CCM yatoa ratiba mrithi wa Lukuvi Isimani

Iringa. Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Iringa Vijijini kimetangaza rasmi kuanza kwa mchakato wa ndani wa kuwapata wanachama watakaowania nafasi ya ubunge katika Jimbo la Isimani, baada ya kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, William Lukuvi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Aprili 16, 2026 na Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, Sure Mwasanguti, wanachama wote wenye sifa wametakiwa kujitokeza kuchukua na kurejesha fomu za kuomba uteuzi kuanzia Aprili 17 hadi Aprili 18, 2026.

Amesema fomu zitatolewa kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 10:00 jioni katika ofisi za chama wilayani humo, likiwa ni sehemu ya maandalizi ya kujaza nafasi hiyo kupitia taratibu za chama.

Kifo cha Lukuvi kimehitimisha safari ndefu ya uongozi wa zaidi ya miongo mitatu katika Jimbo la Isimani, alikochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1995 na kuendelea kuchaguliwa hadi 2025.

Katika kipindi chote hicho, Lukuvi alijijengea sifa ya kuwa kiongozi mwenye ukaribu na wananchi, akisimamia na kuhamasisha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo miundombinu, elimu na huduma za kijamii.

Mbali na uwakilishi wake bungeni, Lukuvi alishika nyadhifa mbalimbali za juu serikalini, ikiwemo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) pamoja na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, mkuu wa mikia ya Dodoma na Dar es Salaam, nafasi zilizomjengea uzoefu mkubwa katika utumishi wa umma.