Matumaini yarejea Mashariki ya Kati, Israel na Lebanon zikisitisha mapigano

Watu waliokimbia makazi yao kufuatia vita nchini Lebanon wameanza kurejea nyumbani leo Ijumaa, Aprili 17, 2026 wakikagua kama nyumba zao bado zimesimama, ingawa baadhi yao hawana mpango wa kubaki kutokana na hofu kuwa usitishaji mapigano wa siku 10 kati ya Hezbollah na Israel unaweza kuvunjika wakati wowote.

Vilima vya vifusi vinaonekana katika maeneo ambayo zamani yalikuwa na majengo katika vitongoji vya kusini mwa mji mkuu, Beirut, vinavyodhibitiwa na Hezbollah—eneo lililoshambuliwa vikali na Israel kwa zaidi ya wiki sita za mapigano yaliyotokana na vita pana kati ya Marekani na Iran.

Katika eneo la Qasmiyeh kusini mwa Lebanon, magari yalionekana yakivuka daraja la muda lililojengwa kwa haraka juu ya Mto Litani, baada ya madaraja yote kuharibiwa na Israel wakati wa vita, ikiwemo lile la Qasmiyeh lililolipuliwa Alhamisi.

“Nimekagua nyumba yangu na namshukuru Mungu bado imesimama,” amesema Ali Hamza, baada ya kutembelea makazi yake katika vitongoji vya kusini vinavyojulikana kama Dahiyeh.

Hata hivyo, ameongeza kuwa “watu wana hofu ya kurejea kuishi, na ni vigumu kuishi katika mazingira haya, hasa kutokana na harufu mbaya. Ni vigumu kurejea kikamilifu kwa sasa licha ya mateso ya kukimbia makazi.”

Rais wa Marekani, Donald Trump, alitangaza kusitishwa kwa mapigano kati ya serikali za Lebanon na Israel jana Alhamisi. Serikali ya Lebanon imekuwa na mvutano mkubwa na Hezbollah kutokana na uamuzi wake wa kuingia vitani huku ikisisitiza kuvuliwa silaha kwa njia ya amani.

Jeshi la Lebanon limeripoti ukiukwaji wa makubaliano hayo na Israel ikiwemo mashambulizi ya hapa na pale katika vijiji vya kusini, na kuwataka wananchi kusubiri kabla ya kurejea katika maeneo hayo. Hakukuwa na kauli ya haraka kutoka jeshi la Israel.

Katika mji wa kusini wa Nabatieh ulioteketea kwa kiasi kikubwa, baadhi ya wakazi waliosema watabaki kwa ujasiri, huku wengine wakisema hakuna kilichobaki cha kurejea.

“Kuna uharibifu mkubwa na hapa hapakaliki. Hatuwezi kuishi. Tunachukua vitu vyetu na tunaondoka tena,” amesema Fadel Badreddine aliyekuwa ameongozana na mkewe na mtoto wao mdogo.

“Mungu atujalie nafuu na amalize hali hii kabisa—sio kwa muda tu—ili tuweze kurejea nyumbani.”

Mazungumzo ya Iran kurejea

Wakati huohuo, Rais Trump amesema ana imani kuwa makubaliano ya kumaliza vita na Iran yanaweza kufikiwa hivi karibuni, na akaitaka Hezbollah kuunga mkono usitishaji mapigano wa siku 10 unaoungwa mkono na Marekani kati ya Lebanon na Israel.

Amesema uwezekano wa kuongeza muda wa usitishaji mapigano wa wiki mbili na Iran upo, ingawa huenda usihitajike.

“Tutaona kitakachotokea, lakini nadhani tuko karibu sana kufikia makubaliano na Iran,” aliwaambia waandishi wa habari, akiongeza kuwa endapo makubaliano yatasainiwa katika mji mkuu wa Islamabad, anaweza kusafiri kwenda kushuhudia tukio hilo.

Mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israel dhidi ya Iran yaliyoanza Februari 28 yamesababisha vifo vya maelfu ya watu, huku yakizua upinzani mkubwa ndani ya Marekani na kumpa changamoto ya kisiasa Trump kabla ya uchaguzi muhimu wa katikati ya muhula.

Vita hivyo, vimesababisha mshtuko mkubwa wa bei ya mafuta duniani huku Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) likipunguza matarajio ya ukuaji wa uchumi wa dunia na kuonya kuwa mzozo ukiendelea unaweza kusababisha mdororo wa uchumi.

Mawaziri wa fedha wa kundi la G7 wamesema kuna haja ya haraka ya kufikia amani ya kudumu ili kupunguza gharama za kiuchumi.

Mafanikio diplomasia ya siri

Chanzo kutoka Pakistan kinachoshiriki katika upatanishi kati ya Marekani na Iran kimesema Ijumaa kuwa kuna maendeleo katika diplomasia ya nyuma ya pazia, na kwamba mkutano ujao unaweza kuzaa makubaliano ya awali kabla ya kufikiwa kwa mkataba kamili ndani ya siku 60.

“Pande zote mbili zimekubaliana kimsingi, na masuala ya kiufundi yatakuja baadaye,” kilisema chanzo hicho kwa sharti la kutotajwa jina.

Chanzo cha kidiplomasia kimeeleza kuwa mpatanishi mkuu wa Pakistan, Mkuu wa Jeshi Asim Munir, amekuwa akifanya mazungumzo mjini Tehran tangu Jumatano iliyopita na amefanikisha hatua muhimu katika masuala magumu.

Miongoni mwa masuala hayo ni mpango wa nyuklia wa Iran ambapo Marekani imependekeza kusitishwa kwa shughuli zote za nyuklia za Iran kwa miaka 20 huku Iran ikipendekeza kipindi cha miaka mitatu hadi mitano.

Iran, pia, imesisitiza kuondolewa kwa vikwazo vya kimataifa wakati Marekani ikitaka urani iliyorutubishwa kwa kiwango cha juu iondolewe nchini humo. Vyanzo viwili vya Iran vimesema kuna dalili za maridhiano huku Tehran ikifikiria kusafirisha sehemu ya akiba hiyo nje ya nchi.