Rais Mwinyi mgeni rasmi The Citizen Rising Woman Zanzibar

Dar es Salaam. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi anatarajiwa kuhudhuria Tamasha la The Citizen Rising Woman Initiative (RWI), ambalo kwa mara ya kwanza linafanyika visiwani Zanzibar.

Huu ni mwaka wa sita kwa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) kuendesha tamasha la RWI kwa Tanzania Bara, na mwaka wa kwanza kwa Zanzibar, ambapo litafanyika Jumatano, Aprili 15, 2026.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni Give to Gain: Elevate Her Rise na toleo la Zanzibar linafanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Zanzibar, Airport mjini Zanzibar.

Toleo hilo la RWI Zanzibar linaendana na ajenda ya kimataifa ya Beijing+30, ambapo mwaka 2026 unaashiria dhamira mpya ya kuharakisha uongozi wa wanawake, ushiriki wao katika uchumi na ushawishi wao katika jamii.

Mkuu wa Masoko, Uhusiano wa Mashirika na Uendelevu wa MCL, Edson Sosten, amesema kampuni hiyo haianzi kutoka sifuri; toleo la sita linakuja na maarifa, mitandao na matokeo yanayopimika kuanzia Dar es Salaam hadi Zanzibar.

“Nguvu ya Rising Woman imejengwa katika miaka sita ya mwendelezo, sasa ikipanua wigo wake kufungua fursa mpya Zanzibar. Baada ya miaka sita ya kuleta matokeo Dar es Salaam, leo ni hatua ya kihistoria ambapo Rising Woman inatua Zanzibar kwa mara ya kwanza. Zanzibar si eneo jipya tu; ni upanuzi wa kimkakati wa jukwaa ambalo limejaribiwa, kuboreshwa na kuthibitishwa kwa miaka sita,” amesema Sosten.

Chini ya kaulimbiu ya Give to Gain: Elevate Her Rise, programu ya mwaka huu inasisitiza thamani ya kuwekeza kwa wanawake kupitia ushauri, fursa, rasilimali na utetezi, kwa kuwa kuwawezesha wanawake si tu wajibu wa kijamii, bali pia ni njia iliyothibitishwa ya kukuza taasisi na maendeleo ya taifa.

Toleo la mwaka huu lina nguzo kadhaa za kimkakati zinazolenga kupanua athari za wanawake katika jamii. Nguzo hizo ni pamoja na kuimarisha uongozi na ushawishi kwa kuongeza uwakilishi wao katika nafasi za juu za uamuzi, kukuza uwezeshaji wa kiuchumi kupitia upatikanaji wa fedha na masoko, pamoja na kuimarisha sera na mifumo ya utetezi ili kuhakikisha uwajibikaji katika utawala unaozingatia usawa wa kijinsia.

Mhariri Mtendaji wa MCL, Mpoki Thomson amesema hafla hiyo itajumuisha mjadala wa jopo, utakaofuatiwa na utoaji wa tuzo kwa taasisi zinazokuza usawa wa kijinsia na kuwa na uwakilishi mkubwa wa wanawake katika uongozi na maamuzi.

Tuzo nyingine, ijulikanayo kama Woman of the Future Award, inalenga kutambua mipango yenye athari inayokuza usawa wa kijinsia kupitia sera na mifumo inayowawezesha wanawake kupanda ngazi za uongozi.

“Katika jitihada zetu za kuwawezesha Watanzania, hatuwezi kuwaacha Wazanzibari. Visiwa hivi vina nafasi muhimu katika maendeleo ya nchi yetu, ambapo wanawake wanachangia kwa kiasi kikubwa katika sekta mbalimbali, kuanzia utalii, ubunifu hadi uchumi wa buluu.

“Kupitia Rising Woman, tumekuwa tukisherehekea mafanikio na hatua zilizofikiwa na wanawake wa Zanzibar. Ili kuendeleza kasi hii, tumetenga tukio hili maalumu kwao, pamoja na kurasa maalumu zitakazohifadhi na kusambaza habari zao duniani,” amesema Thomson.

Mjadala wa jopo utajikita katika nafasi ya wanawake katika kuchochea ukuaji jumuishi wa kiuchumi na maendeleo ya Zanzibar.

Wazungumzaji ni pamoja na Waziri wa Elimu, Leyla Mussa; Mkurugenzi Mtendaji wa Azania Bank, Ester Mangenya; Waziri wa Vijana, Ajira na Uwezeshaji, Shabani Omary; pamoja na Leyla Ghaid kutoka Tony Blair Institute for Global Change.

Aidha, kongamano hilo litaongozwa na Nafisa Jiddawi, huku wadhamini wa hafla hiyo wakiwa ni Azania Bank, CRDB Bank, NMB Bank, ORYX Energies, Tanapa, Zenji Zuri Consultancy na Zanzibar Economic Empowerment Agency (ZEEA).