Polisi yathibitisha kumuhoji mpenzi wa Ashlee aliyefia Zanzibar

Dar es Salaam. Hatimaye mpenzi wa mhamasishaji wa mitandao ya kijamii kutoka Marekani, Ashly Robinson, maarufu Ashlee Jenae, Joe McCann anahojiwa na polisi visiwani Zanzibar.

Ashlee, alifariki dunia Aprili 10, mwaka huu visiwani Zanzibar alikokwenda kwa matembezi ya kitalii na mpenzi wake, Joe McCann, ambaye alimchumbia siku sita kabla ya kifo chake wakiwa visiwani humo.

Taarifa kuhusu kuhojiwa kwa mpenzi wake huyo, imetolewa leo, Jumanne Aprili 14, 2026 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kaskazini Unguja, Benedict Mapujira, alipozungumza na Mwananchi.

Katika taarifa yake hiyo, amesema pamoja na uchunguzi ambao tayari ulishafanyika, lazima jeshi hilo liendelee na mahojiano kujiridhisha kama kuna jinai, hivyo inawahoji watu kadhaa.

“Lazima tuhoji watu wa hotelini, tumuhoji yule mchumba wake, kila kitu ili baadaye tupate hitimisho kama kuna jinai au hatuna jinai,” amesema na alipoulizwa kuhusu alipo McCann alijibu, bado anahojiwa.

Alipoulizwa zaidi kama wanamshikilia McCann, Kamanda Mapujira amejibu, “unajua ukiambiwa unaisaidia polisi unakuwa umebanwabanwa, hata kama una uhuru lakini ukiambiwa unaisaidia polisi taabu.”

Amesisitiza bado uchunguzi wa kitaalamu unaendelea, ikiwemo wa ziada utakaohusisha eneo la kichwa cha marehemu ili kubaini kwa kina chanzo cha kifo chake.

Hata hivyo, amesema linapotokea suala kama hilo linalomuhusisha mgeni, ubalozi wa nchi ambayo mtu huyo anatoka huwa inatoa mwakilishi wao kusimamia mambo yote, ukiwemo uchunguzi.

Amesema ubalozi utatoa mwakilishi huyo baada ya kuandikiwa na ofisa wa upande wa Zanzibar anakuwepo wakati uchunguzi ukiendelea kufanyika.

Jana, Jeshi la Polisi Zanzibar liliweka wazi kuwa Ashlee alipatikana akiwa hai, akaokolewa na kupelekwa hospitalini, ambako alifariki dunia baadaye.

Mama wa marehemu, Yolanda Denise amesema tukio hilo halieleweki, akibainisha kuwa binti yake alikuwa safarini kusherehekea siku yake ya kuzaliwa akiwa na mchumba wake, kabla ya kupoteza maisha ghafla.

Aliongeza kuwa, mawasiliano kutoka kwa mchumba huyo yalikuwa hafifu, na baada ya taarifa za awali, hakuwasiliana nao tena, huku familia ikipata taarifa za kifo kupitia hoteli.

Hoteli ya Zuri Zanzibar, imethibitisha kushirikiana na mamlaka za uchunguzi pamoja na ubalozi wa Marekani, ikieleza kusikitishwa na tukio hilo.

Kwa upande wake, Kaimu Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale, Mudrick Ramadhan Soraga, amesema kinachoendelea sasa ni kusubiri uchunguzi wa kitaalamu ukamilike na kuona hasa tatizo lilikuwa nini.

Amesema wanaheshimu uamuzi wa familia ya marehemu ambayo imetoa taarifa kwamba kama Serikali wasilijadili na kulitolea taarifa yoyote mpaka upelelezi wake utakapokamilika.

“Kwa hiyo sisi hatuna maoni zaidi. Upelelezi unaendelea, tusubiri wataalamu watakapotuletea taarifa rasmi,” amesema Soraga ambaye pia ni Waziri wa Mawasiliano, Teknoloji ya Habari na Ubunifu

Amesema watatoa ushirikiano kwa mamlaka zote na wameshaanza mazungumzo na ubalozi wa Marekani kwa kushirikiana na vyombo vya usalama kutuliza taharuki na kuuhakikishia umma kwamba Zanzibar ni sehemu salama.

“Tunapokea wageni wengi na matukio kama hayo sio kawaida tunachofanya ni kuhakikisha tunapata taarifa za kutosha ya kilichojiri na kuhakikisha wageni wetu wanaendelea kuwa salama na jukumu kubwa ni kuhakikisha ulinzi na usalama unasimamiwa kikamilifu,” amesema Soraga.

Amesema wanaendelea kufanya kazi kwa ukaribu na vyombo na ubalozi wa Marekani kuhusiana na mambo mengine mahususi kumuhusu Ashlee.

Kuhusu muda wa kupata ripoti, amesema hawajajua isipokuwa ni uratibu uliopo kwa sasa na wanaendelea katika ngazi ya watendaji.