Dodoma. Serikali, kupitia Wizara ya Madini, imesimamia uendelezaji wa sekta ya madini nchini, ikiwa ni pamoja na kufuta leseni zisizoendelezwa na kudhibiti vitendo visivyokubalika vinavyoathiri ukuaji wa sekta hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Jumatano, Aprili 15, 2026, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali imeendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa utoaji na uendelezaji wa leseni za madini, ambapo imebaini kuwepo kwa baadhi ya wamiliki wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao kisheria.
Amesema baadhi ya wamiliki wa leseni wamekuwa wakihodhi maeneo bila kuyaendeleza, hawalipi ada stahiki, hawazingatii masuala ya ushirikishwaji wa Watanzania wala uwajibikaji kwa jamii, pamoja na kushindwa kuwasilisha vielelezo vya matumizi ya fedha katika uendelezaji wa leseni zao.
“Vitendo hivi havivumiliki na Serikali itaendelea kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria, ikiwa ni pamoja na kufuta leseni zote zitakazobainika kukiuka masharti ya umiliki,” amesema Mavunde.
Kutokana na hali hiyo, Waziri huyo ametangaza kufutwa kwa leseni 40 za utafutaji madini zenye ukubwa wa ekari 188,163, baada ya wamiliki wake kushindwa kuzitekeleza licha ya kupewa hati za makosa.
Aidha, ameiagiza Tume ya Madini kufuta leseni hizo na kuendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara, huku leseni nyingine 43 zikiwa tayari zimepewa hati za makosa tangu Aprili 10, 2026, zikiwemo leseni 40 za utafutaji na tatu za uchimbaji wa kati.
“Endapo wamiliki wa leseni hizo watashindwa kurekebisha makosa ndani ya siku 30, leseni hizo zitafutwa na maeneo kutolewa kwa wawekezaji wengine,” amesisitiza.
Katika hatua nyingine, Serikali imeeleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la matukio ya “gold rush” katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo watu huvamia maeneo yenye taarifa za uwepo wa madini na kuanza uchimbaji bila leseni halali.
Waziri Mavunde amesema vitendo hivyo ni kinyume cha sheria na vinachangia migogoro, uharibifu wa mazingira pamoja na hatari za kiafya kutokana na msongamano wa watu.
“Kuanzia sasa, ni marufuku kuvamia maeneo ya leseni za madini kwa sababu yoyote ile. Serikali haitasita kuchukua hatua kali za kisheria dhidi ya wote watakaokiuka maelekezo haya,” ameonya Mavunde.
Ameongeza kuwa Serikali imekuwa ikichukua hatua za haraka kudhibiti matukio ya watu kuvamia maeneo na kuanza kuchimba dhahabu (gold rush), ikiwa ni pamoja na kulinda usalama wa wananchi, kudhibiti magonjwa ya mlipuko, kuhakikisha upatikanaji wa huduma za afya na mazingira salama, pamoja na kurasimisha maeneo yasiyo na leseni halali pale inapobidi.
“Serikali imebaini pia kuwepo kwa baadhi ya wachimbaji wadogo wasio waaminifu wanaovamia maeneo yenye leseni halali, hali inayosababisha hasara kwa wawekezaji na kuvuruga usimamizi wa sekta hiyo.”
Mavunde ametoa rai kwa wawekezaji wote kuzingatia Sheria ya Madini, Sura ya 123, na taratibu zake, huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kutoa ushirikiano kwa wawekezaji wenye nia ya kuendeleza sekta hiyo kwa tija.
“Maendeleo endelevu ya sekta ya madini yanategemea uzingatiaji wa sheria, nidhamu na ushirikiano kati ya Serikali, wawekezaji na wananchi,” amesema.
