Barker amrudisha Bajaber Simba | Mwanaspoti

SIMBA imewasili hapa Zanzibar leo Jumatano Aprili 22, 2026 tayari kwa ajili ya kushiriki Kombe la Muungano, huku katika msafara wao yupo staa wao mmoja amerejea lakini kuna hesabu maalum za aina mbili kwa nyota huyo anayecheza eneo la kiungo.

Wakati Simba ikitua tayari kwa mashindano hayo yanayochezwa Uwanja wa New Amaan Complex visiwani hapa, Mohamed Bajaber alikuwa mmoja wa mastaa wa timu hiyo ikiwa ni mara ya kwanza kuonekana kwenye safari za klabu hiyo tangu Wekundu hao wa Msimbazi waliondoe jina lake kwenye mfumo wa wachezaji wanaotumika kwa mashindano mbalimbali kufuatia majeraha aliyokuwa nayo.

Mara ya mwisho Bajaber kuonekana uwanjani ilikuwa Januari 10, 2026 alipocheza kwa dakika tisa tu kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Mtibwa Sugar, anbapo alikaa chini mwenyewe huku akishika mguu wake wa kushoto nyuma ya paja kuashiria maumivu aliyopata.

Kwenye mchezo huo ambao Simba ikiwa nyumbani na kulazimishwa sare ya bao 1-1, Bajaber alitolewa dakika ya 11 na nafasi yake kuchukuliwa na aliyekuwa winga wa timu hiyo, Kibu Denis, ukiwa pia mchezo wa kwanza wa kocha Steve Barker alipoanza kazi kwenye ligi.

Akizungumza na Mwanaspoti, Barker alisema amemuita Bajaber kurudi kwenye kikosi hicho aweze kupata nafasi ya kucheza mechi hizo ikiwa pia ni fursa kwake kuangalia maendeleo yake baada ya kuwa nje kutokana na majeraha.

Barker alisema anataka kutoa nafasi kwa wachezaji wengi ambao hawakuwa wanapata muda wa kucheza kulingana na muda utakavyopatikana kwenye mechi za mashindano ya Muungano.

“Nikweli nimemuita Bajaber, amekuja tuweze kumuangalia juu ya maendeleo yake lakini pia tutampa nafasi ya kucheza kuona namna gani afya yake imeimarika kwa kuwa hizi mechi zinamruhusu kucheza,” alisema Barker.

“Sio tu Bajaber, wako wachezaji wengine ambao wamekuwa hawapati nafasi nao tutaangalia namna ya kuwapa muda wa kucheza ili tuweze kuwajenga kiubora, tutaangalia namna ya muda utakavyopatikana.”

Kesho Alhamisi, Simba itacheza mechi ya robo fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Mafunzo kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, kuanzia saa saa 2:15 usiku.

Endapo Simba itashinda, itacheza nusu fainali dhidi ya mshindi kati ya Mlandege dhidi ya Singida Black Stars.