Mahakama yatoa siku 30 kwa Jamhuri kujadiliana na Salma kesi ya dawa za kulevya

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku 30 kwa upande wa Jamhuri katika kesi ya kusafirisha gramu 3.8 za dawa za kulevya aina ya bangi, inayomkabili mshtakiwa Salma Said (60), kuanza vikao vya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.

Hatua hiyo inatokana na mshtakiwa huyo kumwandikia barua Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), akiomba kufanya majadiliano ya kukiri makosa yake na kuimaliza kesi hiyo (plea bargaining).

Salma anakabiliwa na shtaka moja la kusafirisha gramu 3.8 za bangi, tukio analodaiwa kulitenda Juni 28, 2025 katika eneo la Mbezi Msigani.

Uamuzi wa kutoa siku hizo 30 kwa Jamhuri umetolewa leo, Jumatano, Aprili 22, 2026, na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Gwantwa Mwamkuga.

Hakimu Mwamkuga alimueleza mshtakiwa pamoja na upande wa mashtaka kuwa mahakama hiyo inatoa nafasi ya siku 30 kwa ajili ya pande zote kuanza majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo.

Hakimu Mwamkuga alisema Ijumaa ya Aprili 24, 2026 mazungumzo hayo yanatakiwa yaanze, na kwa kipindi hicho mahakama inasitisha usikilizwaji wa kesi kupisha makubaliano hayo.

Awali, wakili wa Serikali, Pacrasia Protas, alidai wamepokea barua ya mshtakiwa kuhusu kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo, hivyo wanaomba mahakama iwape nafasi ya kufanya makubaliano hayo.

“Kesi imeitwa kwa kutajwa, lakini mshtakiwa ameandika barua ya kukiri shtaka lake kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, hivyo kutokana na hali hiyo tunaomba mahakama itupe muda kwa ajili ya kufanya majadiliano na mtuhumiwa huyu,” alidai wakili huyo.

Hakimu Mwamkuga, baada ya kusikiliza shauri hilo, aliahirisha kesi hiyo hadi Mei 21, 2026, na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Salma anadaiwa kuwa Juni 28, 2025, katika eneo la Mbezi Msigani, Wilaya ya Ubungo, alikutwa akisafirisha gramu 3.8 za dawa za kulevya aina ya bangi kinyume cha sheria.

Kwa mara ya kwanza, alifikishwa mahakamani hapo Desemba 15, 2025 na kusomewa kesi ya jinai yenye shtaka moja la kusafirisha bangi.