Dodoma. Tanzania inahitaji kuwa na magereza 129 ili kukidhi mahitaji ambapo kwa sasa yanatakiwa kujengwa magereza 50 kwa thamani ya Sh40 bilioni.
Kauli hiyo imetolewa bungeni Jumanne Aprili 14, 2026 na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani, Ayoub Mohammed Mahmoud wakati akijibu swali la Mbunge wa Babati Mjini (CCM), Dk Emmanuel Khambay.
Katika swali la msingi, mbunge huyo amehoji ni lini Serikali itafanya maboresho ya makazi ya askari pamoja na kununua magari mapya Gereza la Babati Mjini mkwani majengo yake yamechakaa.
Dk Khambay amehoji kama Serikali inakiri majengo ya gereza hilo yamechakaa ni kwa nini isijenge gereza jipya litakaloendana na hali ya sasa na mahitaji ya kisasa badala ya kuendelea kukarabati lililopo ambalo miundombinu yake imepitwa na wakati.
Naibu Waziri amesema Gereza la Babati ni miongoni mwa Magereza yaliyojengwa miaka mingi tangu 1974 hali iliyosababisha uchakavu wa miundombinu ya gereza na majengo ya makazi ya askari.
“Serikali kupitia Jeshi la Magereza limeanza kutekeleza mpango mkakati wa muda mfupi na mrefu ambapo kwa Gereza Babati ziko nyumba tatu zinaendelea na ujenzi kwa kutumia mapato ya vyanzo vya ndani vya ubunifu,” amesema Mahmoud.
Naibu Waziri amesema katika mwaka wa fedha 2025/26 Serikali imetenga Sh5 bilioni kwa ajili ya ununuzi wa magari 31 kwa shughuli za utawala na kusafirisha mahabusu.
Kuhusu mgawanyo wa magereza, amesema kati ya idadi ya magereza, 10 yanatakiwa kuwa ya kanda, 76 ni magereza ya mikoa na wilaya wakati magereza 43 yatakuwa ni ya wazi ambapo wastani wa ujenzi kwa gereza moja ni Sh8 bilioni.
Amesema kwenye maboresho hayo, Jumla ya Sh2.9 trilioni zitatumika kujenga nyumba 6,368 zitakazokaliwa na zaidi ya kaya 21,187 za askari.