Dar es Salaam. Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesimulia namna alivyoguswa namna alivyoshuhudia wagonjwa wakishindwa kumudu gharama za dawa katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road (ORCI), jambo lililoisukuma Serikali yake kuchukua hatua.
Rais Samia ameeleza hayo leo Aprili 16, 2026 wakati akikagua mabanda ya maonyesho kwenye mkutano wa pili wa kimataifa wa Shirikisho la Jumuiya ya Madaktari wa Upasuaji wa Ubongo, Mgongo na Mishipa ya Fahamu, hali hiyo ilimtoa machozi.
Amesimulia kwamba mwaka 2022, alipotembelea ORCI, alikumbana na taswira iliyomgusa moja kwa moja.
Katika wodi za wagonjwa wa saratani, aliona idadi kubwa ya wagonjwa wakikosa uwezo wa kugharamia dawa, huku wengine wakilazimika kununua dawa kwa gharama kubwa wasiyoiweza.
Amesema aliondoka hospitalini hapo akiwa ameumizwa na kile alichokiona, na akajiapiza kuwa kituo hicho lazima kibadilishwe kuwa hospitali ya mfano inayoweza kuhudumia wagonjwa wa ukanda mzima na nchi jirani.
“Niliona wagonjwa wanateseka, dawa hazipatikani kwa wakati na nyingine zinauzwa kwa gharama kubwa. Nikaondoka nikiwa na maumivu makubwa moyoni,” amenukuliwa akisema Rais Samia, akieleza msukumo wa mageuzi yaliyofuata.
Baada ya ziara hiyo, Serikali ilianza utekelezaji wa maboresho makubwa Ocean Road, ikiwemo uwekezaji wa miundombinu ya kisasa na vifaa tiba vya hali ya juu vinavyolenga kuongeza uwezo wa uchunguzi na tiba ya saratani nchini.
Uwekezaji teknolojia ya kisasa
Mkurugenzi Mtendaji wa ORCI, Dk Diwani Msemwa amesema taasisi hiyo imepata mageuzi makubwa kupitia uwekezaji wa takribani Sh50 bilioni, hatua iliyowezesha kupatikana kwa mitambo ya kisasa ikiwemo Cyclotron yenye thamani ya takribani Sh18.5 bilioni.
Kwa mujibu wake, mitambo hiyo imeiwezesha hospitali kuzalisha dawa za tiba ya mionzi (radioisotopes) hapa nchini, badala ya kuagiza nje ya nchi kama ilivyokuwa awali.
“Tunazalisha dawa zinazotumika kwa wagonjwa wa saratani na zinaweza kutumika kwenye uchunguzi wa PET Scan. Hii imepunguza gharama na muda wa kusubiri matibabu,” amesema Dk Msemwa.
Mtaalamu wa teknolojia ya nyuklia nchini, Dk Tausi Maftaha, amesema Cyclotron ni mtambo wenye uwezo mkubwa wa kuzalisha dawa za wagonjwa wengi kwa muda mfupi.
“Kila baada ya saa chache za uzalishaji, tunaweza kupata dozi za wagonjwa zaidi ya mia moja kwa wakati mmoja. Hii inasaidia sana kuimarisha huduma nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa kwa sasa Tanzania imepiga hatua kwa kuweza kuzalisha dawa hizo ndani ya nchi, hatua inayookoa fedha za kigeni na kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda nje.
Upasuaji na tiba ya kisasa
Katika sekta ya tiba ya magonjwa ya mfumo wa fahamu, Rais wa Shirikisho la Madaktari Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu, Dk Othman Kiloloma amesema Tanzania sasa ina wataalamu waliobobea wanaotoa huduma za kisasa za upasuaji wa ubongo, mgongo na mishipa ya fahamu.
Huduma hizo ni pamoja na upasuaji kwa kutumia darubini (microsurgery), upasuaji wa njia ya matundu bila kufungua fuvu au mgongo, pamoja na tiba za kisasa za matatizo ya akili unde na uvimbe kwenye ubongo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI), Dk Mpoki Ulisubisya amesema Taifa limewekeza katika mashine za kisasa ikiwemo MRI, CT Scan na Cathlab, ambazo zimeongeza uwezo wa uchunguzi wa magonjwa ya ubongo na moyo kwa wakati mmoja.
“Tuna huduma za upasuaji wa kisasa ambazo awali hazikupatikana hapa nchini. Sasa wagonjwa wanatibiwa hapa hapa bila kulazimika kwenda nje ya nchi,” amesema.
Kiharusi na matibabu ya ndani
Mkurugenzi wa Kitengo cha Upasuaji wa Mishipa ya Fahamu na Ubongo wa MOI, Dk Lemery Mchome amesema kiharusi (stroke) bado ni changamoto kubwa nchini, lakini hatua za matibabu zimeanza kuleta matumaini, ambapo zaidi ya wagonjwa 400 tayari wamenufaika na huduma za kisasa na wengi wao kupona.
Taasisi hizo, ikiwemo Muhimbili National Hospital (MNH), Muhimbili Orthopaedic Institute (MOI) na Jakaya Kikwete Cardiac Institute (JKCI), zinaendelea kushirikiana katika rufaa na matibabu ya wagonjwa, huku baadhi ya mitambo ikisaidia huduma katika vituo hivyo.
Baadhi ya washiriki wa mkutano huo, unaotarajiwa kuibua mapendekezo ya kuboresha huduma za dharura, kinga na matibabu ya haraka, sambamba na kuimarisha mtandao wa wataalamu barani Afrika.
Kwa mujibu wa wataalamu, uwekezaji huo wa mabilioni ya shilingi katika vifaa tiba umeimarisha mfumo wa afya nchini na Tanzania sasa ina uwezo wa kutoa huduma za kibingwa ambazo awali zilikuwa zinapatikana nje ya nchi pekee.
Rais Samia amesisitiza umuhimu wa kulinda na kutunza vifaa hivyo vya gharama kubwa, akieleza kuwa vinapaswa kuhudumiwa na wataalamu waliobobea na kufundishwa kwa wengine ili kuhakikisha huduma zinaendelea bila kusimama.
“Tunahitaji watu wengi zaidi waliobobea kuendesha mitambo hii. Tanzania ni kubwa, hatuwezi kutegemea mtu mmoja au hospitali moja pekee,” amesema, akitoa wito wa mafunzo endelevu kwa wataalamu wa afya.
Ameongeza kuwa magonjwa yasiyoambukiza, hususan saratani na kiharusi, yanaongezeka kwa kasi, hivyo uwekezaji huo ni muhimu kuokoa maisha ya Watanzania wengi zaidi.
Kwa ujumla, mageuzi katika ORCI na taasisi nyingine yanaashiria hatua kubwa ya Tanzania katika kuimarisha huduma za tiba za kibingwa huku simulizi ya Rais Samia ikibaki kama chanzo cha msukumo wa mabadiliko hayo makubwa ya sekta ya afya nchini.
