Kauli ya Serikali kuhusu bei ya mafuta

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema Serikali inaendelea kufuatilia mwenendo wa upatikanaji wa mafuta duniani na itaendelea kuchukua hatua za kimkakati kulingana na maendeleo ya hali hiyo.

Hatua hiyo, amesema inalenga kulinda upatikanaji wa uhakika wa mafuta, kuzuia mishtuko inayoweza kuathiri shughuli za kiuchumi na kujenga kinga ya mapema dhidi ya changamoto kwenye mnyororo wa ugavi wa bidhaa za petroli.

Serikali inakuja na kauli hiyo, wakati ambao bei za mafuta zimepanda katika soko la dunia na kuathiri gharama za usafiri, uzalishaji na mwenendo wa bei za bidhaa nyingine.

Kupanda huko kwa bei ya mafuta, kunahusishwa na mivutano ya kisiasa na Mashariki ya Kati, hasa athari za kufungwa kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz unaopitisha zaidi ya asilimia 20 ya mafuta yote duniani.

Ndejembi ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo, Jumatano Aprili 22, 2026 alipowasilisha bajeti ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka wa fedha 2026/27.

“Serikali inaendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa upatikanaji wa mafuta duniani na itaendelea kuchukua hatua za kimkakati ili kuhakikisha nchi yetu inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa mafuta, ili kutoathiri utekelezaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii nchini,” amesema.

Katika maelezo yake, amesema pamoja na ufuatiliaji katika soko la dunia, Serikali imeliwezesha Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), kuagiza mafuta yanayotosheleza matumizi ya miezi mitatu yaani Mei, Juni na Julai 2026.

Ndejembi amesema Tanzania inategemea asilimia 59 ya mafuta kutoka Mashariki ya Kati, yaani Falme za Kiarabu, Saudi Arabia, Bahrain, Oman na Kuwait, huku asilimia 41, ikiagiza kutoka India.

“Utegemezi huu unaifanya Tanzania kuwa katika nafasi nyeti wakati wa misukosuko ya kimataifa, hasa pale changamoto zinapohusu maeneo muhimu ya usafirishaji kama Hormuz,” amesema.

Katika hotuba hiyo, amesema licha ya wastani wa bei ya mafuta ghafi kushuka kwa asilimia 14 na kufikia dola 66 kwa pipa kati ya Julai 2025 na Machi 2026, hali ilibadilika Machi mwaka huu, baada ya bei kupanda hadi dola 102 kwa pipa.

Amesema ongezeko hilo lilisukuma pia bei za mafuta yaliyosafishwa kupanda. Kati ya Februari na Machi 2026, bei za petroli ziliongezeka kwa asilimia 69.12, dizeli asilimia 104.30 na mafuta ya taa na ndege asilimia 115.83.

Ndejembi, amesema pamoja na changamoto hizo, Serikali itaendelea kutumia hatua za kimkakati kulingana na maendeleo ya hali hiyo, huku ikiendelea kufuatilia mwenendo wa soko la dunia.

“Tunafanya hivi ili kuhakikisha shughuli za kiuchumi na kijamii haziathiriwi na mishtuko ya mafuta,” amesema waziri huyo.

Katika maelezo yake pia, amesema Tanzania ilipokea lita bilioni 5.84 za mafuta katika kipindi husika. Kati ya hizo, lita bilioni 1.63 za petroli, bilioni 3.94 za dizeli na milioni 260 za mafuta ya taa na ndege, huku sehemu ya mafuta hayo ikihudumia pia nchi jirani.

Hali hiyo, amesema inaonyesha umuhimu wa tahadhari inayochukuliwa sasa, kwa kuwa changamoto ya mafuta si suala la soko pekee bali pia usalama wa ugavi, uthabiti wa uchumi na uwezo wa nchi kuhimili mishtuko ya kimataifa.