SIMBA imeanza harakati za kujenga kikosi cha msimu ujao mapema ambapo inadaiwa imetua Dodoma Jiji na kuchomoka na saini ya straika kinara wa mabao ndani ya timu hiyo, Edgar William.
Mwanaspoti limepenyezewa kwamba, wakati Simba ipo Arusha ikicheza mechi ya hatua ya 16 bora ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya Dodoma Jiji na kushinda 3-1, mabosi wa klabu hiyo walimalizana na straika huyo.
Straika huyo aliyetua Dodoma Jiji msimu huu akitokea Fountain Gate ambayo aliichezea msimu mmoja tu, rekodi zake zinaonyesha amekosa mechi moja kati ya 18 ilizocheza timu hiyo, akifunga mabao matano, ndiye kinara wao wa ufungaji kikosini hapo katika Ligi Kuu Bara msimu huu.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kwamba, Simba imempa Edgar mkataba wa miaka miwili ambao ataanza kuutumikia msimu ujao.
“Simba inataka kuweka nguvu kubwa msimu ujao eneo la mbele hasa kwa washambuliajia ndio maana wameanza kuwasajili mapema kabla ya msimu kuisha.
“Amepewa mkataba wa miaka miwili na Simba inamuona kama Kibu Denis mpya kutokana na namna yake ya uchezaji wa kasi,” kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kiliendelea kubainisha kwamba, Edgar ambaye mkataba wake na Dodoma Jiji unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu, klabu hiyo ilikuwa katika mkakati wa kumuongezea, lakini dau la Simba limemvutia straika huyo.
“Ofa ya Simba ni kubwa, wamemuwekea Sh100 milioni mezani kiwango ambacho Dodoma Jiji imeshindwa kukifikia ili kumbakiza mshambuliaji huyo,” kilisema chanzo hicho.
Uamuzi huo wa Simba unakuja kutokana na kikosi hicho kuwa na uhaba na washambuliaji ambapo sasa inamtegemea zaidi Seleman Mwalimu anayecheza hapo kwa mkopo unaomalizika mwisho wa msimu huu akitokea Wydad Athletic ya Morocco.
Wakati Mwalimu akiwa tegemeo huku akifunga mabao sita Ligi Kuu Bara na kuongoza kikosini hapo, Simba inaelezwa mwisho wa msimu huu itaachana na mshambuliaji wake, Jonathan Sowah, hivyo ina uhitaji wa kuongeza nguvu eneo hilo.
Taarifa za Simba kutua kwa Edgar zinakuja siku chache baada ya kuripotiwa kumpa mkataba wa miaka miwili winga wa TRA United, Ramadhan Salum Chobwedo ambaye awali pia ilielezwa Yanga ilikuwa ikimpigia hesabu.