Nina wazo. toka pale tulipopata uhuru wetu kutoka kwa waliokuwa wanatutawala, Desemba 9, 1961, miaka 65 iliyopita, tuna wazee wetu ambao mpaka Ijumaa ya leo Mungu wetu mwema amewajalia wako hai japo wako katika ile hali anayosema Mungu mwenyewe kuwa ni wakati wa kuambiwa “twende huku na unakwenda tu” bila kubisha maana umechoka.
Ndio, hali ya kutolewa nje uote jua na jioni unarudishwa ndani. naam, huna tofauti na nguo ya mtumba. kuanikwa na kuanikwa tu.
Hawa ni wazee wetu ambao sasa wana miaka 70 na kuendelea ambao kwa hakika idadi yao imepungua mno. kati ya Watanzania milioni kadhaa waliopo sasa nchini wao wanaweza kuwa milioni chache sana na kadri miaka inavyoyoma mbele wao ndio wanazidi kutoweka.
Hawa ukiwaongeza na wale akina sisi ambao miaka ya 70 ndio tulimaliza shule na ajira zikatutafuta ili kulijenga taifa letu hili na kulifikisha mahali pa kuliwezesha kuwalipa wasemekanao kuwa ni wawakilishi wa wananchi Shilingi milioni 14 kwa mwezi, wakati wastaafu wa kima cha chini tulioijenga nchi kwa jasho na damu yetu tukiambulia kulipwa pensheni ya shilingi laki mbili na hamsini elfu tu kwa mwezi. Halafu kuna watu wanaodai kuwa binadamu wote ni sawa.
Hapa hatumaanishi wastaafu walioajiriwa na Serikali, kampuni na taasisi za umma na binafsi walioijenga nchi, tunazungumzia wale wastaafu wakulima ambao walikuwa wakilima mazao ili akina sisi wa maofisini tupate chakula cha kutuwezesha kuijenga nchi. Tuwape pongezi zao japo inahuzunisha sana sasa kwamba hata Taifa haliwakumbuki wala kuwatambua.
Kuna umuhimu sasa wa Taifa kulazimika kuunda tuzo kwa wastaafu wote nchini, wale rasmi wa kima cha chini wanaopokea pensheni ya shilingi laki unusu na wale ambao hawakuajiriwa rasmi lakini waliweza kulima mazao na kutuwezesha kula na kuweza kuijenga nchi, lakini sasa tunajiona kuwa hatulazimiki kujua kama wanakula. Walitulisha lakini sasa sisi hatuwalishi.
Kuna umuhimu mkubwa kwa Taifa kuanzisha tuzo kwa wazee, wakiwemo wastaafu, ili Taifa liweze kuonyesha shukurani kwa wastaafu hawa, walioajiriwa na wale waliojiajiri kulima ili kulilisha taifa wakati tunalijenga ingawaje sasa hata matibabu ya bure kwa wazee hawa yameishia kuwa maneno ya kanga tu.
Serikali ijipange ili angalau ionekane kwamba inawajali wazee wake hawa waliolijenga Taifa kwa kulima mazao ya chakula ili kuwalisha wale waliokuwa waajiriwa, mbali ya kulima mazao ya biashara kama katani, kahawa, korosho, pamba na mengineyo, na kuifanya nchi iwe na pochi linaloeleweka.
Serikali inaweza kufanya hivi: kila tarehe tisa Desemba, siku ya uhuru ambapo wazee hawa ndio walianza kulijenga Taifa, ikusanye wazee japo 25 kuwakilisha mikoa yao ili kuwawakilisha wenzao zinapofanyika sherehe za kitaifa za uhuru.
Wazee 25 hao watapokea tuzo ya Taifa ya wazee zitakazowawakilisha wazee wote waliokuwa wakulima wastaafu. Baada ya tuzo hiyo kila mkulima mstaafu wa miaka 70 na zaidi atapokea japo shilingi laki moja kwa utaratibu utakaopangwa na Serikali. Miaka 70 inakuwa maalumu ili kupunguza msururu wa wastaafu wa miaka 60 hadi 70 ambao itawabidi wasubiri kwanza kupata tuzo hiyo ya Taifa hadi watakapofikisha miaka 70.
Hii itasaidia kufanya Serikali isiweze kuchomoa kwa kudai kuwa watu ni wengi na haina fedha za kutosha. Mmemsikia CAG mwaka huu kweli? hela za kulipa wakulima wachache waliotulimia wakati tukiijenga nchi, ambayo inakuwa haina hela lakini za kuwanunulia waheshimiwa magari ya shilingi milioni 500 kwa moja ipo.
Wastaafu waajiriwa wa kima cha chini wao wataambulia tu vyeti vya tuzo hizo. angalau wao wanapata japo shilingi laki mbili na nusu kwa mwezi kama pensheni yao, labda kama muhusika atafanya kile kinachotegemewa cha kuwapa wastaafu wa kima cha chini pensheni ya shilingi laki tano kwa mwezi. Kila kitu kinawezekana pamoja na umasikini wetu unaopigiwa sana chapuo, japo nchi si maskini kihivyo. Inataka utashi tu.
Tuzo yetu tunaweza kuiita tuzo ya nyerere kwa wastaafu ili kumkumbuka mstaafu wetu wa Taifa tuliyejenga naye nchi kwa jasho letu. Wastaafu wetu wakulima wakipata japo shilingi laki moja kwa mwaka si haba, watakumbuka jinsi walivyosota kutulisha sisi wa mjini wakati wote tukiijenga nchi.
Tufanye hivyo kila mwaka wakati wa sherehe za uhuru ili Watanzania wenzetu wakulima wastaafu wajione kuwa hatimaye na wao ni Watanzania na nchi imewakumbuka.