprili 15, 2026, mtendaji mkuu huyo wa Serikali, atahitimisha hoja ya mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Anatajwa tumaini, kwa sababu hitimisho lake hilo litakalomalizika kesho, linakuja wakati ambao, yameshatolewa mapendekezo lukuki na wabunge na wadau wengine, kuhusu hatua za kuchukua kuwapunguzia wananchi gharama za maisha.

Sio hivyo tu, hotuba hiyo inakuja kipindi ambacho Serikali na Dk Mwigulu mwenyewe, wameshatoa ahadi mara kadhaa kwamba wapo katika hatua za mwisho za kutangaza uamuzi wa Serikali, kulikabili hilo.

Mbali na wadau vikiwemo vyama vya siasa kama Chadema, ACT-Wazalendo kutaka kuwekwe ruzuku, chama tawala, Chama cha Mapinduzi (CCM) nacho kimeielekeza Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa ruzuku na kuhamasisha kupunguzwa matumizi ya mafuta katika ofisi za umma.

“Chama kinaielekeza wizara kuangalia namna ya kutoa ruzuku kama ambavyo Rais alifanya mwaka 2022 alipotoa zaidi ya Sh100 bilioni kuleta unafuu kwa wananchi wetu waendelee kufurahia matunda kwenye nchi yao.”

Hayo yalisemwa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Kenan Kihongosi, Aprili 7, 2026 alipozungumza na waandishi wa habari wakati akitoa maelekezo ya chama kwa Serikali.

Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya siasa na uchumi, wanaona hotuba ya Dk Mwigulu, ni fursa kwa Serikali kutegua kitendawili cha udhibiti wa athari za kupanda kwa bei ya mafuta.

Kiu za kusikia hatua hizo, inatokana na kupanda kwa bei ya mafuta, kutokana na vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati vikihusisha mataifa ya Marekani, Israel dhidi ya Iran na kusababisha kupanda kwa gharama za maisha duniani.

Bado hakuna matumaini ya ahueni kuhusu hali hiyo, kutokana na kukwama kwa juhudi za mazungumzo kati ya pande zinazohasimiana, hivyo upo uwezekano wa vita kuendelea na bei ya mafuta kuendelea kupanda duniani.

Katika hotuba yake Aprili 1, 2026 akiwasilisha bajeti, Dk Mwigulu aliliomba Bunge limuidhinishie bajeti ya Sh12.5 trilioni kwa ajili ya ofisi yake na wizara zilizo chini yake itakayotumika katika kipindi cha mwaka wa fedha 2026/27.

Juzi Jumapili, Dk Mwigulu akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Mvumi Mision, akiwa kwenye ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani Chamwino, Dodoma, aligusia suala hilo la mafuta.

Dk Mwigulu aliwataka Watanzania kuendelea kuwa watulivu na kwamba Serikali inafuatilia kwa karibu na kwa umakini suala la mafuta na kuhakikisha yanaendelea kupatikana nchini ili shughuli za uzalishaji na usafirishaji zisiathirike.

Alisema suala la upatikanaji wa mafuta si jambo la kuamuliwa na nchi moja kwa sababu si kila nchi ni muagizaji au mzalishaji wa bidhaa hiyo.

“Niwahakikishie Serikali inafuatilia na kila siku kuna vikao tunakaa vya sekta mbalimbali kuweza kuhakikisha bidhaa hii haiadimiki na tunashughulika na masuala ya bei ya bidhaa na bei ya huduma,” alisema.

Mmoja wa viongozi waandamizi serikalini aliyeomba hifadhi ya jina lake amesema mapendekezo yamekwisha kutolewa kutoka kila kona na sasa: “Kinachosubiriwa ni PM (waziri mkuu) kuwaeleza sasa Watanzania wanapataje unafuu kama waliofanyiwa wananchi wa Namibia, Zambia na kwingineko kwa kuondolewa tozo.”

Nchi hizo za Namibia na Zambia zimetangaza kupunguza tozo kwa kipindi cha dharura ili kupunguza machungu kwa wananchi.

“Hapa kwa sasa tumsubiri tu waziri mkuu siku anahitimisha mjadala wake atasema nini. Wabunge waling’aka, chama chake (CCM) kimetoa maelekezo, hakuna anavyoweza kuacha na akisema asiseme nafuu ambayo wananchi wanasubiri, hawezi kueleweka,” amesisitiza kiongozi huyo.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametangaza kubana matumizi akisema misafara yake itakuwa na magari machache na wengine watabebwa kwenye mabasi madogo.

Mjadala wa bajeti hiyo, uligubikwa na hoja sita, zikiwemo kupanda kwa bei ya mafuta, uwajibikaji wa mawaziri wenye majibu yasiyo na tija, umaliziaji wa maboma kabla ya miradi mipya na agizo la Bunge kwa wakurugenzi wa halmashauri ambazo hazikuchukua dawa za kuua vimelea vya mbu.

Mbali na hoja hizo, kilio dhidi ya wapigaji kiliibuliwa pia bungeni humo. Lakini, suala la mafuta ndilo linalosubiriwa kwa hamu, kwa sababu iliahidiwa linakwenda kufanyiwa kazi na Waziri Mkuu mwenyewe na hata Spika wa Bunge, Mussa Zungu alitoa agizo la jambo hilo kutafutiwa dawa.

Agizo la Zungu, liliikutanisha Kamati ya Bunge ya Nishati, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi na Waziri Mkuu mwenyewe na vikao vilifanyika hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, lakini yaliyojadiliwa hayakuwekwa hadharani.

Majibu ya Waziri Mkuu pia yataangaliwa kwenye ubanaji wa matumizi ikiwemo aina ya magari hoja iliyoibuliwa na Mbunge wa Nyasa (CCM), John Nchimbi.

Nchimbi alieleza kuwepo matumizi mabaya ya Serikali katika ununuzi wa magari yenye gharama kubwa ambayo yanaumiza kodi ya wananchi.

“Mfano Mkurugenzi wa hapa Dodoma, hivi ana kazi gani ya kulazimika kutumia V8 wakati shughuli zake ni za hapa jirani, tunaisababishia Serikali kuwa na matumizi makubwa na wakati huo utakuta madereva wanaacha magari yakiunguruma kutwa nzima, lazima tubane matumizi,” alisema Nchimbi.

Hoja ya kuvuja kwa mapato ya Serikali iliibuliwa na wabunge Erick Shigongo, Kangi Lugola, Ahmed Shabiby na Mwita Waitara wote wakieleza namna ambavyo fedha zinaliwa na wajanja, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa na hivyo kuwafanya wachotaji waendelee.

Michango ya wabunge katika hotuba ya Waziri Mkuu iliacha maswali huku baadhi wakimtega kuhusu ufuatiliaji wa maagizo na maelekezo anayotoa kwenye ziara zake, lakini wengi walipendekeza kupunguzwa kwa baadhi ya tozo kwenye mafuta.

Baada ya hitimisho hilo, zitafuata Wizara zilizo chini ya Ofisi ya Rais ambapo, Aprili 16 ni Uwekezaji na Mipango. Aprili 17, ni Wizara ya Utumishi na Utawala Bora ambayo ndiyo itakuwa na mjadala wa ajira. Zote zitajadiliwa kwa siku mojamoja.

Mmoja wa walimu tarajali waliofanya usaili mwishoni mwa mwaka jana, Emmanuel Charles, alisema matumaini ya kupata ajira kwa kundi lao yanaendelea kufifia kutokana na kucheleweshwa mara kwa mara bila maelezo ya kina.

Emmanuel alieleza kuwa, licha ya kuendelea kuambiwa wavute subira, bado wanashuhudia matangazo mapya ya ajira yakitolewa, jambo linalozua maswali na sintofahamu miongoni mwao.

Alisema ndani ya makundi yao ya mawasiliano, vijana waliofanya usaili huo wamekuwa wakijadiliana na kujiuliza sababu ya ucheleweshaji huo, hasa ikizingatiwa kuwa awali waliarifiwa kuwa wangeanza kazi Januari 2026.

Hata hivyo, muda huo uliahirishwa hadi Machi, kabla ya kusogezwa tena mbele kwa mwezi mmoja zaidi.

Kutokana na hali hiyo, Emmanuel alisema sasa wanasubiri kwa hamu kauli rasmi ya waziri inayotarajiwa kutolewa wiki hii, ili kupata ufafanuzi juu ya hatma ya ajira zao.

Mbunge wa Ukonga, Bakari Shingo, alisema kuwa siyo rahisi kwa Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine duniani kuajiri kila kijana anayehitimu elimu ya juu, akieleza kuwa uwezo huo haupo katika mazingira ya sasa ya kiuchumi.

Alisisitiza kuwa badala ya kutegemea ajira rasmi pekee, kuna haja kwa Serikali kuweka mkazo katika kuwajengea vijana uwezo wa kujitegemea kupitia ujasiriamali na stadi za vitendo zitakazowawezesha kujiajiri.

Shingo, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati ya Bunge inayoshughulikia masuala ya elimu, alisema changamoto kubwa inaendelea kujitokeza katika mfumo wa mitaala ya elimu nchini, ambao bado unajenga dhana kuwa kila mhitimu wa chuo kikuu anapaswa kuajiriwa.

Alibainisha kuwa mtazamo huo siyo halisi katika soko la ajira la sasa, hivyo kuna umuhimu wa kuifanyia maboresho mitaala hiyo ili iendane na mahitaji halisi ya uchumi na kuwawezesha wahitimu kuwa wabunifu na kujitegemea.

“Ni kweli, vijana wengi watasubiri siku ya hotuba kusikia Serikali imetoa vibali vingapi vya ajira na mambo mengine, lakini kwangu naona siyo jambo jema kuwa na fikra za namna hiyo, huu ni wakati wa sisi kujikita kujenga uwezo wa masomo yatakayowapeleka vijana kwenye kujiajiri wenyewe,” alisema Shingo.