Michango holela shuleni yaibuka tena bungeni, Serikali yatoa majibu

Dodoma. Serikali imekiri kuwepo kwa michango ya mitihani na masomo ya ziada kwa shule za msingi lakini ikaeleza michango hiyo isiwe ya kiholela na lazima ipitie kamati na bodi za shule.

Hata hivyo, Serikali imesema michango hiyo haitakiwi kuwazuia wanafunzi kupata elimu na kuwa usumbufu kwa wazazi.

Imeelezwa kuwa sehemu kubwa ya gharama zinabebwa na Serikali ingawa kila mzazi anatakiwa kushiriki katika gharama za elimu ya mtoto wake na kusisitiza sera inasema ni elimu bila ada na siyo elimu bila malipo.

Suala hilo la michango limeibuliwa tena bungeni jijini Dodoma leo Jumatano, Aprili 15, 2026 na Mbunge wa Segerea (Chaumma), Agnesta Kaiza ikiwa ni wiki moja imepita tangu hoja hiyo ya michango holela kuulizwa na mbunge huyo huyo na Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba kulitolea maelezo.

Leo Jumatano, katika kipindi cha maswali na majibu, Agnesta ameuliza ni nini msimamo wa Serikali kuhusu suala la wazazi kuchangia mitihani, masomo ya ziada na chakula shule za msingi.

Kwenye swali lake la nyongeza, Kaiza ametaka Serikali ione haja ya kuongeza fedha za ruzuku kwa wanafunzi ambayo ni Sh10,000 kwa wanafunzi wa msingi na Sh25,000 kwa wanafunzi wa sekondari ili kuwapunguzia mzigo wazazi.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye, amesema kuwa bado kuna tatizo na madhara makubwa akaomba Serikali iamue kuwaondolea mamlaka wazazi na bodi ili wasianze kutoza michango hiyo, kwani inasababisha baadhi ya watoto kushindwa kufanya mitihani.

Naye Mbunge wa Tarime Vijijini (CCM), Mwita Waitara ameliambia Bunge, katika baadhi ya maeneo walimu wamekuwa na utaratibu wa kuwafungia kwenye chumba maalumu watoto ambao hawachangii chakula pindi wenzao wanapokula na ukifika muda wote wanafunguliwa na kuingia darasa kitendo alichosema kinawaumiza kisaikolojia wanafunzi hao.

Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange amesema mwaka 2016 Serikali ilianza utekelezaji wa elimu msingi bila ada kupitia waraka wa elimu namba 3 wa mwaka 2016 ambao unabainisha majukumu ya mzazi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mtoto anapata vifaa vya kujifunzia, sare za shule, chakula na huduma za afya.

“Mheshimiwa Spika, kwa ajili ya kuboresha ujifunzaji na ufundishaji ikiwa ni pamoja na ustawi wa wanafunzi, kamati na bodi za shule kupitia vikao vya wazazi zimekuwa zikianzisha michango mbalimbali,” amesema Dk Dugange.

Amesema ili kudhibiti michango holela Serikali imekuwa ikiwaelekeza viongozi wa sekretarieti za mikoa na mamlaka za serikali za mitaa kuhakikisha michango ya aina yoyote inaridhiwa kupitia vikao rasmi vya wazazi na kamati au bodi za shule.

Kwa upande wa wanafunzi wa bweni amesema Serikali imeweka katika fomu za maelekezo (joining instructions) mahitaji na michango ambayo mwanafunzi anatakiwa kwenda nayo shuleni.

Dk Dugange amesema Serikali imekuwa ikifuatilia kuhakikisha hakuna michango holela na kiongozi au mwalimu yeyote anayebainika kuanzisha michango iliyo kinyume na utaratibu hatua za kinidhamu na kiutawala zimekuwa zikichukuliwa.

Aprili 9, 2026 mjadala huo uliibuka bungeni baada ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu kueleza msimamo wa Serikali kuhusu michango hiyo wakati akijibu swali la Kaiza.

Mbunge huyo alitaka kufahamu hatua zinazochukuliwa na Serikali kukomesha michango holela inayotozwa katika baadhi ya shule, jambo ambalo limekuwa likilalamikiwa na wazazi katika maeneo mbalimbali nchini.

Akijibu swali hilo, Dk Mwigulu alisema Serikali haina tatizo na michango ya chakula shuleni pale inapokubaliwa na jamii husika kwa lengo la kuboresha lishe ya wanafunzi.

Hata hivyo, alisisitiza michango mingine yote lazima ifuate mwongozo wa Serikali na ipate kibali cha mamlaka husika, hususan wakuu wa mikoa.

“Michango yote lazima ifuate utaratibu uliowekwa. Haiwezekani kila shule ikaibua tozo zake kiholela. Serikali imeweka utaratibu wa kugharamia huduma muhimu za elimu, hivyo shule hazipaswi kuwatoza wazazi michango isiyo rasmi,” alisema Dk Mwigulu.