SMZ kuimarisha upatikanaji dawa kwa asilimia 100

Unguja. Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) imesema inaendelea kuchukua hatua mathubuti kufanya mageuzi makubwa ya sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuongeza bajeti ya dawa, ili kuondoa changamoto ya wananchi kukosa huduma hizo wanapokwenda katika vituo vya afya.

Hayo yamebainishwa leo Aprili 15, 2026 na Kaimu Waziri wa Afya, Dk Saada Mkuya wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 15 wa mapitio ya sekta ya afya, akisema wanaongeza uwazi na uwajibikaji kuhakikisha fedha zinasimamiwa kikamilifu.

“SMZ inakusudia kuongeza bajeti ambapo mwaka 2023/24 ilitenga Sh20.4 bilioni kwa ajili ya dawa na imepanda mpaka Sh36.1 bilioni mwaka 2024/25.”

Kwa upande wa rasilimali watu ambayo bado ni changamoto, Dk Saada amesema wamehakiki katika kila ngazi na kubaini wana uhaba wa wafanyakazi 3,574 katika sekta ya afya ambapo Serikali inaendelea kuziba pengo hilo kwa kutangaza nafasi zaidi ya 1,500.

Dk Saada ambaye pia ni Waziri Ofisi ya Rais Ikulu, amesema wameweka lengo ifikapo mwaka 2027 kuwe na wahudumu wa afya ngazi ya jamii wapatao 3,000 na mpaka sasa wapo 2,292.

Naye Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk Ndoungou Salla Ba amesema katika mwaka uliopita, wameona maendeleo mazuri kuelekea ufadhili endelevu wa afya, yakichangiwa na ongezeko la michango ya ndani pamoja na uzinduzi wa Mfuko wa Huduma za Afya Zanzibar.

Amesema safari kuelekea ufadhili wa moja kwa moja wa vituo vya afya ina uwezo wa kubadilisha kabisa huduma za afya ya msingi Zanzibar, kwa kuongeza uhuru wa uamuzi huku ikiimarisha uwajibikaji kupitia kamati za usimamizi wa vituo vya afya.

“Ni lazima tufanye vizuri zaidi na tuharakishe safari, Tuna utapiamlo, tuna upungufu wa virutubisho  na tumeona viwango vinavyopanda vya unene kupita kiasi,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu Wizara ya Afya, Dk Amour Mohamed amesema majadiliano hayo yamethibitisha tena wajibu wa pamoja kuhakikisha mipango inayotegemea ushahidi na maamuzi yanayoongozwa na data ndiyo yanayoongoza sekta ya afya.

Amesema licha ya mahudhurio ya kwanza ya kliniki ya wajawazito (ANC) kuongezeka kwa kiasi kikubwa katika kipindi cha 2022–2024, huku kiwango cha mawasiliano ya kwanza kikiongezeka hadi zaidi ya asilimia 80 mwaka 2024/25, changamoto bado zipo, hasa katika kutambua na kushughulikia mimba zilizo hatarini.

“Pia anemia kali, ambayo bado haijabadilika sana. Hii inaonesha kuwa ingawa kesi kali si za kawaida, bado ni changamoto kubwa inayohitaji mawasiliano endelevu na uhamasishaji wa jamii, na kuboresha utoaji wa huduma za msingi ili kuhakikisha utambuzi wa mapema na usimamizi wa mimba hatarishi ili kupunguza vifo vya wajawazito.