Sababu wenye ualbino kutaka ongezeko bajeti ya elimu, afya

Mwanza. Watu wenye ualbino wameiomba Serikali kuongeza bajeti ya huduma za elimu na afya kwa watoto wenye ualbino kuelekea mwaka wa fedha 2026/27, wakitaja sababu ya ombi hilo kuwa ni changamoto wanazokumbana nazo ikiwemo uhaba wa vifaa kinga, upungufu wa huduma za afya ya ngozi na mazingira yasiyo rafiki ya kujifunzia shuleni.

Akitoa ombi hilo kwa niaba ya wenzake, Mwenyekiti wa Chama cha Watu Wenye Ualbino Mkoa wa Mwanza (TAS), Masumbuko Marco amesema bado kuna pengo kubwa kati ya mahitaji halisi ya huduma na bajeti inayotengwa, jambo linaloathiri moja kwa moja maisha na maendeleo ya watoto wenye ualbino.

Amesema kupitia mradi wa Kesho Ang’avu kwa Watoto wenye Ualbino unaotekelezwa kwa kushirikiana na ActionAid Tanzania katika wilaya za Kwimba na Misungwi, wamebaini changamoto zinazoendelea kujirudia katika sekta za afya na elimu.

“Kupitia afua hizi, Chama kinatoa wito kwa Serikali kuongeza uwekezaji wa bajeti katika huduma rafiki za elimu na afya kwa watoto wenye ualbino, ili kuhakikisha wanapata haki sawa na fursa stahiki za maendeleo kuelekea mwaka wa fedha 2026/27,”amesema Marco.

Alieleza kuwa katika sekta ya afya, watoto wenye ualbino wanakosa vifaa muhimu vya kujikinga na mionzi ya jua ikiwemo mafuta kinga, kofia pana na miwani, hali inayowaweka katika hatari kubwa ya kupata saratani ya ngozi.

Alisema vituo vingi vya afya vinakabiliwa na uhaba wa vifaa tiba pamoja na upungufu wa wataalamu wa ngozi, jambo linalosababisha wagonjwa kuchelewa kupata huduma au kusafiri umbali mrefu kufuata matibabu.

Katika sekta ya elimu, Marco alisema watoto wenye ualbino wanakumbana na changamoto za ukosefu wa walimu wenye ujuzi wa kuwahudumia pamoja na uhaba wa vifaa vya kujifunzia vinavyokidhi mahitaji yao, hususan vitabu vyenye maandishi makubwa vinavyowasaidia wenye uoni hafifu.

Akizungumzia hali hiyo, Mchagizi wa mradi wa Kesho Ang’avu kwa watoto wenye Ualbino kutoka ActionAid Tanzania, Yusuph Bwango alisema mazingira ya kujifunzia bado si rafiki, jambo linalochangia baadhi ya watoto kushindwa kumaliza elimu ya msingi na kuendelea na sekondari.

“Ukiangalia takwimu zilizopo, kati ya watoto 10 wenye ualbino wanaoanza shule ya msingi, ni takribani nusu pekee wanaofanikiwa kumaliza, na wachache zaidi huendelea hadi sekondari. Miongoni mwa changamoto kubwa ambazo zinawakumba watoto wetu kutofanya vizuri ni kukosa miundombinu wezeshi ya kuwafanya waweze kusoma vizuri,” amesema.

Aliongeza kuwa uoni hafifu unaowakumba watoto hao, unahitaji uwekezaji maalum katika vifaa saidizi kama vikuza maandishi na vitabu maalum ili kuboresha uwezo wao wa kujifunza.

Kwa upande wa afya, Bwango alisema ukosefu wa mafuta kinga bado ni changamoto kubwa, akibainisha kuwa gharama yake ni kubwa na upatikanaji wake bado hauendani na mahitaji halisi ya jamii hiyo.

“Wenzetu wanahitaji mionzi baridi ya kuanza kuwatibia viashiria vya saratani nayo ni gharama na havipatikaniki kwa urahisi hasa hasa vituo vya zahanati. Kwahiyo tunaiomba Serikali iwewekeze vifaa tiba vianze kupatikana ngazi ya zahanati,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa chama hicho Wilaya ya Kwimba, Anastazia Masunzu amesema baadhi ya changamoto zimeanza kupungua kutokana na juhudi za miradi mbalimbali, lakini bado zinahitaji suluhisho la kudumu kupitia ongezeko la bajeti ya Serikali.

Amesema kuimarika kwa huduma za elimu na afya, kutachangia watoto wenye ualbino kupata haki sawa na kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.