Wanasheria waonya sintofahamu mradi wa Sinza mpya

Dar es Salaam. Wakati kukiwa na sintofahamu miongoni mwa wananchi kuhusu utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Sinza mpya, wanasheria waliozungumza na Mwananchi wameonya juu ya uwezekano wa kujitokeza migogoro iwapo hakutakuwa na uelewa wa kutosha kwa wamiliki wa ardhi, kabla ya kuanza kwa utekelezaji.

Wamesema ni muhimu Serikali ikahakikisha wamiliki wanapatiwa elimu ya kina kuhusu mradi huo, ikiwamo masuala ya fidia, makazi mbadala na mgawanyo wa faida pindi ujenzi utakapokamilika, ili kuepusha malalamiko na migogoro ya baadaye.

Mradi huo wa muda mrefu wa miaka 20 (2026–2046), umeibua hofu kwa baadhi ya wamiliki wa viwanja katika Kata ya Sinza, huku wengine wakidai kutoshirikishwa kikamilifu katika hatua za awali za maandalizi.

Hata hivyo, Serikali imesisitiza kuwa mradi huo ni muhimu kwa maendeleo jumuishi ya eneo hilo na hautamdhulumu mtu yeyote, kwa sababu utekelezaji wake utafanyika kwa kuzingatia sheria za nchi.

Chanzo kikubwa cha sintofahamu kimeelezwa ni mpango wa kuunganisha viwanja, ambapo Serikali imebainisha kuwa kutokana na udogo wa maeneo mengi ya Sinza, wamiliki wanane watalazimika kuunganisha viwanja vyao ili kupata eneo moja kubwa litakaloruhusu ujenzi wa majengo ya ghorofa kati ya nane hadi 20 kulingana na ramani ya mji.

Hata hivyo, imeelezwa kuwa yapo maeneo ambayo hayatahusishwa katika mpango huo kutokana na udongo kutostahimili majengo marefu.

Maeneo hayo ni pamoja na Sinza D na E, ambako majengo yatakayoruhusiwa ni ya ghorofa mbili hadi nne.

Akizungumzia mradi huo kwa mtazamo wa kisheria, mwanasheria Deo Bwire amesema changamoto kubwa hutokea pale utekelezaji wa miradi mikubwa unapoanza kabla ya wadau wakuu kuuelewa kikamilifu.

“Hakuna mwananchi asiyependa maendeleo, lakini akipinga mara nyingi ni kwa sababu hajapewa uelewa wa kutosha. Ni muhimu kwanza wamiliki waelimishwe kabla ya hatua za utekelezaji kuanza,” amesema Bwire.

Ameeleza kuwa mpango wa kuunganisha viwanja unaweza kuwa changamoto kubwa kisheria, kwa kuwa kila mmiliki ana hati yake ya ardhi, hivyo kuhitaji ufafanuzi wa kina kuhusu umiliki mpya utakaotokana na muunganiko huo.

“Wamiliki wanane wanaunganishwa kuwa eneo moja, nani atakuwa mmiliki halali? Hili ni jambo linalohitaji ufafanuzi wa kina ili kuepusha migogoro ya baadaye,” amesema.

Aidha, ameongeza kuwa ni muhimu tathmini ya thamani ya kila kiwanja ifanyike kwa uwazi ili kila mmiliki ajue haki yake na kile anachostahili endapo kutakuwa na fidia au mgawanyo wa faida.

Katika mkutano wa hivi karibuni kati ya Wizara ya Ardhi na wamiliki, Ofisa Mipango Miji, Emily Mwasogye alieleza kuwa katika baadhi ya majengo, wamiliki wanaweza kugawana umiliki kwa asilimia 50 kwa 50 na mwekezaji baada ya ujenzi kukamilika, hoja iliyozua maswali miongoni mwa wananchi.

Akifafanua hilo, Bwire amesema ni muhimu kubainisha wazi namna mgawanyo huo utakavyofanyika, ikiwamo nani atapata nini na kwa vigezo gani, ili kuondoa sintofahamu na migogoro inayoweza kujitokeza baadaye.

“Migogoro mingi huanzia pale watu wanapoingia kwenye mradi bila kuelewa kikamilifu. Ushirikishwaji wa wadau unapaswa kuwa endelevu hadi maswali yote yajibiwe,” amesema.

Kwa upande wake Aloyce Komba amesema utekelezaji wa mradi huo unapaswa kuanza kwa kufanya sensa ya kina ya wamiliki wa ardhi ili kubaini ukubwa wa maeneo, idadi ya wamiliki na aina ya uwekezaji uliopo katika kila kiwanja.

“Sinza si eneo la makazi tu, kuna majengo ya biashara na baadhi yana wamiliki zaidi ya mmoja. Hivyo, ni lazima kuwe na utaratibu unaoeleweka kwa kila kundi la wamiliki,” amesema.

Ameongeza kuwa fidia itakayolipwa haipaswi kuwa ya kiwango sawa kwa wote, bali izingatie thamani ya uwekezaji na ukubwa wa eneo la kila mmiliki.

Wanasheria hao pia wameonya dhidi ya matumizi ya nguvu katika utekelezaji wa mradi huo, wakisisitiza umuhimu wa mazungumzo na makubaliano ya hiari kati ya Serikali na wananchi.

Kwa mujibu wa sheria za Tanzania, ardhi ni mali ya umma inayosimamiwa na Serikali, lakini matumizi yake yanapaswa kuzingatia haki za wamiliki waliopo, ikiwamo fidia stahiki au makazi mbadala pale panapohitajika.

Kwa ujumla, wadau waho wanaona kuwa mafanikio ya mradi wa Sinza mpya yatategemea kiwango cha ushirikishwaji wa wananchi, uwazi wa taarifa na utayari wa kujibu maswali yote ya kisheria na kijamii kabla ya utekelezaji kuanza.

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Anna Henga amesema mradi huo ni mzuri kwa maendeleo kwani Sinza haijapangwa vizuri.

“Cha muhimu katika hili ni wamiliki wasionewe kwani hizi process huwa zina kesi nyingi, tunapokwenda kwenye maendeleo hayo watu wasionewe kama ni fidia wapewe waondoke au mradi ukikamilika haki itendeke katika mgawanyo wa asilimia,” amesema.

Hata hivyo, wamiliki wa ardhi maeneo ya Sinza, wameonekana kutaka fidia ili waondoke, baadhi wakitaka Sh1 bilioni na wengine hadi Sh3 bilioni, japo wizara kupitia kwa ofisa mipango miji, Emily imefafanua kwamba kuna njia tatu za wamiliki kushiriki kwenye mradi huo.

Njia ya kwanza ni wamiliki kugawana asilimia 50 kwa 50 na mwekezaji ambaye atatafutwa na wizara ndiye, wamiliki wanaweza kupangisha au kuuza maeneo yao na kuondoka kupisha mradi au wamiliki wanane wanaweza kukubaliana kuunganisha viwanja vyao na kujenga jengo jipya wenyewe kulingana na ramani.