……….
Na Carlos Claudio, Dodoma.
Mkurugenzi wa Bodi ya Pamba Tanzania, Marco Mtunga, amesema mfumo wa ushirika nchini unahitaji kufanyiwa maboresho ya kina ili kuongeza ufanisi na tija katika tasnia ya pamba.
Akizungumza jijini Dodoma wakati wa mkutano wa wadau wa tasnia hiyo, Mtunga alibainisha kuwa bado kuna changamoto kadhaa zinazoathiri maendeleo ya zao la pamba, ikiwemo ugawaji wa pembejeo, matumizi sahihi ya mizani pamoja na usimamizi wa ubora wa pamba wakati wa mauzo. Alieleza kuwa changamoto hizo zinachangiwa pia na ukosefu wa mamlaka ya kutosha kwa viongozi wa vyama vya ushirika kuwachukulia hatua wanaokiuka taratibu.
Katika hatua za kuboresha uzalishaji, Mtunga alisema serikali imenunua ndege nyuki 60 kwa ajili ya kupulizia mashamba makubwa, ambapo ekari moja inaweza kupuliziwa kwa dakika 10, hatua inayoongeza ufanisi katika kudhibiti wadudu waharibifu. Aidha, matrekta 16 ya kisasa ya kupulizia (self-propelled) yameanza kutumika, yakipunguza muda wa upuliziaji hadi chini ya dakika tatu kwa ekari moja.
Pia alitaja juhudi za kusimika kiwanda cha kuzalisha mbolea hai, ambacho kinatarajiwa kuongeza rutuba ya udongo na kuinua tija kwa wakulima.
Akizungumzia Mfuko wa Maendeleo ya Pamba, Mtunga alisema mfuko huo ndio injini ya maendeleo ya zao hilo, ukiwa unagharamia pembejeo kama mbegu, viuatilifu na vinyunyizi, utafiti wa pamba, shughuli za ugani pamoja na uwekezaji katika mitambo ya kilimo.
Hata hivyo, alibainisha kuwa kutokana na athari za mafuriko msimu wa 2023/2024 na ukame wa 2024/2025, mfuko huo umejikuta ukitumia zaidi ya makusanyo na hivyo kuingia kwenye deni la shilingi bilioni 206.
Kuhusu hatua za kupunguza gharama za uzalishaji, Mtunga alisema serikali imeanza kusimika kiwanda cha kuchakata mbegu kitakachopunguza matumizi ya mbegu kwa asilimia 50 kupitia matumizi ya teknolojia ya tindikali kuondoa mbegu zisizofaa. Hatua hiyo pia itasaidia kuhamasisha upandaji wa pamba kwa kutumia vipandio badala ya njia za kawaida.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anamringi Macha, alisema mkoa wake unaongoza kwa uzalishaji wa pamba nchini, jambo lililochangia yeye kuteuliwa kuwakilisha wakuu wa mikoa inayolima zao hilo.
Alitoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa mchango wake mkubwa katika kuendeleza sekta ya pamba kupitia upatikanaji wa pembejeo, matrekta na ruzuku kwa wakulima. Alieleza kuwa matrekta takribani 300 yaliyotolewa na serikali yameongeza tija kwa wakulima wengi.
“Tunachokihitaji sasa ni kuongeza tija zaidi kupitia wataalamu wa ugani ili kuhakikisha wakulima wanapata mavuno bora na yenye faida,” alisema Macha.
Alibainisha kuwa pamoja na mafanikio hayo, suala la bei ya pamba bado ni changamoto kwa wakulima wengi, huku akitoa mfano wa mkulima mmoja kutoka mkoa wa Mara aliyefanikiwa kuvuna kilo 2,700 na kupata zaidi ya shilingi milioni 3, mafanikio yanayoonesha uwezekano wa kuongeza uzalishaji endapo mazingira yataboreshwa.
Naye Mbunge wa Bunda, Mhe. Getere Mwita, alipendekeza kuwepo kwa mfumo wa kilimo cha mkataba ili kuwahakikishia wakulima soko la uhakika na bei nzuri ya pamba. Alisema mfumo huo utaongeza ari ya uzalishaji kwani wakulima watakuwa na uhakika wa wanunuzi kabla ya kuanza kilimo.
Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuweka sheria zitakazolazimisha wakulima kufuata kanuni bora za kilimo cha pamba ili kuongeza tija na ubora wa zao hilo.
Mkutano huo wa wadau wa tasnia ya pamba uliofanyika Dodoma umebeba kaulimbiu isemayo, “Nguvu ya Pamoja kwa Tasnia ya Pamba Endelevu,” ukilenga kuimarisha ushirikiano kati ya wadau wote katika kukuza na kuendeleza sekta ya pamba nchini.




