Askofu Mfumbusa afariki, TEC yaelezea mchango wake

Dodoma. Kufuatia kifo cha Askofu wa Jimbo Katoliki Kondoa, Bernardin Mfumbusa, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limesema kiongozi huyo ameitendea haki taaluma yake ya mawasiliano na kukuza waandishi wengi nchini.

Kwa mujibu wa TEC, Askofu Mfumbusa ametoa mchango mkubwa wa kuendeleza kitivo cha mawasiliano alipokuwa Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Agustino.

Kulingana na baraza hilo, Askofu Mfumbusa alifariki dunia jana, Aprili 14, 2026, katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, jijini Dodoma kwa tatizo la shambulio la moyo, alipokuwa akipatiwa matibabu ya dharura.

Kwa mujibu wa taarifa za TEC, mipango ya mazishi inaendelea kufanyika na marehemu anatarajiwa kuzikwa Aprili 22, 2026, katika Jimbo Katoliki Kondoa.

Askofu Mfumbusa alizaliwa Aprili mosi, 1962, mjini Kondoa na kupadrishwa Juni 14, 1992. Baadaye aliteuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Katoliki Kondoa Machi 12, 2011 na kuwekwa wakfu Mei 15, 2011. Katika maisha yake ya utumishi, alilitumikia kanisa kwa miaka 33 kama padri na miaka 14 kama askofu.

Mbali na majukumu yake ya kichungaji, marehemu alitambulika kama gwiji wa mawasiliano ndani ya kanisa. Aprili 9, 2026, Baba Mtakatifu, Pope Leo XIV, alimteua kuwa Rais wa Kamati ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Afrika na Madagascar (CEPACS), na pia mjumbe wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii.

Akielezea mchango wa Askofu Mfumbusa kwenye taaluma ya habari, Katibu Mkuu wa TEC, Padri Charles Kitima, amesema kiongozi huyo alifundisha Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino kuanzia mwaka 2002 hadi 2011,

akifanya pia tafiti pamoja na kulea waandishi wa habari.

“Alikuwa mtu wa viwango katika taaluma ya uandishi, na ndiyo maana mpaka sasa alikuwa ameteuliwa kuwa Rais wa idara inayohusika na mawasiliano ya Kikatoliki Afrika nzima, katika mabaraza ya maaskofu kwa nchi 53.

“Ameitendea haki taaluma yake na amelea waandishi wa habari wengi, na wengi wanaendelea kulitumikia Taifa kwa uelewa mkubwa. Pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vyombo vya Habari (MCT). Tunamshukuru Mungu kutupatia zawadi ya Askofu Mfumbusa,” amesema.

Amesema uelewa wa Askofu Mfumbusa katika fani ya mawasiliano ulimfanya kuendelea kuwa mtumishi muhimu wa kanisa katika eneo hilo.

Amesema Askofu Mfumbusa alikuwa mbobezi mkubwa katika teknolojia za mawasiliano na amekuwa msaada mkubwa kwa Kanisa Katoliki Afrika, hususan Afrika Mashariki na Kati.

Akizungumzia kifo chake, Katibu Mkuu wa TEC, Padri Kitima, amesema baada ya Askofu Mfumbusa kupata shambulio la moyo akiwa jimboni kwake, alikimbizwa Hospitali ya Benjamin Mkapa, ambapo alipatwa tena na tatizo hilo na kumsababishia mauti.

“Kwa masikitiko makubwa tumempoteza askofu kijana mwenye miaka 64, aliyezaliwa mwaka 1962. Aliteuliwa kuwa askofu mwaka 2011 akiwa askofu mwanzilishi wa Jimbo Katoliki Kondoa,” amesema.

Awali, amesema askofu huyo alikuwa akisumbuliwa na tatizo la upungufu wa damu, na matibabu yake alikuwa akipatiwa nchini Kenya, na alipopata nafuu alirejea nchini.

“Amerudi nyumbani Ijumaa, Aprili 11, 2026, ndipo akapata shambulio la moyo. Aliporejea hali yake ilikuwa nzuri, lakini tatizo hili jipya  alilopata ndilo limemuondoa,” amesema.

Padri Kitima amesema mazishi ya askofu huyo yatafanyika wiki ijayo, na kwa sasa wanasubiri ratiba rasmi kutoka jimboni.

“Tutapewa taarifa rasmi kwamba mazishi yatakuwa wiki ijayo. Kwa sasa, kamati za kijimbo zinafanya taratibu zake ziweze kutup muda,” amesema.