KAMISHENI ya Usimamizi wa Ngumi za Kulipwa Tanzania, imezindua rasmi tovuti yake leo Alhamisi, Aprili 16, 2026, ambayo ina mfumo maalum wa kuratibu na kudhibiti masuala yote ya ngumi za kulipwa nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya muda ya uongozi wa TPBRC, Patrick Nyembera, amesema kuanzia sasa taratibu zote za uendeshaji ngumi za kulipwa zitafanywa kidijitali ambapo ni lazima wadau wote muhimu wa mchezo huo wasajiliwe kupitia mfumo uliowekwa katika tovuti ya TPBRC.
Nyembera amesema hatua hiyo itasaidia kudhibiti mambo haramu ambayo yamekuwa yakifanywa kupitia ngumi za kulipwa.
“Kamisheni ya ngumi za kulipwa imeanza kuchukua hatua ya kuwasilisha kwa serikali majina ya wote wanaojihusisha na uharamia huo.
“Tovuti hii itakwenda kutatua changamoto nyingi lakini pia kutoa usaidizi kwa masuala mbalimbali yanayohusu ngumi,” amesema Nyembera.
Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Neema Msitha, ameipongeza TPBRC kwa juhudi kubwa inayofanya katika kuendeleza ngumi za kulipwa nchini.
“Leo tumekutana kufurahi. Naongea hapa nikiwa na bashasha na matarajio makubwa ambayo nimekuwa nayaota kwa mchezo wa ngumi. Naomba niwaombe ndugu zangu muelewe kwamba malengo ya serikali ni kutaka kila mtu anufaike na mchezo huu.
“Utaratibu haulengi kuondoa waasisi wa michezo ambao walikuwepo. Unataka kuwachanganya na wengine ambao wataongeza kitu ambacho kitatufanya wote tujisikie fahari.
“Kupitia hiki kinachokwenda kuzinduliwa kupitia mifumo ndio tunaenda kudhibiti hili. Kuepuka haya mambo ambayo yanaiumiza serikali. Sasa hivi tumefika angalau kuna mwanga. Tuungane tufike mahali tuupende huu mchezo,” amesema Msitha.
Mkuu wa Chuo cha Michezo Mallya, Dk. Jonas Tiboroha, amesema kuwa anaamini ndondi itafanikiwa zaidi kama weledi utazingatiwa.
“Tunachokiona sasa hivi ni tunabadilika. Tulipotoka na tunapokwenda ni vitu viwili tofauti. Sasa ndondi inaonekana ni mchezo wa kulipwa kweli.
“Ujumbe wangu ni mmoja. Maendeleo sehemu yoyote yanahitaji weledi. Kama hakuna elimu huwezi kuendelea. Tunataka tutoe kozi za wataalam wa ndondi kwa nyanja mbalimbali. Ninaamini kwa kufanya hivyo hata harakati za kusogeza mchezo wa ndondi, zitafanikiwa zaidi,” amesema Tiboroha.
Makamu wa Rais wa Yanga ambaye ni miongoni mwa waalikwa katika hafla ya uzinduzi wa tovuti hiyo, Arafat Haji, amesema anaamini kwamba mfumo huo utasaidia kukuza ngumi za kulipwa Tanzania.
