Wataalamu wasio na sifa tishio sekta ya mipango miji

Dar es Salaam. Wakati Tanzania ikishuhudia kasi kubwa ya ukuaji wa miji, changamoto mpya imeibuka ndani ya sekta ya mipangomiji, baada ya kubainika kuwepo kwa wataalamu na kampuni zisizo na sifa stahiki zinazopewa dhamana ya kutekeleza miradi ya maendeleo hali inayotia shaka ubora na mustakabali wa upangaji wa miji nchini.

Hayo yameelezwa leo Jumanne Aprili 14, 2026 na Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji (TPRB), Martha Mkupasi, wakati wa semina maalumu ya kuwajengea uwezo wakurugenzi wa kampuni za mipango miji jijini Dar es Salaam.

Mkupasi amesema hali hiyo inachangia kudhoofisha ubora wa miradi na kuharibu taswira ya taaluma ya mipangomiji nchini.

“Baadhi ya miradi inatekelezwa na watu au kampuni zisizo na sifa, jambo linalodhoofisha ubora na kuharibu taswira ya taaluma hii,” amesema.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Kalimenze (kulia) na Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wataalamu wa Mipango Miji (TPRB), Martha Mkupasi wakiwa katika picha ya pamoja na waofisa wa TPRB.

Ameongeza kuwa ukosefu wa mifumo madhubuti ya uendeshaji katika baadhi ya kampuni umeendelea kupunguza ushindani wao sokoni, akisisitiza umuhimu wa kuhakikisha miradi yote inasimamiwa na wataalamu waliothibitishwa rasmi.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, TPRB imeandaa mafunzo maalumu kwa viongozi wa kampuni za mipango miji, yakilenga kuongeza ufanisi wa uendeshaji, ushindani na uwezo wa kushiriki zabuni za miradi mikubwa ndani na nje ya nchi.

Kwa mujibu wa Mkupasi, mafunzo hayo pia yatawasaidia wataalamu kupanua huduma zao kimataifa na kuendana na mabadiliko ya kisasa katika taaluma hiyo.

Akizungumza katika semina hiyo, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Kalimenze amesema elimu endelevu ni muhimu kwa wataalamu ili kuhimili kasi ya ukuaji wa miji.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Deogratius Kalimenze akizungumza wakati wa semina maalumu ya kuwajengea uwezo wakurugenzi wa kampuni za mipango miji jijini Dar es Salaam.

Amesema mafunzo hayo yanatoa jukwaa la kubadilishana uzoefu na kujifunza mbinu mpya za kukabiliana na changamoto za ukuaji wa miji.

Kalimenze ameonya kuwa ukuaji wa miji usioendana na mipango bora umechangia zaidi ya asilimia 67.9 ya makazi kujengwa katika maeneo yasiyopangwa, hali inayosababisha changamoto za miundombinu duni, huduma hafifu za kijamii na uvamizi wa maeneo ya wazi.

Aidha, amesema changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinahitaji wataalamu kuzingatia uhimilivu wa miji ili kuhakikisha maendeleo endelevu.

Wakati Tanzania ikiendelea kushuhudia kasi ya ukuaji wa miji, takwimu zinaonesha kuwa karibu asilimia 50 ya Watanzania wanaishi mijini, ikilinganishwa na asilimia 5.7 mwaka 1967, hali inayoakisi mabadiliko makubwa ya kijamii na kiuchumi.