Wachumi wabainisha mbadala tozo ujenzi wa barabara

Dar es Salaam. Kauli ya Mbunge wa Tanganyika (CCM), Seleman Kakoso kupendekeza Serikali kuongeza tozo ya Sh100 kwenye simu ili kujenga barabara, imewaibua wachumi wakisema hakuna haja ya kuwapa wananchi mzigo badala yake Serikali ibane matumizi yake.

Mbali na kubana matumizi, wamesema Serikali inapaswa kuimarisha mifumo ya ukusanyaji kodi kuliko kuwapelekea wananchi zaidi mzigo.

Kakoso alitoa mapendekezo hayo Aprili 13, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akichangia mjadala wa hotuba ya Waziri Mkuu unaohitimishwa Jumatano, Aprili 15, 2026, akisema mpango huo unaweza kukusanya hadi Sh1 trilioni.

Kakoso amesema Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) ndio uweke kima hicho kwenye maongezi ya simu na fedha hizo zitatumika kugawiwa katika mafungu mawili, yaani Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

“…mimi nina mapendekezo mawili, kwanza Serikali iendelee kudhibiti mapato lakini tukubaliane kuanzisha chanzo kipya cha mapato kwenye muda wa maongezi katika simu zetu,” alisema Kakoso ambaye ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu.

Taarifa zilizopo zinaonyesha mpaka sasa Tanzania inatoza kodi kwa takribani asilimia 40 katika huduma za simu nchini, sehemu kubwa ikiwa ni Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na ushuru wa bidhaa.

Pendekezo hilo la Kakoso ni kama ambalo limewahi kutolewa mwaka 2021 na Mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Zungu la kuanzishwa kodi ya uzalendo itakayokatwa katika mitandao ya simu kwa kila Mtanzania.

Pendekezo la Zungu ambaye sasa ni Spika wa Bunge, lilifanyiwa kazi ambapo kwenye bajeti ya 2021/22 Serikali ilianzisha kodi kwenye simu na Zungu akichangia bungeni Juni 17, 2021 alitetea uamuzi huo wa Serikali.

Alisema Tanzania ina watu milioni 55 lakini wanaolipa kodi hawafiki milioni tano, hivyo ili kuibeba nchi ni lazima Watanzania wote wajitoe mhanga. Alisisitiza tozo hiyo inamfanya mwananchi wa kawaida achangie mchango wake kwenye barabara, bima na afya.

Baada ya Kakoso kutoa pendekezo hilo, kumekuwa na mjadala mitandaoni na Mwananchi limezungumza na wataalamu wa uchumi, ambao wameshauri maeneo ambayo fedha zinaweza kupatikana kugharamia ujenzi wa barabara badala ya kuongeza tozo.

Noel Shao, mchambuzi wa masuala ya kijamii amesema badala ya wabunge kufikiria kuwaongezea wananchi mzigo, ni vyema kuangalia ni namna ya kuwasaidia na kuibana Serikali kupunguza matumizi.

“Kuleta tozo ni kumuumiza mwananchi, ipo mianya mingi ya upotevu wa mapato ya Serikali, ukiangalia Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) fedha nyingi zinapotea mifukoni mwa watu sasa, tukifanyia kazi eneo hilo tu fedha za barabara tunapata,” amesema.

Mbali na hiyo amesema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) bado haijafikia maeneo mengi kukusanya kodi, hivyo ukusanyaji ungeimarishwa na wazo la kuwaongezea wananchi tozo lisingekuwepo.

Akitoa maoni yake kuhusu pendekezo hilo, Mchambuzi wa Masuala ya Uchumi, Oscar Mkude amesema, wabunge wanapaswa kujadili namna fedha za Serikali zinavyotumika na kubana matumizi ili kupata fedha za kujenga barabara.

Amesema kuwatoza wananchi ni wazo rahisi ambalo linawaumiza Watanzania wa kipato cha chini ambao wakati mwingine wanashindwa kumudu milo miwili kwa siku.

“Matumizi ya Serikali ili yapungue, unaweza kukuta waziri au mkuu wa mkoa anaambatana na wasaidizi wake kwenda kukagua mradi au kwenda kwenye hafla akiwa na mshururu wa magari na hapo wanalipwa posho, mafuta ya gari, wanaposafiri nje ya nchi ndio usiseme, sasa haya yote yakipunguzwa  yatatusaidia,”amesema.

Mkude amesema ripoti ya CAG na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imebaini upotevu mkubwa wa fedha ambazo kama zingetumika kwenye miradi ya Serikali ingekuwa na tija.

Amesema ni vyema ripoti hizo zinapotoka zifanyiwe kazi, akisisitiza Tanzania tatizo lililopo ni usimamizi wa fedha zilizopo.

Hakuna haja kuumiza wananchi

Naye Mtaalamu wa Uchumi Profesa Haji Semboja amesema tayari upo Mfuko wa Maendeleo ya Barabara, hivyo hakuna haja ya kuwaumiza wananchi kwa tozo.

Ametolea mfano, bei ya mafuta inaonekana kuwa na maumivu kutokana na uwepo wa tozo nyini.

“Hoja ni kupata mapato kwa ajili ya kuleta maendeleo, sasa tuna rasilimali nyingi, nilitegemea wabunge wajiulize ndani ya nchi yetu hizi dhahabu tulizonazo tunazifanyia nini, tuteteneze sera na tuwe na taasisi ambazo zitafanyia kazi rasilimali hizi na tupate mapato hapo,”amesema.

Profesa Semboje amesema Tanzania imebainika kuwa na mafuta, madini ya Tanzanite lakini bado hakuna unafuu unaoonekana na hivyo kuwaongezea wananchi kodi ni kutofikiria vyema matumizi ya rasilimali zilizopo.

Naye Rehema Jackson mkazi wa Tabata amesema mawasiliano ni huduma muhimu, hivyo hayaipaswi kutozwa zaidi.

“Hii itapunguza uwezo wa watu kuwasiliana na hata kupata huduma za kifedha kwa simu,” amesema.

Ameishauri Serikali itafute vyanzo vingine vya mapato visivyogusa moja kwa moja wananchi wa kawaida.

Kwa upande mwingine, Hamisi Ally, mkazi wa Mbagala amesema tozo hiyo inaweza kuongeza pengo la kidijitali.

“Watu wa vijijini na wenye kipato cha chini wataachwa nyuma zaidi,” amesema,

Amependekeza uwekezaji katika sekta za uzalishaji kama viwanda ili kuongeza mapato ya taifa bila kuwaumiza wananchi.