Mtoto aliyepotea apatikana, mwingine aibwa

Mwanza. Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limefanikiwa kumpata mtoto wa kike mwenye umri wa miaka mitatu na miezi kumi, aliyeripotiwa kupotea Aprili 18, 2026 baada ya kudaiwa kuibwa kwa kubebwa kwenye pikipiki katika eneo la Kona ya Bwiru, Wilaya ya Ilemela.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa Aprili 20, 2026, amesema tukio hilo liliripotiwa na mama wa mtoto huyo, Neema Sesela (19), mkazi wa Nyampala “B”, Kata ya Nyamanoro.

Amesema siku ya tukio, Aprili 18, 2026 saa 5:00 asubuhi katika Mtaa wa Barabara ya Vumbi, Kona ya Bwiru, mama huyo alipokuwa katika shughuli zake aligundua kuwa mtoto wake ameondoka na mtu asiyejulikana kwa kutumia pikipiki, ambayo namba zake za usajili hazikufahamika.

Baada ya kupokea taarifa, polisi walianza uchunguzi na msako wa kumtafuta mtoto huyo. Aprili 20, 2026 majira ya saa 3:30 usiku, taarifa zilipatikana kuwa mtoto huyo ameonekana akiwa ametelekezwa katika makaburi ya Nyasaka, Wilaya ya Ilemela.

Wasamaria wema walimuokota na kumpeleka kwa mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamuge, Kata ya Nyasaka.

Mtoto huyo alikutwa na michubuko usoni na kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Sekou Toure kwa uchunguzi zaidi. Wazazi wake, akiwemo baba aitwaye Mwankunja Edward (30), fundi seremala, wamemtambua rasmi mtoto huyo.

Uchunguzi wa afya ya mtoto unaendelea, huku Kamanda Mutafungwa akitoa wito kwa wazazi kuimarisha uangalizi wa watoto wao ili kuhakikisha usalama wao.

Katika tukio lingine la wizi wa mtoto, Aprili 19, 2026 majira ya saa 6:00 mchana, katika Mtaa wa Bukala, Kata ya Ibisabageni, Wilaya ya Sengerema, Levina Leonard (32), mkulima, aligundua kuwa mtoto wake mwenye umri wa miezi kumi ameibwa na mtu asiyejulikana akiwa nyumbani.

Mama huyo alitoa taarifa polisi siku hiyo hiyo katika Kituo cha Polisi Sengerema. Hadi sasa mtoto huyo hajapatikana na juhudi za kumtafuta pamoja na kumsaka mtuhumiwa zinaendelea.

Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wenye taarifa zitakazosaidia kupatikana kwa mtoto huyo kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa sahihi kwa mamlaka husika.