Kisa Katiba Mpya, Ado agombaniwa kama mpira wa kona bungeni

Dodoma. Hakuna kauli iliyonjema zaidi ya hii, kwamba aligombaniwa kama mpira wa kona ambao kila mtu anataka kupiga kichwa.

Ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini (ACT-Wazalendo), Ado Shaibu aliyegombaniwa na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiwemo Naibu Waziri kutokana na mchango wake alioutoa jana Jumatatu, Aprili 13, 2026.

Alikuwa akichangia makadirio ya mapato na matumizi ya ofisi ya waziri mkuu ya mwaka 2026/27 ya Sh12.5 trilioni aliyoiwasilisha Aprili 1 na itahitimishwa kesho Jumatano, Aprili 15, 2026 kwa Hotuba ya Waziri Mkuu ya maombi ya fedha kwa mwaka 2026/27 mchango alioutoa jana Jumatatu Aprili 13,2026.

Shaibu ni kama aliwagusa mahala ambapo hawakupataka ndipo wakamshukia kama mwewe kwa kumuombea taarifa kiasi cha kuvuruga mpangilio mzima wa mchango wake ingawa muda wote alijitahidi kutokuhama kwenye mrengo alioutaka.

Sababu iliyowasimamisha kundi la wabunge wa CCM ni pale alipogusa suala la Katiba mpya akisema hajaoa likitiliwa mkazo kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ambalo lilionyesha kuagusa wabunge wa CCM, Ester Bulaya (Bunda Mjini) na Timotheo Mzava (Korogwe Vijijini) lakini ikamlazimu Naibu Waziri wa Tamisemi, Dk Festo Dugange.

Wote hao kila mmoja aliposimama alionesha kutokubaliana na Shaibu wakisema Serikali ya CCM imeahidi suala hilo kulitekeleza na lipo kwenye Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2025/2030.

Hivi umewahi kumwona mwene anavyomvamia kuku mwenye vifaranga, je umewahi kushuhudia ukali wa mtu mwenye kidonda kilichoanza kupona akiguswa eneo hilo hata kama ni kitambaa laini kikimpitia kwenye eneo hilo.

Katika mchango wake, Shaibu alisema haoni nia njema ya Serikali katika utungwaji wa Katiba mpya kwani jambo hilo halikuzungumzwa kwenye hotuba ya Waziri Mkuu licha ya kuwa ilikuwa ni ahadi ya Serikali.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, sioni nia njema ya Serikali katika hili, ikumbukwe suala la Katiba mpya siyo takwa la CCM wala Serikali pekee, ni dai la Watanzania, sioni mahali popote kwenye hotuba ya Waziri Mkuu ambapo imezungumzwa kuhusu Katiba mpya,” alisema Shaibu.

Kauli hiyo ilimfanya Bulaya kusimama kwa mujibu wa kanuni za Kibunge kuomba ampe taarifa mzungumzaji ambapo alimweleza kuwa Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ina nia njema na kwamba jambo hilo litakuja kwa wakati wake.

Mwenyekiti aliyekuwa akiongoza kikao, Cecilia Pareso alimpa nafasi Shaibu kama amepokea taarifa na akasema haipokei akaendelea ndipo akaombewa taarifa tena kutoka Mzava akimweleza suala la Katiba Mpya ni takwa la lazima katika Ilani ya uchaguzi ya CCM.

Taarifa hiyo haikumshibisha Mbunge huyo akaikataa ndipo akasimama Naibu Waziri, Dk Dugange ambaye nayo aliikataa kisha akasimama kwa mara ya pili Bulaya akisisitiza mbunge huyo kuwa na utulivu muda ukifika suala la Katiba litakuja.

Wakati wabunge hao wakimpa taarifa, kulikuwa na wabunge wengine kutoka CCM ambao nao walikuwa wanaomba kutoa taarifa lakini muda wa mchangiaji ulikuwa umekwisha.

Shaibu aliamua kuachana na hoja hiyo ya katiba mpya na kuhamia suala la rushwa akisema haoni hasa mikakati ya kupambana nayo kama alivyokuwa akifanya aliyewahi kuwa Waziri Mkuu, Edward Sokoine kwa kuikemea hadharani na kuwashughulikia waliotuhumiwa.

Katika hitimisho la mchango wake, Mbunge huyo wa Tunduru Kaskazini alisema pamoja na usumbufu waliomfanyia lakini ujumbe utakuwa umewafikia walengwa na Watanzania wametambua mkwamo wa Katiba mpya unaanzia wapi.