Dk Kigwangalla kuwania ubunge au urais 2030?

Dar es Salaam. Mwanasiasa wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hamisi Kigwangalla, alisema uamuzi wake wa kurejea kuwania nafasi za kisiasa utategemea wito na mahitaji ya wananchi na Taifa.

Alisema iwapo wananchi wa Nzega Vijijini watamhitaji, yuko tayari kuwatumikia na iwapo Taifa litamuita, pia yuko tayari kulitumikia bila kusita.

Iwapo atagombea nafasi ya urais, haitakuwa mara ya kwanza, kwani alishawahi kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho mwaka 2015 akiwa miongoni mwa makada zaidi ya 38 waliojitokeza, lakini hakufanikiwa kuvuka hatua za mchujo wa ndani ya chama.

Dk Kigwangalla, ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri wa Afya na baadaye Waziri wa Maliasili na Utalii, alimaliza kipindi chake cha ubunge mwaka jana baada ya kushindwa katika kura za maoni ndani ya CCM na hivyo kutoteuliwa kugombea tena.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam, alisema kwa sasa amejikita katika shughuli zake binafsi na kuendelea kutoa mchango kwa jamii kupitia njia zisizo za moja kwa moja za kisiasa.

Atagombea ubunge au urais?

Alipoulizwa iwapo atarejea tena kwenye siasa za ushindani, alisema uamuzi wake utategemea wito wa wananchi au Taifa.

“Kama Tanzania itaniita, bado nipo tayari kutumikia. Kama Nzega Vijijini itanihitaji, niko tayari pia. Lakini kwa sasa najikita zaidi kwenye shughuli zangu binafsi za kijamii,” alisema.

Alisisitiza hana maumivu wala chuki dhidi ya mtu yeyote kufuatia mabadiliko ya nafasi yake ya kisiasa, akieleza kuwa amechagua njia mpya ya maisha inayomruhusu kuendelea kuhudumia wananchi.

“Mwaka huu niko katika wilaya moja kupitia mradi wangu wa kijamii, mwakani nitaongeza wilaya nyingine. Nimeamua kuendelea kusaidia wananchi kwa namna nyingine,” alisema.

Kwa nini hakurudi tena hospitalini?

Alipoulizwa kuhusu uamuzi wake wa kutorudi kufanya kazi ya kitabibu hospitalini, Dk Kigwangalla alisema bado ni daktari lakini anafanya kazi kwa mtazamo mpana zaidi wa afya ya jamii.

Alisema kwa sasa anajihusisha zaidi na elimu ya afya ya kinga (preventive medicine) na afya ya kuhamasisha jamii (promotive medicine), badala ya kutoa huduma za moja kwa moja za matibabu.

Alieleza hamu ya kufanya kazi ya kitabibu hospitalini ilipungua kutokana na changamoto alizokutana nazo katika miaka ya mwanzo ya kazi yake, hususan wakati wa migomo ya madaktari mwaka 2004/2005.

“Wakati huo tulikaa muda mrefu bila kujua mustakabali wetu wa ajira. Tulikuwa benchi kuanzia Novemba 2004 hadi Julai 2005,” alisema.

Alisema wakati huo waliporudishwa kazini, alipangiwa Hospitali ya Kitete Tabora, lakini alipofika hakupokelewa ipasavyo, hali iliyomkatisha tamaa.

“Nilipofika hospitali Mganga Mfawidhi hakutaka kunipokea. Hali hiyo iliendelea kwa siku kadhaa ndipo nikaamua kuacha na kwenda kuendelea na shughuli zangu za kilimo Bunda,” alisema.

Alieleza alilima mazao mbalimbali kama mtama, mahindi na pamba ili kujikimu, huku rafiki yake ambaye hakusoma sana akiwa tayari ameendelea kiuchumi.

Akizungumzia tukio la Oktoba 29 mwaka jana, siku ya uchaguzi mkuu iliyoshuhudia vurugu na kusababisha vifo na uharibifu wa mali, Dk Kigwangalla alisema makala yake ya “Oktoba Tunatiki Vs Oktoba Tunatoka” ilieleweka kwa mitazamo tofauti.

Alisema lengo lake lilikuwa kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa vurugu na kuhimiza pande husika kutafuta suluhu ya mazungumzo badala ya mgongano.

“Nilikuwa najaribu kuweka usawa kati ya pande zote mbili, lakini pia kuonya kwamba kuandamana siku ya uchaguzi ni hatari kwa Taifa,” alisema.

Alisema alichokifanya kilikuwa ni kuhimiza mazungumzo ili kuepusha machafuko, jambo ambalo baadaye lilitokea kama alivyohofia.

Hata hivyo, alisema hawezi kuthibitisha ukubwa wa vurugu au idadi ya vifo, akisema hilo ni jukumu la tume iliyoundwa kuchunguza tukio hilo na kutoa taarifa rasmi.

Aliunga mkono uamuzi wa Serikali kuunda tume ya uchunguzi, akisema ni hatua muhimu kuelekea maridhiano na uponyaji wa Taifa.

“Sisi kama wananchi tunapaswa kusubiri ripoti ya tume ili tujue kilichotokea na mapendekezo yake,” alisema.

Dk Kigwangalla alisema changamoto ya ajira kwa vijana ni kubwa na inahitaji mabadiliko ya fikra.

Alisema kila mwaka zaidi ya wahitimu milioni moja huingia sokoni, lakini nafasi za ajira rasmi hazitoshi hata kufikia laki moja.

“Hata tukijumlisha sekta zote, ajira rasmi ni chache sana ukilinganisha na idadi ya wahitimu,” alisema.

Alionya kuwa kama hali hiyo haitapatiwa suluhu, inaweza kusababisha athari kubwa kijamii na kiusalama kutokana na ongezeko la vijana wasio na ajira.

Alisema suluhisho ni vijana kujiajiri na Serikali kuwekeza zaidi katika viwanda na kilimo ili kuzalisha ajira.

“Lazima tuwafundishe vijana kufikiri nje ya mfumo wa kawaida wa ajira. Vinginevyo tutakuwa na jamii yenye hasira,” alisema.

Akiwa Naibu Waziri wa Afya, Dk Kigwangalla alisema walisimamia mabadiliko yaliyoongeza mapato ya Hospitali ya Taifa Muhimbili ndani ya miezi sita kupitia maboresho ya mifumo ya kidijitali.

Pia, aliboresha huduma za wagonjwa mahututi kwa kuongeza uwezo wa ICU kufikia kiwango kilichokidhi mahitaji ya hospitali kubwa.

Akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii, alisema walibadilisha mfumo wa ugawaji wa vitalu vya uwindaji kwa kuondoa mamlaka ya moja kwa moja ya waziri na kuweka mfumo wa uwazi wa kidijitali.

Hatua hiyo ilisababisha mapato kuongezeka, kuongeza uwazi na kupunguza upendeleo.

Hata hivyo, alikiri kuwa uamuzi huo ulipingwa na baadhi ya watu waliokuwa wakinufaika na mfumo wa awali.

Alisema kutokana na maamuzi yake ya mageuzi, aliwahi kupewa ulinzi baada ya tathmini ya kiusalama kuonyesha uwezekano wa hatari dhidi ya maisha yake.

“Sikuomba ulinzi, nilipewa tu kwa sababu ya tathimini ya usalama,” alisema.

Dk Kigwangalla alisema siku yake huanza mapema kwa sala na mazoezi ya Yoga, kisha hufuatiwa na mazoezi ya nje au gym.

Alisema hupenda kukimbia au kutembea umbali wa kilomita tano hadi 10, kabla ya kuanza kusimamia shughuli zake za kila siku.

Baada ya hapo, hujikita katika kufuatilia miradi yake binafsi kupitia simu au kwa kwenda moja kwa moja kwenye maeneo husika.

Alisema pia hupenda michezo kama mpira wa kikapu, gofu na tenisi, ingawa aliacha mpira wa miguu baada ya kuumia goti mwaka 2022.

Aidha, ni mtaalamu wa kareti mwenye mkanda mweusi.