Dar es Salaam. Upande wa Jamhuri katika kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa tisa, wanaokabiliwa na mashtaka ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni, umeieleza mahakama kuwa ipo katika hatua za mwisho kukamilisha majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.
Wakili wa Serikali, Titus Aron, ametoa taarifa hiyo leo, Aprili 16, 2026, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Franco Kiswaga.
“Kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa na tupo katika hatua za mwisho kukamilisha mchakato wa majadiliano na washtakiwa kwa ajili ya kuimaliza kesi.
“Hivyo, kutokana na hali hiyo, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kukamilisha hatua iliyosalia,” amedai Titus.
Baada ya kusikiliza maelezo hayo, wakili wa utetezi, Meshack Dede, alidai ameshafanya malipo ya asilimia 50 kwa mshtakiwa wa pili (Fredrick), hivyo aliomba tarehe fupi kwa ajili ya kukamilisha.
Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hiyo hadi Aprili 29, 2026, na washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Jasmine Elphas, aliyekuwa ofisa wa benki ya Equity makao makuu, na mfanyabiashara Fredrick Elphas Ogenga.
Wengine ni Halifa Maina, Kaizilege Mohamed, Daudi Fata, Mrisho Mrisho, Neema Paul na Jefferson Ogenga, wote ni wafanyabiashara.
Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 20, yakiwemo ya kuongoza genge la uhalifu na kujipatia zaidi ya Sh5.7 bilioni kwa udanganyifu, mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.
Katika kesi ya msingi, kwa pamoja wanakabiliwa na uhujumu uchumi namba 18447 ya mwaka 2025.
Kwa mujibu wa mashtaka, washtakiwa wanadaiwa kati ya Agosti 30, 2024 hadi Juni 28, 2025 katika maeneo tofauti ndani ya Jiji la Dar es Salaam, waliongoza genge la uhalifu na kujipatia Sh5.7 bilioni mali ya benki ya Equity Tanzania Limited.
Katika tarehe hizo, mshtakiwa Jasmine na Ogenga, wakiwa ndani ya makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, waliiba Sh3.6 bilioni zilizokuwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika akaunti ya clearing and settlement mali ya benki ya Equity.
Mshtakiwa Caroline katika tarehe hizo, akiwa katika makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, anadaiwa kuiba Sh728 milioni mali ya benki hiyo.
Pia inadaiwa kuwa kati ya Februari 28 na Aprili 2, 2025, makao makuu ya benki hiyo, Lilian aliiba Sh26 milioni kutoka akaunti ya benki hiyo.
Vilevile, kati ya Januari mosi hadi Aprili 24, 2025, katika benki hiyo, Maina alidaiwa kuiba Sh101 milioni mali ya benki hiyo.
Ilidaiwa kuwa kati ya Januari 22 hadi Aprili 24, 2025, katika ofisi hizo za benki hiyo, Mohamed aliiba Sh57 milioni, huku Fata akidaiwa kuiba Sh758 milioni, tukio analodaiwa kulitenda kati ya Novemba 2, 2024 hadi Mei 25, 2025.
Mahakama ilieleza kuwa kati ya Januari 9 hadi Mei 25, 2025, makao makuu ya benki ya Equity iliyopo Ilala, Mrisho aliiba Sh211 milioni mali ya benki hiyo.
Vilevile kati ya Januari 9 hadi Mei 28, 2025, makao makuu ya benki hiyo, mshtakiwa Neema aliiba Sh32 milioni mali ya benki hiyo.
Pia ilidaiwa washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 ya utakatishaji fedha walizodaiwa kuiba.
