Wanawake wanne mbaroni na kilo 129 za mirungi Kilimanjaro

Moshi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Kilimanjaro linawashikilia wanawake wanne kwa tuhuma za kusafirisha dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilo 129.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amesema limetokea leo Ijumaa, Aprili 17, 2026, majira ya saa tano na nusu asubuhi katika eneo la Mjohoroni, Wilaya ya Moshi, kwenye barabara kuu ya Tanga–Moshi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro akizungumzia kuhusu tukio la wananwake wanne kukamatwa na dawa za kulevya aina ya mirungi.

Kamanda Maigwa amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Vaileth Jerome Mlay, Anjela Jackson Mtui, Sabina Zakayo Msela na Vaileth Elimunisa Temba, wote wakazi wa mji mdogo wa Himo, Kitongoji cha Makuyuni.

Amesema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa wanatokea Tarakea, Wilaya ya Rombo, wakielekea Moshi mjini wakiwa na shehena hiyo ya mirungi.

Gari aina ya Nissan Cara Van, linalodaiwa kukamatwa na dawa hizo aina ya mirungi

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, askari waliokuwa doria walilitilia shaka gari aina ya Nissan Caravan walilokuwa wakisafiria.

Amesema baada ya kulisimamisha na kulifanyia upekuzi, walibaini kuwepo kwa dawa hizo.

“Taratibu za kisheria zinaendelea, na zikikamilika hatua zaidi zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa,” amesema.