Dar es Salaam. Kwa miongo kadhaa, mjadala kuhusu mustakabali wa Afrika umeendelea kushika kasi huku bara hilo likikabiliwa na changamoto zinazojirudia katika nyanja za usalama, uchumi na uimara wa taasisi zake za kikanda.
Taasisi hizi zilizoundwa kuwa nguzo ya ushirikiano wa pamoja, mara nyingi zimekuwa zikikosolewa kwa kukosa nguvu ya utekelezaji hali inayodhoofisha ufanisi wake katika kushughulikia matatizo ya pamoja.
Kwa wengi, mjadala huu umeendelea kufufua maumivu ya athari za ukoloni kama chanzo kikuu cha matatizo ya kihistoria na ya sasa. Wakati huo huo, mataifa ya Magharibi kupitia taasisi zao za kimataifa yameendelea kujijenga kama wadau muhimu wa maendeleo barani Afrika.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa ushirikiano huo bado unabeba mizigo ya ushawishi usio sawa, hasa katika masuala ya sera, uchumi na utawala.
Katika muktadha huo, mjadala umechukua sura mpya kufuatia wito wa Rais wa Kenya, William Ruto aliyesisitiza umuhimu wa kufumua muundo wa Afrika ili kuendana na kasi ya changamoto za kisasa na kuimarisha uwezo wa kufanya uamuzi wa pamoja ndani ya Umoja wa Afrika (AU).
Akizungumza Aprili 10, 2026 katika kikao cha Kamisheni ya Ujasusi ya AU, Ruto alieleza kuwa mfumo wa sasa wa AU bado umebeba urasimu mkubwa unaochelewesha uamuzi wa pamoja, hususan katika masuala ya usalama na maendeleo. Alisisitiza kuwa vitisho vya sasa havina mipaka, hivyo vinahitaji majibu ya haraka na ya pamoja.
“Afrika inahitaji mfumo wa uamuzi wa haraka na wa pamoja, kwa sababu changamoto za sasa haziheshimu mipaka wala muda wa kusubiri taratibu ndefu za kiutawala,” alinukuliwa akisema.
Alisema muundo wa sasa unahitaji mageuzi ya kina ili kuendana na hali halisi ya dunia ya leo.
Kauli hiyo imeibua upya mjadala mpana kuhusu uhusiano wa muda mrefu kati ya Afrika na Ulaya, ambao kwa nyakati mbalimbali umekuwa ukilalamikiwa kuwa na sura ya kinyonyaji. Akizungumzia suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Rasul Ahmed anasema mataifa ya Magharibi, hasa kupitia taasisi kama Umoja wa Ulaya (EU) yanaendelea kubeba historia tata inayochangia kutokuwapo kwa usawa wa kweli katika uhusiano huo.
“Historia ya ukoloni imeendelea kujitokeza katika lugha, mitazamo na mahitaji ya kiuchumi. Hii imeifanya Afrika mara nyingi kuwa katika nafasi ya utegemezi,” anasema.
Anasema ushirikiano uliopo bado haujabadilika kikamilifu kutoka mfumo wa misaada kwenda ushirikiano wa kweli unaojikita katika maarifa na teknolojia.
Hata hivyo, mtazamo huo unapewa changamoto na Jeronimo Maillo Gonzalez-Orus, anayesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya ni mdau muhimu wa maendeleo ya Afrika.
Kwa mujibu wake, si sahihi kuubebesha lawama za kudhoofisha maendeleo ya bara hilo.
Anasema Umoja wa Ulaya ulianzishwa baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia kwa lengo la kuzuia vita na kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kijamii, kwamba umefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kukuza amani, utawala bora, haki za binadamu na demokrasia.
“Kuanzishwa kwa EU kulisaidia kuepusha vita na kuleta mafanikio makubwa katika uchumi, haki za binadamu na demokrasia,” anasema akidai kuwa ukuaji wa umoja huo kutoka mataifa sita hadi 27, ni ushahidi wa mafanikio ya muungano wa kisera na kiuchumi.
Katika mjadala wa taasisi za Afrika, Dk Rasul Ahmed anasema licha ya uwepo wa mashirika, mahakama na jumuiya za kikanda, bado kuna changamoto kubwa ya utekelezaji wa uamuzi. Anasema hali hiyo inachangiwa na ukosefu wa nguvu ya pamoja ya kisiasa miongoni mwa mataifa wanachama.
“Taasisi hizi zimekuwa na maazimio mengi, lakini utekelezaji wake unabaki dhaifu kwa sababu mataifa wanachama hayazipi nguvu ya kisheria. Tatizo kubwa hapa ni kukosekana kwa utashi wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa bara hili,” anasema Dk Ahmed.
Mtazamo huo unaungwa mkono na Dk Zemelak Ayele wa Chuo Kikuu cha Addis Ababa, anayeeleza kuwa changamoto ya Afrika haiishii katika udhaifu wa taasisi pekee, bali pia inajengwa na ukosefu wa mshikamano wa kisiasa miongoni mwa mataifa yake.
“Bara la Afrika lina jamii zinazofanana kihistoria na kiutamaduni, hii ni fursa kubwa ya kuunganisha nguvu,” anasema.
Hata hivyo, anasema licha ya uwepo wa taasisi mbalimbali, bado zinakosa utashi wa pamoja wa kuzifanya zifanye kazi kikamilifu.
Wakati baadhi ya wadau wakizitazama taasisi za Afrika kama dhaifu na zisizojibu ipasavyo mahitaji ya bara, kwa upande wake, Duncan Ouma wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) anatetea nafasi ya taasisi za kifedha.
Anasema benki hiyo imekuwa mhimili muhimu wa maendeleo kupitia uwekezaji katika miradi ya miundombinu, nishati na afya.
“Tumechangia miradi mikubwa kama reli ya kisasa (SGR) Tanzania, barabara za kikanda na miradi ya afya katika nchi mbalimbali. Changamoto si taasisi, bali ni mazingira ya utekelezaji,” anabainisha.
Mjadala huu una mizizi yake katika fikra za waasisi wa Afrika, akiwamo Kwame Nkrumah, Julius Nyerere na Jomo Kenyatta, waliotetea kwa nguvu dhana ya umoja wa Afrika kama msingi wa uhuru wa kweli na maendeleo ya bara.
Hata hivyo, Dk Azaveli Lwaitama anatoa mtazamo wake, akieleza kuwa changamoto kuu ya Afrika ni kuendelea kukumbatia mipaka ya kikoloni iliyogawa bara hilo kwa maslahi ya wakoloni.
“Tatizo la Afrika ni kwamba, licha ya uwepo wa African Union, bado hakuna taifa linaloitwa Afrika. Bara lenye zaidi ya watu bilioni 1.3 kama China au India, limegawanyika katika nchi nyingi zenye mipaka ya kikoloni,” anasema.
Anaongeza kuwa hali ya Waafrika kuendelea kuchukuliwa kama wageni au wakimbizi ndani ya bara lao ni ishara ya kushindwa kwa mradi wa umoja wa kisiasa. “Leo mtu anatoka Burundi kwenda Uganda anaitwa mkimbizi, huu ni upungufu mkubwa katika uwezo wa kupanga mikakati ya pamoja ya bara,” anasisitiza.
Kwa mtazamo wake, kushindwa kuvunja mipaka ya kikoloni kunazuia Afrika kulinda rasilimali zake na kujenga nguvu ya pamoja ya kiuchumi na kisiasa.
Akirejea historia, anataja mifano ya mataifa kama Marekani, Ujerumani, India na China kwamba nguvu yao imetokana na umoja wa ndani badala ya mgawanyiko.
Katika muktadha huo, mjadala mpya uliochochewa na kauli ya Rais Ruto unaiweka Afrika njia panda, kati ya kuendelea na mageuzi ya taratibu au kuchukua hatua za mabadiliko ya kimuundo yatakayobadili kabisa mustakabali wa Umoja wa Afrika na nafasi yake katika siasa za kimataifa. Swali linalobaki ni iwapo bara litaendelea kushikilia mfumo wa sasa au litafungua ukurasa mpya wa umoja wa kweli wa kisiasa na kiuchumi.
Wachambuzi wengi wanasisitiza umuhimu wa kurejea katika misingi ya kuasisiwa kwa umoja huo.
