Iran yatoa tamko awamu mpya ya mazungumzo, Trump alegeza

New York. Serikali ya Iran imesema iko tayari kuingia katika duru mpya ya mazungumzo na Marekani lakini imeweka sharti la kuondolewa zuio la kijeshi pamoja na kusitishwa kile ilichokiita ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Akizungumza leo Jumatano Aprili 22, 2026 na chombo cha habari cha Iran cha Shargh, Balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa, Amir-Saeid Iravani, amesema hatua yoyote ya mazungumzo haiwezi kuanza kabla ya Marekani kurekebisha msimamo wake.

“Marekani lazima isitishe ukiukwaji wa usitishaji mapigano kabla ya kuanza kwa duru mpya ya mazungumzo,” amesema Iravani.

Ameongeza kuwa pindi zuio hilo litakapoondolewa, mazungumzo yajayo yatafanyika katika mji wa Islamabad, Pakistan akibainisha kuwa Iran iko tayari kwa hali yoyote itakayojitokeza.

“Tutakapoondolewa zuio hilo, duru inayofuata ya mazungumzo itafanyika Islamabad. Iran iko tayari kwa hali yoyote,” amesisitiza.

Katika msimamo wake, Iravani amekanusha madai ya Iran kuwa chanzo cha mvutano wa kijeshi, akisisitiza kuwa nchi yake haijaanzisha uchokozi wowote.

“Hatujakuwa waanzilishi wa mashambulizi ya kijeshi. Ikiwa wanataka suluhisho la kisiasa, tuko tayari. Ikiwa wanataka vita, Iran iko tayari pia,” amesema.

Katika hatua nyingine, Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kuongeza muda wa kusitisha mapigano dhidi ya Iran bila kuweka kikomo maalumu, akisema uamuzi huo umechochewa na ombi kutoka kwa viongozi wa Pakistan.

Kupitia ujumbe aliouchapisha kwenye mitandao ya kijamii, Trump amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya kupokea maombi kutoka kwa Mkuu wa Majeshi wa Pakistan, Asim Munir, pamoja na Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Shehbaz Sharif.

 “Kwa kuzingatia kwamba, Serikali ya Iran imegawanyika sana na kufuatia ombi kutoka Pakistan, tumeombwa kusitisha shambulio letu dhidi ya Iran hadi wakati ambapo viongozi wao wataweza kuwasilisha pendekezo la pamoja,” amesema Trump.

Amesema ombi hilo, linalenga kutoa nafasi kwa viongozi wa Iran kuwasilisha pendekezo la pamoja kwa ajili ya kufanikisha mazungumzo ya amani.

“Katika mambo mengine yote, jeshi liendelee kuwa tayari. Nitaongeza muda wa kusitisha mapigano hadi pendekezo lao litakapowasilishwa na mazungumzo kukamilika,” amesisitiza.

Imeandikwa kwa msaada wa Mashirika ya Habari