Global Publishers
April 14, 2026
0 Comments
Kiongozi wa Hezbollah, Naim Qassem, ametangaza wazi kupinga mazungumzo yanayotarajiwa kufanyika kati ya mabalozi wa Lebanon na Israel jijini Washington, D.C., nchini United States.
Akihutubia Jumatatu, Qassem alisema kundi hilo linakataa kabisa mazungumzo na kile alichokiita dola vamizi, akisisitiza kuwa majadiliano hayo hayana manufaa kwa Lebanon bila kuwepo kwa makubaliano ya kitaifa kuhusu mwelekeo wa mazungumzo hayo.
“Tunakataza mazungumzo haya. Hayana tija na yanahitaji makubaliano ya Waleabanon wote kabla ya kubadili msimamo kutoka kutokujadiliana hadi kujadiliana moja kwa moja,” alisema.
Katika hotuba yake, Qassem pia alitoa msimamo mkali wa kundi hilo, akiahidi kuwa Hezbollah haitasalimu amri katika mvutano unaoendelea.
“Hatutasalimu amri na tutaendelea kupigana hadi pumzi ya mwisho. Tutakabiliana na kudai haki, na tunataka kuwa mfano kwa dunia kwamba Lebanon, kupitia jeshi lake, wananchi wake na upinzani wake, haiyumbishwi na adui,” aliongeza.
Kauli hiyo inakuja wakati mvutano ukiendelea kuongezeka katika mpaka wa kusini mwa Lebanon, huku mashambulizi ya makombora yakirushwa kuelekea Israel katika siku za hivi karibuni.
Mazungumzo hayo yanayopangwa kufanyika Washington yanatarajiwa kuwa sehemu ya juhudi za kidiplomasia za kupunguza mivutano, lakini msimamo wa Hezbollah unaashiria changamoto kubwa katika kufikia suluhisho la kudumu.