Kijana auawa kwa kipigo Arusha, uchunguzi unaendelea

Arusha. Kijana Adam Bakari (23), mkazi wa Mbauda jijini Arusha, ameuawa kwa kipigo na watu wanaodaiwa kumtuhumu kuhusika na wizi wa Sh5.8 milioni na simu mbili.

Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, amesema Jeshi la Polisi limeanza uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa tukio hilo, na taarifa kamili itatolewa mara uchunguzi utakapokamilika.

“Hilo tukio tunaendelea kuchunguza undani wake, tukikamilisha tutawajuza tulichobaini,” amesema Kamanda Masejo bila kueleza kama kuna mtu yeyote aliyekamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Kwa upande wake, dada wa marehemu, Diana Moshi, amesema kuwa kwa mujibu wa mashuhuda, mdogo wake aliuawa usiku wa Aprili 10, 2026 katika eneo la Mbauda baada ya kuitwa na rafiki yake.

Amesema siku ya tukio, marehemu alipigiwa simu jioni na rafiki yake na  kuombwa wakutane katika kona ya Mbauda.
Amesema hata hivyo, kabla hawajakutana alikamatwa na wanaume watatu waliompeleka katika nyumba ya mwanamke mmoja jirani yao aliyedai kuibiwa, ambako alidaiwa kuanza kupigwa na kumtesa wakimtuhumu kuwaibia fedha na simu.

Ameeleza kuwa jitihada za marafiki wa marehemu kumtetea hazikuzaa matunda, huku akidai kuwa watesaji waliendelea kumpiga na hata kumrekodi wakimlazimisha akiri alipoziweka fedha hizo bila mafanikio.
“Walikuwa wanampiga huku wakimrekodi wakimtaka aseme fedha zilipo bila mafanikio, Mwishowe walimuua na baadaye kuutupa mwili wake barabarani,” amedai.

Diana ameongeza kuwa familia ilipokea taarifa za kifo hicho asubuhi, na walipofika eneo la tukio walikuta tayari polisi wameuchukua mwili na kuupeleka Hospitali ya Muriet jijini Arusha.
Amesema mwili wa marehemu ulikuwa na majeraha makubwa sehemu mbalimbali za mwili, ikiwemo kichwani, mgongoni na miguuni, hali inayoashiria kupigwa kikatili.
Aidha, ameomba mamlaka husika kuchukua hatua kali dhidi ya waliohusika, kwani ndugu yake hakuwa mwizi kama inavyodaiwa.

“Mdogo wangu si mwizi, wanamsingizia tu, Naomba Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wote waliohusika kwani wanafahamika, lakini hadi sasa hakuna aliyekamatwa,” amesema Diana.

Mmoja wa marafiki wa marehemu, Huseni Said amesema kuwa siku ya tukio alisikia rafiki yao amechukuliwa na watu wanaodai kuwaibia na walipofuatilia walijua nyumba waliyoingia.

“Tuliingia hiyo nyumba na kukuta wanampiga mwenzetu na kumtesa huku wakimrekodi na tulipomtetea walianza kutupiga na sisi kisha wakatutoa nje na  kutufukuza.”

“Tuliona hiyo sio haki, kumpiga mtu ndani na kituo cha polisi kipo karibu hivyo tuliamua kwenda Polisi kutoa taarifa na walipokuja tulikuta wameshamuua na kumtupia nje ya nyumba hapo barabarani,”amesema Said.

Amesema kuwa pamoja na askari hao kuonyeshwa waliosababisha mauaji, na ushahidi wa video hadi sasa hakuna aliyekamatwa kuhojiwa.

Naye jirani wa marehemu, Ally Hamad, amesema kijana huyo alikuwa akijishughulisha na kazi za bodaboda pamoja na upakaji rangi nyumba ili kujipatia kipato.

“Kuhusu tuhuma za wizi siwezi kuthibitisha, kwa sababu mara nyingi huwa sipo nyumbani mchana, Tunakutana zaidi usiku baada ya kila mmoja kurejea nyumbani,” amesema Ally.