Sababu maumivu ya mgongo kwa watoto, vijana kushika kasi

Dar es Salaam. Katika miaka ya hivi karibuni, tatizo la maumivu ya mgongo kwa watoto na vijana walio chini ya miaka 18, hasa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari, limeanza kuibuka kwa kasi na kuwa changamoto mpya ya kiafya katika jamii.

Kwa muda mrefu jamii imekuwa na mtazamo kwamba maumivu ya mgongo ni tatizo linalowahusu zaidi watu wazima na wazee. 

Hata hivyo, hali imeanza kubadilika, huku wataalamu wa afya wakieleza kuwa idadi ya watoto wanaolalamikia maumivu hayo imeongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma.

Takwimu mbalimbali zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 50 ya watoto na vijana waliopo shuleni wamewahi kukumbwa na tatizo hilo kwa kiwango fulani. 

Hali hiyo inaashiria umuhimu wa jamii kuanza kuangalia kwa makini chanzo cha tatizo na kuongeza juhudi za elimu ya afya ili kupunguza visababishi vinavyoweza kuepukika.

Akizungumza kuhusu hali hiyo, mtafiti na mwanzilishi wa Doctor Rafiki Afrika, Dk Julieth Seba, pamoja na ofisa wa fiziotherapia, Daniel Materu, wanasema mabadiliko ya mtindo wa maisha ni miongoni mwa sababu kuu zinazochangia tatizo hilo.

Wanasema tofauti na zamani ambapo watoto walikuwa wakijihusisha zaidi na shughuli za kimwili na michezo kama mpira wa miguu, kuruka kamba, rede na kuogelea, watoto wengi wa sasa hutumia muda mwingi wakiwa wameketi.

“Watoto wa sasa hutumia muda mrefu darasani, lakini pia nyumbani wanakaa kwa muda mrefu wakitazama runinga au kucheza michezo ya kielektroniki. Hali hii husababisha mwili kutopata mazoezi ya kutosha,” anaeleza Materu.

Mbali na hilo, wataalamu hao wanasema ubebaji wa mabegi mazito ya shule kwa namna isiyo sahihi, pia ni sababu nyingine ya maumivu ya mgongo kwa watoto ambao miili yao bado ipo katika hatua ya ukuaji.

Kwa mujibu wa Materu, kitaalamu mtoto anashauriwa kutumia begi lenye mikanda miwili na kuhakikisha uzito wa begi hauzidi asilimia 10 hadi 15 ya uzito wa mwili wake.

“Ubebaji wa begi zito kila siku au kubeba begi kwa kutumia mkanda mmoja pekee kunaweza kuongeza hatari ya kupata maumivu ya mgongo,” anasema.

Pia, mikao mibaya wakati wa kukaa darasani kwa muda mrefu imeelezwa kuwa chanzo kingine cha tatizo hilo. Wataalamu wanasema baadhi ya watoto huanza kuonekana na mabadiliko ya umbo la mgongo, ikiwemo kupinda kwa mgongo au kuonekana na kibiongo.

Mara nyingi hali hiyo hutokana na kutumia viti visivyoendana na maumbile ya miili yao au kukaa kwa muda mrefu bila kubadilisha mkao.

Aidha, mabadiliko ya aina ya vyakula vinavyoliwa na watoto nayo yametajwa kuwa sababu inayoweza kuchangia udhaifu wa mifupa. 

Upungufu wa madini muhimu kama calcium, magnesium na zinc unaweza kufanya mifupa isiwe imara.

Vilevile, matumizi makubwa ya vyakula vyenye mafuta na sukari nyingi yamechangia ongezeko la uzito kupita kiasi kwa baadhi ya watoto, hali ambayo pia huongeza shinikizo kwenye mgongo.

Wataalamu wanashauri wazazi kuwa makini wanapoona watoto wakilalamika maumivu ya mgongo mara kwa mara. Dalili kama homa, maumivu yanayosambaa hadi miguuni, maumivu makali hasa wakati wa usiku au kupungua kwa nguvu za mwili zinapaswa kuwa ishara ya kumpeleka mtoto hospitali mapema kwa uchunguzi zaidi.

Kwa mujibu wa wataalamu, elimu kwa wazazi, walimu na watoto kuhusu mkao sahihi, lishe bora na umuhimu wa mazoezi ya mwili, inaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hili linalozidi kujitokeza kwa kasi.