Jeuri ya Pedro, akiwazidi kete Barker, Ibenge

KUNA bato linaendelea kwa timu tatu za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara kufukuzana, lakini ndani ya mbio hizo, ipo jeuri wanayotamba nayo benchi la ufundi la Yanga linaloongozwa na kocha mkuu, Pedro Goncalves.

Jeuri hiyo inawahusisha viungo 18 kutoka timu tatu za Yanga, Simba na Azam wakipambana kwa ubora huku wale wa Yanga wakionekana kuwa tishio mpaka sasa wakiwabeba zaidi mabingwa hao.

Jana Alhamisi ambapo Yanga ilikuwa uwanjani kuikaribisha Mbeya City katika mechi ya Ligi Kuu Bara, takwimu zinaonyesha licha ya kikosi hicho kukumbana na changamoto ya majeraha kwa washambuliaji wake wawili tegemeo, Prince Dube na Laurindo Aurelio ‘Depu’, lakini imeendelea kuwa bora ikibebwa na viungo wake sita ambao wamehusika kwenye mabao 33 kati ya 38 ya timu hiyo.

Wakati Pedro akitamba, amewazidi kete washindani wake, Steve Barker wa Simba na Florent Ibenge anayeinoa Azam, huku makocha wote hao huu ukiwa ni msimu wao wa kwanza kufundisha Ligi Kuu Bara.

Kinara wa ufungaji ndani ya kikosi hicho kwenye Ligi Kuu Bara msimu huu kabla ya mechi dhidi ya Mbeya City alikuwa Mudathir Yahya mwenye mabao saba na asiti moja, nyuma yake kuna washambuliaji Dube na Depu wenye mabao sita kila mmoja, lakini upande wa viungo, Pacome Zouzoua aliyefunga mabao matano na asisti mbili anafuatia baada ya Mudathir.

Viungo wengine ni Maxi Nzengeli aliyefunga mabao matatu na asisti mbili, Allan Okello ana mabao mawili na asisti nne, Mohammed Damaro akifunga bao moja sawa na Duke Abuya ambaye ndiye kinara wa asisti kwenye timu hiyo akiwa nazo tano.

Viungo hao sita kwa ubora wao, umeitengenezea Yanga jumla ya mabao 19 na asisti 14, timu hiyo ikionyesha kuwa na idara ya viungo yenye ufanisi bora si tu kuchezesha, bali hata kufunga kiasi cha kuiweka kileleni ikiwa na mapambano ya kutetea ubingwa wake ilioubeba mara nne mfululizo.

Nyuma ya Yanga, inakuja Azam ambayo nayo viungo wake wamefanya makubwa wakiongozwa na staa wao namba moja, Feisal Salum ‘Fei Toto’ aliyefunga mabao saba huku akitengeneza asisti tano mpaka sasa.

Anafuatia Idd Seleman ‘Nado’ ambaye amefunga mabao matano na asisti mbili, wakati Yahya Zayd akiwa na bao moja huku Himid bao akiwa na asisti moja.

Azam kwa ujumla wake viungo hao wameipa timu hiyo mabao 13, lakini pia wakitengeneza asisti tisa wakihusika kwenye jumla ya mabao 22.

Simba ambayo inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara, hapa viungo wake wameifanya kushika nafasi ya tatu ambapo kinara wao Libasse Gueye aliyefunga mabao matatu akiwa ameingia kwenye timu hiyo kupitia usajili wa dirisha dogo la Januari 2026, hana asisti, akifuatiwa na Elie Mpanzu aliyefunga mabao mawili lakini ndiye anaongoza kwa asisti ndani ya timu hiyo akipiga tano sawa na Abuya wa Yanga na Fei Toto wa Azam.

Wamo pia Anicet Oura ambaye aliingia sawa na Gueye akiwa na mabao mawili, hana asisti, Neo Maema akiwa na bao moja na asisti moja, wakati Morris Abraham akiwa na asisti moja pekee.

Mzambia Clatous Chama ambaye ameingia kikosini hapo dirisha dogo msimu huu, ameifungia Simba bao moja na asisti moja, lakini jumla ana mabao matatu na asisti, mawili aliyafunga akiwa Singida Black Stars kabla ya kuhama pia huko alitoa asisti moja, hivyo mabao hayo na asisti moja haihesabiki ndani ya Simba.

Viungo hao wa kocha Steve Barker wameitengenezea Simba jumla ya mabao tisa na asisti nane na kufanya kuhusika jumla ya mabao 17 kwenye timu hiyo.

Akizungumzia namna viungo wa kikosi chake wanavyofanya kazi kubwa ya kufunga mabao na kutengeneza, Kocha Mkuu wa Yanga, Pedro Goncalves amesema: “Tulikutana na changamoto kubwa ya wachezaji kupata majeraha lakini ilikuwa zaidi kwa washambuliaji, nashukuru viungo tulionao wanafanya kazi kubwa ya kufunga na kuendelea kuiweka timu sehemu salama.”

Yanga kabla ya kucheza na Mbeya City, ilikuwa na pointi 44 ikiongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara huku ikifunga mabao 38 na kuruhusu matatu, ikishinda mechi 13 na sare tano, haijapoteza iliposhuka dimbani mara 18.

Simba inashika nafasi ya pili ikikusanya pointi 39, imefunga mabao 29 na kuruhusu sita, ikipoteza mechi moja kati ya 18, ikishinda 11 na sare sita.

Azam ambayo nayo haijapoteza mechi ya ligi msimu huu kati ya 18 ilizocheza, inashika nafasi ya tatu kwa pointi 34, ikifunga mabao 23 na kuruhusu matano. Imeshinda nane na sare 10.