Dar es Salaam. Mpango wa Tanzania wa kubadilisha mfumo wake wa elimu, unazidi kuchukua mwelekeo wa vitendo, huku walimu sasa wakiwa kitovu cha mageuzi yanayolenga kuzalisha nguvu kazi yenye ujuzi na iliyo tayari kwa ajira.
Hatua ya hivi karibuni ya kuwapeleka wakufunzi 150 wa elimu ya amali upande wa uhandisi nchini India kwa mafunzo ya kina ya ujuzi, inaashiria hatua muhimu katika mabadiliko ya nchi kuelekea mfumo wa elimu unaozingatia umahiri chini ya Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 (Toleo la 2023).
Hatua hii inaonesha dhamira na mkakati wa kushughulikia mojawapo ya changamoto sugu kwenye mfumo wa elimu ambayo ni uwezo wa walimu.
Wadau wamekuwa wakieleza wasiwasi kuhusu utekelezaji wa mkondo wa amali katika shule za sekondari uliotokana na mabadiliko ya sera na mitalaa.
Wakosoaji walielekeza kuwapo kwa pengo kubwa kati ya matarajio ya sera na hali halisi darasani: idadi ndogo ya walimu, ujuzi mdogo wa vitendo na ukosefu wa vifaa vya kutosha kusaidia ujifunzaji wa vitendo.
Maswali yaliendelea kuwepo kuhusu iwapo nchi ilikuwa inakwenda kwa kasi mno bila kuweka msingi unaohitajika.
Baadhi ya walimu wa masomo ya uhandisi wakiwa katika hafla ya kuagwa kabla ya kuanza safari ya kwenda mafunzoni nchini India.
Hata hivyo, hatua za hivi karibuni zinaashiria mwitikio wa matumaini kutoka upande wa Serikali.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amekuwa wazi kuhusu mwelekeo huo.
Akizungumza wakati wa hafla ya kuwaaga walimu hao, alieleza kuwa programu ya mafunzo nchini India ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa kuelekeza elimu kwenye ujuzi wa vitendo.
“Mwelekeo huu umekuwa ukisisitizwa mara kwa mara na Rais… hakuna kurudi nyuma,” Profesa Mkenda, akisisitiza dhamira ya kuendeleza mageuzi.
Alisema kuwa mpango wa mafunzo hayo ni utekelezaji wa sera ya elimu ya lazima ya miaka 10, unaolenga kujenga umahiri wa ufundishaji na kuandaa kizazi cha wataalamu wenye ushindani wa kimataifa.
Ushirikiano na India si mpya. Zaidi ya Watanzania 1,000 tayari wamenufaika na mafunzo kupitia programu ya Ushirikiano wa Kiufundi na Kiuchumi ya India (ITEC) katika sekta kama afya, Tehama na rasilimali za maji.
Hata hivyo, mkazo wa sasa kwa walimu wa ufundi unaonesha mwelekeo mahsusi wa kulinganisha elimu na mahitaji ya soko la ajira pamoja na uhalisia wa mapinduzi ya nne ya viwanda.
Mwalimu mmoja wa ufundi aliyechaguliwa kushiriki katika programu hiyo alielezea mpango huo kama “hatua ya mabadiliko makubwa,” akibainisha kuwa uzoefu wa vitendo katika nchi yenye mfumo uliokomaa wa mafunzo ya ufundi, utasaidia kuziba pengo kati ya nadharia na vitendo hapa nyumbani.
“Tumekuwa tukifundisha kwa zana chache na uzoefu mdogo. Mafunzo haya yatatusaidia kurejea tukiwa tumejiamini na mbinu mpya zitakazowanufaisha wanafunzi moja kwa moja,” alisema mwalimu huyo.
Wanufaika wengine wa mafunzo hayo, Judith Faustine kutoka Shule ya Sekondari Mwadui Ufundi shukuru Serikali kwa kuwapatia nafasi hii ya kipekee.
Wanasema ni heshima kubwa na fursa ya kuongeza maarifa yatakayowawezesha kuendeleza mageuzi ya elimu nchini.
Sauti kama hizi zinaakisi matumaini yenye tahadhari miongoni mwa waelimishaji, ambao wengi wao wamekuwa wakihisi kutokuwa tayari vya kutosha kukidhi mahitaji ya ufundishaji unaozingatia umahiri.
Mbali na mafunzo, Serikali pia imeanza kushughulikia upungufu kwenye miundombinu ambao ni changamoto nyingine kubwa iliyotajwa na wadau.
Serikali kwa upande wake inasema upanuzi wa warsha, ununuzi wa vifaa na usambazaji wa nyenzo za kujifunzia umeanza kutekelezwa hatua kwa hatua, hasa katika shule zilizoteuliwa kwa mkondo wa elimu ya amali.
Jitihada hizi zinaendana na mfumo mpana wa ushirikiano, unaojumuisha wadau mbalimbali wenye lengo la kuimarisha usimamizi wa walimu, kuboresha mazingira ya kujifunzia na kukuza elimu jumuishi.
Mfumo huo chini ya Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Elimu 2025/26–2029/30 unatambua kuwa juhudi za Serikali pekee hazitoshi, na hivyo kuhimiza ushirikiano na washirika wa maendeleo pamoja na sekta binafsi.
Wachambuzi wa elimu wanasema kuwa kuwafundisha walimu 150, licha ya kuwa ni jambo la kupongezwa, ni mwanzo tu wa kuandaa walimu zaidi kwani kadri shule zitakavyoanzisha mikondo ya ufundi, mahitaji ya walimu yataongezeka.
Maswali pia yanaendelea kuhusu uendelevu ikiwa walimu waliopata mafunzo wataweza kusambaza maarifa kwa wengine kwa haraka, na kama maendeleo endelevu ya kitaaluma yataendelezwa. Hata hivyo, Serikali inasema changamoto hizo zinashughulikiwa.
“Hatua kama kufanya kazi na India, nchi ambayo sekta ya ufundi imefanikiwa sana, ni mojawapo ya njia nyingi tunazotumia kushughulikia changamoto zinazohusiana na utekelezaji wa mahitaji ya elimu yetu,” anasema Profesa Mkenda.
Kwa upande wake, mdau wa elimu, Dk Thomas Jabir anasema mbinu ya sasa, inayochanganya uzoefu wa kimataifa, uwekezaji wa ndani na uratibu wa sera, inatoa njia pana zaidi ya kufikia mabadiliko.
Anabainisha kuwa ushirikiano na India unaonesha umuhimu wa kujifunza kutoka kwa nchi zilizofanikiwa kupitia mabadiliko kama haya.
“Uzoefu wa India katika kupanua mafunzo ya ufundi, kuunganisha teknolojia na kuhusisha elimu na viwanda unatoa maarifa ya vitendo ambayo Tanzania inaweza kuyaendana na mazingira yake,” anaeleza.
Wakati nchi ikielekea mwaka 2028, ambapo uandikishaji katika mikondo ya elimu ya kawaida na elimu ya amali unatarajiwa kuongezeka maradufu, Tanzania inaweza kuweka msingi wa mfumo wa elimu ulio imara zaidi na unaokidhi mahitaji ya wakati.
