Ziara ya Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV imeingia siku ya pili leo Aprili 14, 2026 ambapo amebeba ujumbe wa amani kwa mataifa yote hasa katika kipindi hiki ambacho ulimwengu umetawaliwa na mizozo.
Papa Leo XIV alianza ziara yake jana Aprili 13, 2026 katika nchi ya Algeria na baadaye ataendelea na ziara hiyo, huko Cameroon huku akitarajiwa kuendelea na ziara hiyo katika nchi nyingine za Angola na Equatorial Guinea hadi atakapohitimisha Aprili 23, 2026.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 70, anatarajiwa kusafiri zaidi ya kilomita 18,000 akizitembelea nchi za Algeria, Cameroon, Angola na Equatorial Guinea ambapo atatoa hotuba 11 na kuongoza misa saba kabla ya kurejea Vatican, Aprili 23.
Akitarajiwa kugusia masuala mbalimbali ikiwemo migogoro, haki za binadamu, uhamiaji na rushwa, papa huyo mzaliwa wa Marekani atatumia ziara hiyo kuzungumzia changamoto zinazoikabili dunia kwa sasa, hasa katika kipindi cha sintofahamu kinachochochewa na vita vya Mashariki ya Kati na athari zake kiuchumi.
Hii ni safari yake ya tatu nje ya Italia tangu alipochaguliwa Mei 2025, baada ya ziara zake za awali katika nchi za Uturuki na Lebanon mwaka jana, pamoja na Monaco, Machi 2026.
Jana, Papa Leo XIV aliwasili Algeria na kutoa hotuba yake ya kwanza katika taifa hilo kwenye mnara wa mashujaa wa Maqam Echahid, ambapo alihimiza msamaha na kusisitiza kuwa “mustakabali wa baadaye ni wa wanaume na wanawake wa amani.”
Ziara hiyo imeandika historia mpya, ikiwa ni mara ya kwanza kwa papa kukanyaga ardhi ya Algeria. Baada ya safari ya takribani saa mbili kwa ndege, Papa Leo XIV hakuelekea kukutana na wanadiplomasia au viongozi wa serikali, bali alielekea moja kwa moja kwenye mnara wa taifa unaowaenzi mashujaa waliopoteza maisha katika harakati za kupigania uhuru wa nchi hiyo.
Katika mvua iliyokuwa ikinyesha kwa vipindi, papa aliweka shada la maua kwenye mnara huo na kusimama kwa muda akifanya sala huku bendi ya kijeshi ikipiga muziki wa heshima. Baadaye, aliwahutubia wananchi waliohudhuria, akianza kwa salamu: “Amani iwe nanyi! As-salamu alaykum!”
Papa Leo alisema amefika Algeria kama mrithi wa mtume Petro, lakini zaidi ya yote kama ndugu anayelenga kuimarisha uhusiano wa upendo. Akiwatazama wananchi wa Algeria, akisema: “Naona sura ya watu imara na vijana, ambao ukarimu na undugu wao nimeushuhudia mara nyingi.”
Aliongeza kuwa: “Ndani ya moyo wa Mualgeria, urafiki, uaminifu na mshikamano si maneno matupu, bali ni maadili yenye thamani yanayotoa joto na nguvu katika maisha yenu ya pamoja.”
Akirejea historia ya Algeria, Papa Leo alitambua mizizi yake ya kitamaduni pamoja na vipindi vya maumivu na vurugu ilivyopitia. “Uwepo wetu hapa kwenye mnara huu ni heshima kwa historia ya Algeria na roho ya watu waliopigania uhuru, heshima na mamlaka ya taifa hili,” alisema.
Baadaye, Papa Leo XIV alielekeza hotuba yake kwenye ujumbe mkuu wa amani inayojengwa juu ya haki, utu na msamaha.
“Mungu anatamani amani kwa kila taifa: amani ambayo si kukosekana kwa vita tu, bali ni kielelezo cha haki na utu,” alisema. “Amani hii, inayotuwezesha kuukabili mustakabali kwa moyo uliopatanishwa, inawezekana tu kupitia msamaha.”
Aliongeza: “Mapambano ya kweli ya ukombozi yatashinda kikamilifu pale tu tutakapopata amani mioyoni mwetu. Najua kusamehe si jambo rahisi. Hata hivyo, wakati migogoro ikiendelea kuongezeka duniani, hatupaswi kuongeza chuki juu ya chuki, kizazi hadi kizazi.”
Aliendelea kusisitiza kuwa: “Mustakabali ni wa wanaume na wanawake wa amani. Mwishowe, haki itashinda daima dhidi ya dhuluma, na vurugu, licha ya kuonekana kuwa na nguvu, hazitakuwa na neno la mwisho.”
Papa Leo XIV ameingia kwenye majibizano na Rais wa Marekani, Donald Trump baada ya kueleza kutounga mkono mzozo unaoendelea Mashariki ya Kati huku akisisitiza haja ya amani katika kutafuta suluhisho.
Hata hivyo, katika ujumbe wake kupitia mtandao wa Truth Social, Trump aliandika kuwa Papa ni dhaifu katika suala la uhalifu na mbaya kwa sera za nje. Kauli hiyo imezua mjadala kimataifa, hasa miongoni mwa waumini wa Kanisa Katoliki na wachambuzi wa siasa.
Akizungumza akiwa safarini kuelekea Algeria katika ziara yake ya siku 11 barani Afrika, Papa Leo alisema hataki kuingia kwenye mabishano ya kisiasa na Trump, bali ataendelea kusimamia ujumbe wa amani.
