Dar es Salaam. Sinza unayoiona leo iliyosheheni msongamano wa nyumba chakavu, mrundikano wa fremu za maduka na makazi yasiyopangwa, haitakuwa hivyo miaka 20 ijayo, ikiwa mpango wa Serikali wa kulijenga na kulipatia eneo hilo sura mpya, utatekelezwa.
Kwa mujibu wa mpango huo unaoratibiwa na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Sinza kufikia mwaka 2046 kutajengwa nyumba za ghorofa kuanzia 20, 15 hadi nane kulingana na aina ya udongo, kwa ajili ya makazi, biashara na huduma jumuishi.
Hata hivyo, mpango huo umeibua manung’uniko kutoka kwa baadhi ya wakazi na wamiliki wa ardhi wa Sinza, wakisema hawaridhishwi kwa namna wanavyoshirikishwa, hivyo hawaelewi kinachoendelea.
Ukiacha Sinza, mwaka 2011 Serikali iliwahi kuutambulisha mpango kama huo kwa ajili ya eneo la Msasani, Dar es Salaam lakini, utekelezaji wake haujakamilika. Vilevile iliwahi kutambulisha miradi mingine ya Kigamboni na Luguruni ambayo pia maendeleo yake hayajaonekana.
Ramani ya Sinza mpya, inaonyesha maeneo ya Sinza A hadi C ambayo ni Shekilango, Kwa Remmy, Mori, Madukani, Afrika Sana, Palestina, Mapambano hadi uelekeo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kutajengwa nyumba za ghorofa kuanzia 20, 15 hadi nane kulingana na aina ya udongo.
Katika maeneo hayo, wamiliki wa ardhi hadi wanane watatakiwa kuunganisha maeneo yao, ili kupata kiwanja kimoja, wakati kwa wale wa Sinza D na E ambayo ni maeneo ya Kijiweni na mitaa ya ndani hadi uelekeo wa Makongo wamiliki hawataunganisha viwanja vyao.
Akifafanua zaidi, Ofisa Mipango Miji wa wizara hiyo, Emily Mwasogye amesema wale wa Sinza D na E hawatounganisha viwanja vyao kutokana na aina ya udongo wa maeneo hayo.
Amesema ramani inaonyesha Sinza D na E kutajengwa majengo ya kuanzia ghorofa nne hadi mbili, huku shule na hospitali, zikibaki palepale zilipo sasa, ingawa zitaboreshwa kuwa za ghorofa.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Makazi wa wizara hiyo, Deogratius Kalimenze amesema katika mpango huo wa kuanzia 2026-2046, waendelezaji ni wamiliki wenyewe wa maeneo katika Kata ya Sinza.
Amesema mpango huo utaanza mara tu utakapoidhinishwa wakati wowote kuanzia sasa, akifafanua kuna njia tatu za wamiliki kuendeleza maeneo yao katika mpango huo wa Sinza mpya.
“Njia ya kwanza ni mmiliki mwenye uwezo kuendeleza eneo mwenyewe, katika yale maeneo ambayo yatahitajika viwanja kuunganishwa ili kupata kiwanja kimoja, wamiliki wakikubaliana wakaamua kuendeleza wenyewe itakuwa sawa,” amesema.
Amesema njia ya pili ni mwekezaji kuendeleza na kugawana asilimia 50 kwa 50 na mmiliki au wamiliki ambao watakuwa wameunganisha viwanja vyao; njia ya tatu ni wamiliki kuuza au kupangisha maeneo yao kwa mwekezaji ambaye bado hajajulikana au hajatajwa.
Alipoulizwa kuhusu mradi wa Msasani alisema bado unaendelea, ni mradi wa 2011-2031. Kuhusu Kigamboni alisema una historia ndefu lakini ulifutwa wakati ule wa Luguruni bado unaendelea na ni wa muda mrefu.
Ingawa Mwananchi inafahamu hadi Aprili 4, 2025 kulikuwa na sintofahamu kwa wananchi wa eneo huku mradi huo ukiwa umebakisha miaka mitano kukamilika.
Hawa Hussein, ni mmiliki wa ardhi eneo la Sinza, amesema walikwenda ofisi za serikali za mtaa kupata taarifa na wakataka rasimu iandikwe Kiswahili, lakini hilo halijapewa uzito.
Kwa upande wa Latifa Mustapha, amesema si kama wananchi hawataki maendeleo, lakini kinachotakiwa ni kuwapa uelewa wa mpango huo na ushirikishwaji katika kila hatua.
“Mfano hadi siku ya kikao (Jumapili iliyopita) wengi hatukuwa na taarifa kuhusu mpango huo, tulipata taarifa siku ya mkutano kupitia kwa jirani, Serikali inadai kuna spika zilipita kutangaza lakini si kweli.
“Hata hivyo hatupingi mpango na si kama hatutaki maendeleo, tunayataka lakini vitu viwe wazi, wao wanasema baada ya kikao cha juzi (Jumapili iliyopita) atakuja waziri, anakuja kufanya nini wakati wananchi hawajaelewa huo mpango?” amehoji.
Katika kikao kilichofanyika Jumapili ya Aprili 19, 2026, baadhi ya wamiliki walionekana kutokubaliana na mpango huo, wengine wakipinga zaidi mpango wa wamiliki wanane kuunganisha viwanja ili kupata kimoja.
Wengine walienda mbali wakidai kama Serikali ina nia ya kuendeleza eneo hilo, ikae nao wathaminishwe na kulipwa fidia ya kuanzia Sh1 bilioni hadi Sh3 bilioni kupisha mradi.
Akifafanua hilo, Mwasogye amesema kila kitu kitakuwa wazi kwa mujibu wa sheria, kwani katika mpango huo kuna miaka mitano ya hatua za awali zikiwamo za mazungumzo kati ya wamiliki na mwekezaji.
“Hakuna atakayedhulumiwa au kunyang’anywa eneo lake, kila kitu kitafanyika kwa mujibu wa sheria na taratibu, lengo likiwa kuboresha eneo la Sinza kwa kulijenga kwenda juu,” amesema.
Akizungumza kwa muktadha wa uchumi, Profesa Haji Semboja, amesema hilo linaruhusu ukuaji wa uchumi, kwani katika miji iliyoendelea ndicho kinachofanyika.
“Ukitazama ujenzi wa miji yetu wengi hawatumii ramani au utaalamu. Kwa wenzetu walioendelea nyumba mijini zinajengwa na mashirika binafsi, Serikali na makampuni ya nje na ndani na wananchi wanauziwa kwa masharti nafuu, hayo ndiyo maendeleo si mtu mmoja mmoja anajenga.
“Kwa Sinza wengi wataondolewa, baada ya ujenzi watarudi. Kwanza mji utabadilika, miundombinu itakuwa imara. Wapo wengine katika hilo wanatoka nje ya mji na jengo likimalizika naye anapata gawio inakuwa ni eneo lake la kibiashara linalomwingizia pesa, hivyo kipato chake kinakuwa na sura ya mji inabadilika,” amesema.