Matumizi yasiyostahili, yasiyo na tija yapoteza Sh126.18 bilioni

Dar es Salaam. Wakati mjadala wa uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za umma ukiendelea kupewa kipaumbele, ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2024/25 imebaini matumizi yasiyofaa ya Sh126.18 bilioni katika mashirika ya umma na taasisi za Serikali.

CAG anaeleza tatizo hilo linatokana na udhaifu wa mifumo ya udhibiti, ukiukwaji wa sheria na matumizi ya fedha nje ya taratibu rasmi za kifedha na utumishi wa umma.

“Katika mwaka ulioishia Juni 30, 2025, nilibaini mashirika tisa yenye matumizi yasiyostahili ya Sh8.56 bilioni,” inaeleza ripoti hiyo.

Kiasi hicho kimeongezeka kwa asilimia 27, ukilinganisha na upotevu wa Sh6.75 bilioni ulihusisha mashirika 10 mwaka uliopita (2023/24), hali inayoibua maswali kuhusu ufanisi wa udhibiti wa matumizi ya fedha za umma.

Uchambuzi unaonesha fedha hizo zilihusisha malipo ya posho zisizoidhinishwa, mishahara isiyoendana na miundo ya utumishi na malipo kwa watu wasiostahili, wakiwemo waliokwishaondoka kazini au waliokaimu bila kibali.

Mashirika yaliyotajwa katika kundi hili ni Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Kampuni ya Gesi Tanzania (GASCO), Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).

Mengine ni Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Musoma (Muwasa), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB), Mfuko wa Huduma ya Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro (NCAA) na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC).

Katika baadhi ya taasisi hizo, ATCL ilibainika kulipa mishahara na posho nje ya viwango vilivyoidhinishwa, huku GASCO ikitoa posho za mazingira magumu nje ya utaratibu rasmi. Dawasa nayo ilifanya malipo ya posho za kazi za ziada na hatari ambazo hazijaidhinishwa na mamlaka husika.

CAG pia amebaini matumizi yasiyo na tija ya Sh117.62 bilioni katika mashirika 16 ya umma. Haya yanajumuisha riba za mikopo, faini za ucheleweshaji wa malipo ya kodi na pensheni, malimbikizo ya madeni, pamoja na gharama zinazoweza kuepukika kutokana na usimamizi duni wa mikataba na fedha.

Mashirika yaliyohusika ni Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Dawasa, Kampuni ya Uwekezaji ya TANOIL (TANOIL), Bohari Kuu ya Dawa (MSD), Chuo Kikuu Mzumbe (MU), Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Mamlaka ya Elimu Tanzania (TIE) na Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB).

Mengine ni Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Babati (Bawasa), Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (Tawiri), Kituo cha Zana za Kilimo na Teknolojia Vijijini (CAMARTEC), Bodi ya Maziwa Tanzania (TDB) na Chuo cha Usimamizi wa Wanyamapori Afrika – Mweka (CAWM).

Katika ripoti hiyo, Tanesco imebeba sehemu kubwa ya gharama hizo kutokana na riba na malimbikizo ya muda mrefu ya malipo, huku taasisi nyingine zikikumbwa na faini za ucheleweshaji wa kodi, pensheni na malipo ya wakandarasi.

CAG anaonya kuwa, katika baadhi ya mashirika hayo, fedha zililipwa bila uthibitisho wa kutosha au kwa watumishi wasiostahili, jambo linaloonesha udhaifu mkubwa wa mifumo ya udhibiti wa ndani.

“Upungufu huu unaonesha matumizi mabaya ya fedha za umma na kuhatarisha ufanisi wa taasisi,” inaeleza ripoti hiyo.

CAG amependekeza kuimarishwa kwa mifumo ya udhibiti wa ndani ili kuhakikisha malipo yote yanafanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na mikataba.

Amesisitiza kurejeshwa kwa fedha zote zilizolipwa isivyo halali, pamoja na kuhakikisha posho za kukaimu na maslahi mengine zinapitishwa na Katibu Mkuu (Utumishi) kabla ya malipo kufanyika.

Kwa ujumla, ripoti hii inaonya kuwa, bila hatua madhubuti za uwajibikaji na mageuzi ya mifumo ya fedha, mashirika ya umma yataendelea kupoteza mabilioni ya fedha za wananchi kupitia matumizi yasiyofaa, hali inayodhoofisha utoaji wa huduma na maendeleo ya taifa.