Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, amehitimisha bajeti yake kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2026/27, huku suala la bei ya mafuta likiwa si miongoni mwa mambo yaliyopata jawabu.
Hitimisho hilo la Dk Mwigulu leo, Aprili 15, 2026 limekuwa kimya kuhusu bei ya mafuta, licha ya suala hilo kuibua mjadala mkali kutoka kwa baadhi ya wabunge walipokuwa wakijadili bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya Sh12.5 trilioni.
Ukiacha mtendaji mkuu huyo wa Serikali kutoligusia suala hilo wakati wa hitimisho lake, hata Waziri wa Nishati na naibu wake hawakuwa sehemu ya mawaziri waliozungumza wakati mawaziri mbalimbali wakichangia.
Mambo yameenda hivyo, ingawa hitimisho hilo la Dk Mwigulu lilitarajiwa kutoa kauli ya Serikali kuhusu hatua ilizozichukua kuwapunguzia wananchi gharama za maisha baada ya kupanda kwa bei ya mafuta iliyoanza kutumika Aprili mosi, 2026.
Ilitarajiwa hivyo, tayari kulishafanyika vikao kadhaa kulijadili hilo, kikiwemo kilichoihusisha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, iliyoitishwa kukaa na Spika wa Bunge, Mussa Zungu.
Kamati hiyo ilikaa vikao vyake pamoja na Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi, Waziri Mkuu mwenyewe na Zungu pia, yote hayo yakiwa na lengo la kuja na jawabu kuhusu hatua za kuchukua baada ya kupanda kwa bei ya mafuta.
Bei ya mafuta imepanda duniani kote baada ya vita Mashariki ya Kati inayolihusisha Taifa la Marekani, Israel dhidi ya Iran. Vita hivyo vimeathiri miundombinu ya uzalishaji na mnyororo wa ugavi wa nishati hiyo duniani.
Dk Mwigulu amehitimisha mjadala huo leo, Jumatano, Aprili 15, 2026, baada ya hoja mbalimbali za wabunge na michango ya mawaziri bungeni, jijini Dodoma.
Ukiacha kukosekana kwa jawabu kuhusu kupanda kwa bei ya mafuta, Dk Mwigulu alielekeza hitimisho lake akipongeza juhudi zilizofanywa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuleta maendeleo.
Miongoni mwa mambo aliyopongeza ni kuongezeka kwa bajeti za wizara mbalimbali, ikiwemo kilimo, iliyoongezeka zaidi ya mara tano kutoka takriban Sh270 bilioni hadi zaidi ya Sh1.2 trilioni.
Ametaja kuwa mageuzi katika sekta za uzalishaji yamefanyika na sasa kumekuwa na miradi ya umwagiliaji iliyogharimiwa zaidi ya Sh30 bilioni, jambo alilosema lilikuwa nadra miaka ya nyuma.
“Rais amekuta miradi takriban 13 ya umwagiliaji, na sasa kuna miradi zaidi ya 780 inayojengwa kwa ajili ya shughuli za umwagiliaji,” amesema.
Dk Mwigulu pia amesema Rais Samia anaingia katika kumbukumbu za kiongozi aliyetekeleza miradi mikubwa, likiwemo Bwawa la Umeme la Julius Nyerere (JHPP), na kufanya Tanzania kuwa na ziada ya umeme.
Mtendaji mkuu huyo wa Serikali amesema suala la kukatika kwa umeme kwa sasa si upungufu wa nishati hiyo, bali linasababishwa na changamoto katika gridi iliyojengwa muda mrefu, ambayo haendani na uzalishaji wa sasa.
“Miradi imejengwa kwa siku nyingi na wakati huo makadirio ya umeme yalikuwa kwa matumizi ya watu wachache, kwa sasa hivi ni kila kijiji. Rais ameliona hilo—kuna mradi wa Sh1.2 trilioni wa kujenga gridi imara ili kuondokana na kukatika kwa umeme,” amesema.
Baada ya Bunge kuipitisha bajeti hiyo, Spika, Mussa Zungu, aliwapongeza wabunge kwa kazi kubwa waliyoifanya: “Mmeweza kubainisha kero zote za nchi yetu na Serikali imeweza kuzijibu.” Akawatakia kheri Ofisi ya Waziri Mkuu katika kuitekeleza.
