ALIYEWAHI kuwa Kocha wa timu za soka hapa nchini ikiwamo Stand United ‘Chama la Wana’, Pamba (kwa sasa Pamba Jiji), Athuman Bilali ‘Bilo’, amefariki dunia huku chanzo kikiwa bado hakijafahamika.
Bilo ambaye hadi anakutwa na umauti, alikuwa anamiliki kituo cha michezo na timu ya Bilo Queens ya Ligi Kuu ya Wanawake.
Akizungumza na Mwanaspoti, Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Mwanza (MZFA), Leonard Malongo, amethibitisha kufariki kwa kocha huyo akieleza kuwa ni masikitiko makubwa kwa wadau na mashabiki wa soka mkoani humo na Tanzania kwa ujumla.
Amesema taarifa za awali zinadai kuwa, kocha huyo jana Aprili 15, 2026 aliendelea na shughuli zake za mazoezi na timu yake ya Bilo Queens katika Uwanja wa Shule ya Msingi Nyasaka jijini humo hadi jioni ambapo wachezaji walimuacha eneo hilo akiwa amekaa.
“Jana alikuwa uwanjani akifanya mazoezi na timu yake, ila hadi wanaondoka wachezaji wakamuacha amekaa hadi kukutwa asubuhi amefariki dunia hapohapo.
“Bado hatujajua chanzo zaidi kwa kuwa mwili wake upo hospitali, tutafahamu kwa ujumla ikiwamo ratiba na taratibu zingine za mazishi, lakini kwetu wadau na mashabiki ni pigo,” amesema Malongo.
Bilo kipindi cha uhai wake, amefundisha timu kadhaa ikiwamo Toto Africans aliyoichezea pia, Gwambina FC, Alliance FC na hadi anakutwa na umauti alikuwa mmliki wa Kituo cha Michezo cha Bilo Sports chenye timu ya Bilo Queens inayoshiriki Ligi Kuu Soka Wanawake Tanzania Bara.
