Bunge la Tanzania launga mkono hadhi ya mwangalizi kwa Bunge la Kiarabu

Dar es Salaam. Bunge la Tanzania limeunga mkono azimio la kulipa Bunge la Kiarabu hadhi ya mwangalizi ndani ya Mtandao wa Mabunge ya Nchi Zisizofungamana (NAM-PN).

Naibu Spika wa Bunge, Daniel Sillo, alitoa kauli hiyo Aprili 15, 2026 alipohutubia Mkutano wa Tano wa Mabunge ya NAM-PN uliofanyika katika Hoteli ya Hilton Istanbul Bomonti, jijini Istanbul, Uturuki.

Katika mkutano huo, Sillo amemwakilisha Spika wa Bunge, Mussa Azzan Zungu na aliambatana na Mbunge Elibariki Kingu.

Akizungumza katika mkutano huo, Sillo amesema kuwa Bunge la Tanzania linaunga mkono azimio hilo, akibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kuimarisha ushirikiano wa kimabunge katika jukwaa la NAM-PN.

“Bunge la Tanzania linaunga mkono azimio la kulipa Bunge la Kiarabu hadhi ya mwangalizi ndani ya mfumo wa NAM-PN,” alisema Sillo.

Kwa mujibu wa azimio hilo, mabunge wanachama yalitambua umuhimu wa kuimarisha uhusiano na taasisi nyingine za kimataifa ili kuboresha maendeleo ya taasisi na ufanisi wa mtandao huo.

Azimio hilo pia limezingatia ombi rasmi lililowasilishwa na Bunge la Kiarabu likiomba hadhi ya mwangalizi.

Hadhi hiyo ikitolewa, Bunge la Kiarabu litashiriki katika mikutano na shughuli za NAM-PN kama mwangalizi, hatua inayotarajiwa kuimarisha ushirikiano wa mabunge na kukuza malengo ya pamoja ya nchi wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana.

Uamuzi huo unaonyesha dhamira ya kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na nchi za Kiarabu zinazowakilishwa katika Bunge la Kiarabu.

Wakati huohuo, wawakilishi wa Bunge la Tanzania walioshiriki mikutano ya Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) mjini Istanbul walitumia Jukwaa la Wanawake kuitangaza Tanzania kuelekea Mkutano wa 153 wa IPU utakaofanyika nchini Oktoba 2026.

Wabunge hao walishiriki jukwaa hilo Aprili 15 katika Hoteli ya Hilton Istanbul Bomonti na kuwakaribisha wajumbe kuhudhuria mkutano huo.

Akizungumza kwa niaba ya ujumbe, Balozi Dk Pindi Chana amewahakikishia washiriki kuwa Tanzania ni salama.

“Tanzania ni salama chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, na tunawakaribisha kushiriki Mkutano wa 153 wa IPU utakaofanyika nchini kwetu Oktoba,” alisema.

Dk Chana aliongeza kuwa Serikali imeendelea kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika shughuli za kiuchumi, maendeleo ya jamii na maamuzi katika ngazi mbalimbali.