Makambako. Katika jitihada za kukabiliana na mikataba kandamizi inayowakandamiza madereva bodaboda, Mbunge wa Makambako na Waziri wa Kilimo, Daniel Chongolo ametoa msaada wa Sh10 milioni kwa umoja wa madereva hao ili kuwawezesha kujikomboa kiuchumi.
Fedha hizo zimetolewa kwa lengo la kuwa dhamana itakayowawezesha madereva bodaboda kukopesheka pikipiki kutoka taasisi za kifedha, hatua inayotarajiwa kupunguza utegemezi wa mikataba yenye masharti magumu kutoka kwa wamiliki wa vyombo hivyo.
Akizungumza Aprili 15, 2026, baada ya kukabidhi fedha hizo, Katibu wa Mbunge wa Makambako, Imani Fute amesema msaada huo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa mwaka jana, huku akiwataka wanachama hao kupanga matumizi bora ya fedha hizo ili kufikia malengo yao ya kiuchumi.
Kwa upande wao, madereva bodaboda wameeleza kuwa msaada huo utakuwa mkombozi kwao. Wamesema kwa muda mrefu wamekuwa wakifanya kazi chini ya mikataba inayowalazimu kulipa kiasi kisichopungua Sh10,000 kwa siku kwa wamiliki wa pikipiki, hali inayowakosesha faida.
Mmoja wa madereva hao, Hassan Ndimbaya, alimshukuru mbunge huyo akisema msaada huo ni wa kipekee na wa kwanza kuwahi kutolewa kwao tangu waanze kazi hiyo.
“Tunamshukuru mbunge wetu, hatujawahi kupata ufadhili kama huu. Alianza kutusaidia kwenye leseni na sasa ametupa mtaji,” amesema Ndimbaya.
Naye Judith Nyakasonga amesema awali alidhani ahadi hiyo ni ya kisiasa, lakini utekelezaji wake umempa matumaini mapya.
“Kwa kweli fedha hii ni kubwa kwetu. Tunaweza kupata pikipiki zaidi na kuachana na mikataba kandamizi, tukijitegemea kupitia umoja wetu,” amesema Judith.
Katibu wa Umoja wa Madereva Bodaboda Makambako, Victor Nyato, amesema fedha hizo zitaongeza nguvu ya mfuko wao wa pamoja na kunufaisha wanachama wote, hasa katika kuboresha mazingira yao ya kazi.
Amebainisha kuwa changamoto kubwa inayowakabili ni mikataba isiyo na usawa inayowaumiza kiuchumi; hivyo, msaada huo utakuwa chachu ya mabadiliko.
Wakati huo huo, Mkaguzi wa Polisi Wilaya ya Kipolisi Makambako, Francis Ngatunga, amewataka madereva hao kuongeza umakini katika kulinda pikipiki zao kutokana na ongezeko la matukio ya wizi.
Amewahimiza pia kutoa taarifa kwa vyombo vya dola wanapobaini uhalifu ili kuimarisha usalama wa mji huo.
