CAG abaini dosari Tanesco, mabilioni ya IPTL

Dar es Salaam. Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebaini Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Serikali vinakabiliwa na deni la zaidi ya Sh268 bilioni, baada ya kushindwa kurejesha fedha zilizolipwa kwa niaba ya kampuni ya Independent Power Tanzania (IPTL).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya mwaka wa fedha unaoanzia Julai 2024 na kuishia Juni 2025, CAG anaonesha dosari katika ufuatiliaji wa mabilioni hayo ya fedha, hali inayotia shaka uwajibikaji wa taasisi husika na kuacha mzigo huo mikononi mwa walipa kodi.

Sambamba na hilo, ripoti hiyo imebainisha uchakavu wa mitambo na uzalishaji usioridhisha wa umeme kuwa miongoni mwa mambo yanayokwaza upatikanaji wa nishati hiyo kwa uhakika nchini.

Akizungumzia hilo na mengine ambayo CAG ameyabaini, Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, Lazaro Twange, amesema kuna utaratibu wa kisheria wa kujibu yanayohusu hoja zilizoibuliwa katika ripoti ya CAG, hivyo watatumia utaratibu huo kujibu.

Ameeleza baada ya kupita bungeni, kuna utaratibu wa maofisa husika kuitwa kwa ajili ya kujibu hoja zilizoibuliwa, badala ya kuijadili kwa njia ya simu.

“Ripoti ya CAG haijadiliwi kwa simu. Kuna utaratibu wa kujibu hoja zilizoibuliwa, ndugu mwandishi. Kwa hiyo, tutajibu kwa utaratibu huo,” amesema Twange.

Katika ripoti yake hiyo, CAG ameibua dosari kwa Serikali na Tanesco kushindwa kurejesha fedha zilizolipwa kwa niaba ya kampuni ya IPTL.

Kiasi kinachohusika ni Dola milioni 100 za Marekani (zaidi ya Sh268 bilioni), kilicholipwa kwa Benki ya Standard Chartered, tawi la Hong Kong, nchini China.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, malipo hayo yalifanyika katika mwaka wa fedha 2024/25 baada ya Serikali, kupitia Wizara ya Fedha, kuipatia Tanesco fedha kwa ajili ya maendeleo, kisha shirika hilo kulipa benki hiyo ili kulinda maslahi ya Serikali.

Hata hivyo, chanzo cha malipo hayo kinatokana na makubaliano ya awali ya mwaka 2013, na Serikali iliingia Hati ya Kujikinga na Hasara ili kujilinda dhidi ya madai yoyote yanayoweza kutokea kuhusiana na fedha za akaunti ya Escrow.

Aidha, makubaliano ya baadaye ya mwaka 2021 yalibainisha wazi kuwa kampuni ya IPTL ndiyo iliyokuwa na wajibu wa kulipa deni hilo kwa benki husika.

Licha ya kuwepo kwa masharti hayo, ukaguzi umebaini juhudi za kuhakikisha IPTL inarejesha fedha hizo hazijawa za kuridhisha.

CAG anaeleza hakukuwa na ushahidi wa kutosha unaoonesha kuwa hatua za ufuatiliaji zilichukuliwa kwa umakini, hali inayozua wasiwasi kuhusu uwajibikaji na usimamizi wa mikataba ya kifedha.

Ripoti hiyo inaonya kuwa hali hiyo inaacha mzigo kwa Serikali na walipa kodi, huku ikiibua maswali kuhusu ufanisi wa mifumo ya kudhibiti na kurejesha fedha za umma zinazolipwa kwa niaba ya wahusika wengine.

“Hali hiyo inaacha mzigo mkubwa kwa Serikali na walipa kodi, huku ikiibua maswali kuhusu ufanisi wa mifumo ya kudhibiti na kurejesha fedha za umma zinazolipwa kwa niaba ya wahusika wengine,” imeeleza ripoti hiyo.

Kutokana na hilo, CAG amesisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua madhubuti za kisheria na kifedha ili kuhakikisha IPTL inatekeleza wajibu wake wa kulipa deni hilo.

Aidha, katika kitabu cha ukaguzi wa ufanisi cha ripoti hiyohiyo, CAG amebaini uchakavu wa mitambo na uzalishaji usioridhisha wa umeme, hali inayohatarisha upatikanaji wa nishati ya uhakika.

Katika ripoti yake ya ukaguzi, CAG anaeleza mfumo wa uzalishaji umeme kwa kutumia maji, bila kujumuisha Mradi wa Bwawa la Julius Nyerere (JHPP), unategemea vituo vinane vyenye uwezo wa kuzalisha megawati 1,501.8.

Hata hivyo, vituo hivyo vinakabiliwa na changamoto ya uchakavu wa mitambo, hali inayolazimu kufanyika kwa ukarabati mkubwa au hata ubadilishaji wa baadhi ya vifaa.

Ripoti hiyo inaonesha baadhi ya vituo hivyo vimefikia au kuvuka muda wake wa matumizi uliopangwa.

Amevitaja vituo hivyo ni Kidatu, kilichoanza kazi mwaka 1975, chenye uwezo wa kuzalisha kilowati 204,000, na kituo cha Nyumba ya Mungu, kilichoanza kazi mwaka 1968, chenye uwezo wa kilowati 8,000.

Kufikia mwisho wa mwaka wa fedha 2024/25, vituo vyote viwili vilikuwa vimefikisha miaka 50 tangu kuanza kufanya kazi, muda ambao, kwa mujibu wa viwango vya kiufundi, unachukuliwa kuwa mwisho wa maisha ya kawaida ya mitambo hiyo.

Kutokana na hali hiyo, ufanisi wa uzalishaji umepungua maradufu. Uzalishaji katika Kituo cha Kidatu umefikia asilimia 49 ya uwezo wake, wakati Nyumba ya Mungu kikiwa katika asilimia 82.

Kushuka huko kwa uzalishaji, ripoti hiyo inasema, kunatafsiriwa kama ishara ya uchakavu wa mitambo na ukosefu wa uwekezaji wa kutosha katika matengenezo makubwa.

Aidha, ripoti inaeleza ukosefu wa mipango madhubuti ya ukarabati, ikiwamo mikakati ya kifedha, umechangia kwa kiasi kikubwa kuzorota kwa hali ya vituo hivyo.

“Badala ya kuwa na mpango wa muda mrefu wa kuboresha au kubadilisha mitambo, Tanesco imekuwa ikitegemea matengenezo ya kawaida ambayo hayatoshi kurejesha ufanisi wa awali wa uzalishaji,” imeeleza ripoti hiyo.

Matokeo yake, ripoti inasema, ni kuongezeka kwa gharama za matengenezo na kuharibika kwa mara kwa mara kwa mitambo, hali inayosababisha kukosekana kwa uhakika wa upatikanaji wa umeme.

CAG ameonya hali hiyo ni kinyume na Kanuni ya 9(2) ya Kanuni za Fedha za Umma (Usimamizi wa Mali za Umma) za mwaka 2024, ambayo inazitaka taasisi za umma kuhakikisha mali zake zinatunzwa na kuendelezwa ili kutoa huduma kwa ufanisi.

Mbali na changamoto za vituo vya maji, ukaguzi huo umebaini pia matatizo katika kituo cha kuzalisha umeme cha Ubungo I.

Kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha megawati 102, sawa na kilowati 893,520,000 kwa mwaka. Hata hivyo, uzalishaji halisi umekuwa wa kilowati-saa 393,282,000 kwa mwaka, sawa na asilimia 44 tu ya uwezo wake halisi.

CAG anafafanua kuwa kushuka huko kwa uzalishaji kunasababishwa na kuharibika kwa mashine tatu muhimu, ambapo hitilafu ya kwanza ilitokea Julai 31, 2022.

Pamoja na kupita kwa zaidi ya miaka mitatu tangu hitilafu hiyo itokee, ripoti inaonesha hakuna ukarabati wala ubadilishaji uliofanyika hadi kufikia Januari 15, 2026, wakati wa ukaguzi.

Hali hiyo, kwa mujibu wa ripoti, ni kinyume na Aya ya 14 ya Mwongozo wa Usimamizi wa Mali za Umma wa mwaka 2019, unaotaka taasisi kuchukua hatua za haraka pale mali inapoharibika ili kuzuia hasara zaidi.

“Kutokuchukuliwa kwa hatua kwa wakati kumeendelea kudhoofisha uwezo wa kituo hicho, huku kikizalisha chini ya nusu ya uwezo wake,” imeeleza ripoti.

Sababu kuu inayotajwa kuchangia hali hiyo, ripoti inasema, ni ukosefu wa fedha za kutosha kwa ajili ya ukarabati au ubadilishaji wa mitambo na udhaifu katika utekelezaji wa mipango ya matengenezo.

CAG anaonya hali hiyo si tu inapunguza uzalishaji, bali pia inasababisha kutokuwepo kwa uwiano kati ya takwimu za uwezo wa uzalishaji unaoripotiwa na uzalishaji halisi unaofikiwa.

Mkanganyiko huo wa takwimu, ripoti inasema, unaweza kuathiri upangaji wa sera na mipango ya nishati, kwani maamuzi yanaweza kufanyika kwa kuzingatia takwimu zisizoakisi hali halisi ya uzalishaji.

Hivyo, CAG anasisitiza umuhimu wa kurejesha ufanisi wa kituo hicho kupitia ukarabati au ubadilishaji wa mitambo, pamoja na kuhakikisha kunakuwepo bajeti ya kutosha kwa ajili ya matengenezo ya mara kwa mara.

Uzalishaji wa nguzo za zege janga

Wakati huohuo, ripoti hiyo inabainisha changamoto nyingine katika kampuni ya kuzalisha nguzo za Uueme za zege Tanzania, ambayo ni kampuni tanzu ya Tanesco.

Kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 2014 ikiwa na lengo la kuzalisha nguzo za zege na kufanya majaribio ya ubora wa vifaa, lakini kwa zaidi ya miaka 10 imekuwa ikisuasua kutekeleza jukumu hilo.

CAG anaeleza kampuni hiyo imeshindwa kuwekeza vya kutosha katika uzalishaji wa nguzo za zege kutokana na ufinyu wa fedha, na badala yake imekuwa ikitumia mtaji wa hisa uliotolewa na Tanesco kwa ajili ya gharama za uendeshaji.

“Hali hiyo imeifanya kampuni ishindwe kujitegemea na kutimiza malengo yake ya msingi,” imeeleza sehemu ya ripoti hiyo.

Kutokana na hali hiyo, CAG anasema kampuni imeendelea kutegemea maabara za nje kwa ajili ya vipimo vya ubora, jambo linalopingana na madhumuni ya kuanzishwa kwake kama chombo cha uzalishaji na uhakiki wa ubora kwa wakati mmoja.

Aidha, utegemezi huo unaongeza gharama na kupunguza ufanisi wa shughuli zake.

Katika mwaka wa fedha 2024/25, kampuni hiyo ilikabidhi asilimia 54 ya mkataba wenye thamani ya Sh5.83 bilioni kwa upande wa tatu, kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa kiwanda cha nguzo za zege mkoani Tabora.

“Hatua hiyo inaonesha udhaifu wa uwezo wa ndani wa kampuni na kuibua maswali kuhusu sababu za kuanzishwa kwake, iwapo haiwezi kutekeleza majukumu yake yenyewe,” amesema CAG kupitia ripoti hiyo.

Katika ripoti hiyo, CAG anapendekeza umuhimu wa kufanya tathmini ya kina ya vituo vya uzalishaji vilivyochakaa, kuandaa mipango ya ukarabati yenye uhakika wa kifedha na kuhakikisha kunakuwepo bajeti za kutosha kwa ajili ya matengenezo.

Aidha, anasema kuna haja ya kuimarisha usimamizi wa mikataba na kuhakikisha wahusika wote wanatekeleza wajibu wao wa kifedha.

“Iwapo hatua hizi zitachukuliwa kwa uzito unaostahili, zinaweza kusaidia kurejesha ufanisi wa uzalishaji wa umeme na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati nchini.

“Lakini bila mabadiliko ya haraka, changamoto hizi zinaweza kuendelea kuathiri juhudi za Tanzania katika kufikia uchumi wa viwanda unaotegemea nishati ya uhakika na endelevu,” anasema.