Ndejembi ajibu sababu katikatika ya umeme

Dar es Salaam. Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema kuwapo kwa changamoto ya kukatika kwa umeme katika baadhi ya maeneo, kunachangiwa na changamoto katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa nishati hiyo.

Amesema kwa sasa uzalishaji wa umeme unazidi mahitaji, akifafanua megawati zinazozalishwa ni 4,522.54 na mahitaji ni megawati 1,908.02. Lakini, kazi za kuunganisha miundombinu ya nishati hiyo ndiyo sababu ya umeme unakatikakatika.

Kauli hiyo inakuja, katikati ya malalamiko ya kukatikakatika kwa umeme kunakotokea mara kwa mara katika baadhi ya maeneo, huku wananchi wakihoji sababu za changamoto hiyo wakati uzalishaji wa umeme unatajwa kuongezeka.

Ndejembi ameeleza hayo bungeni jijini Dodoma leo Jumatano Aprili 22, 2026 wakati wa hotuba yake ya bajeti ya mpango na makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/27.

Amesema changamoto hiyo haihusiani na upungufu wa uzalishaji, bali kazi zinazoendelea za kuimarisha miundombinu ya gridi ya Taifa, kuunganisha miradi mipya ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme na maboresho ya mtandao wa usambazaji yanayolenga kuongeza uthabiti wa huduma.

“Changamoto zinazojitokeza sasa ni sehemu ya kipindi cha mpito cha kuimarisha mfumo wa umeme, huku hatua zinazotekelezwa zikilenga kuhakikisha uzalishaji ulioongezeka unaendana na uwezo wa miundombinu ya kuusafirisha na kuusambaza kwa uhakika,” amesema.

Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Machi 2026, amesema uzalishaji wa umeme uliongezeka kwa megawati 1,718.70 sawa na ongezeko la asilimia 61.29, ikilinganishwa na uwezo wa megawati 2,803.84 uliokuwapo Machi 2025.

Ndejembi, amesema ongezeko hilo limetokana na kukamilika kwa miradi mbalimbali ya uzalishaji wa umeme, ikiwamo kuanza kwa uzalishaji kutoka mradi wa Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JNHPP) na vyanzo vingine.

Hata hivyo, amesema ongezeko hilo la uzalishaji limeambatana na mahitaji ya kuimarisha miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme huo, ili uwezo wa uzalishaji uliopo ufike kwa uhakika kwa watumiaji.

Amesema Serikali inaendelea kutekeleza miradi ya kuimarisha njia za kusafirisha umeme, ikiwamo ujenzi wa njia za msongo wa kilovolti 400, 220 na 132 na vituo vya kupoza na kusambaza umeme, hatua zinazolenga kuongeza uthabiti wa gridi na kupunguza changamoto za kukatika kwa umeme.

Katika hotuba hiyo, amesema upatikanaji wa umeme nchini umefikia asilimia 78.4, huku vijiji vyote 12,318 vikiwa vimefikishiwa na vitongoji 42,783 kati ya 64,359 vikiwa vimeunganishwa, sawa na asilimia 66.48.

Amesema upanuzi huo wa mtandao wa umeme nao umeongeza mzigo kwenye baadhi ya maeneo ya usambazaji, hali inayolazimu kuendelea kwa uwekezaji katika miundombinu ili kuendana na ongezeko la watumiaji na mahitaji ya umeme.

Ndejembi, amesema katika kipindi kijacho Serikali itaendelea na utekelezaji wa miradi ya kuimarisha gridi ya Taifa, kupunguza upotevu wa umeme katika mfumo na kuboresha huduma kwa wateja kupitia uwekezaji katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha ongezeko la uzalishaji wa umeme linatafsiriwa kuwa upatikanaji wa huduma bora zaidi kwa wananchi, sekta za uzalishaji na shughuli nyingine za kiuchumi.