Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amekutana na mwakilishi wa Jumuiya ya Madola, ambaye pia ni Rais wa zamani wa Malawi, Lazarus Chakwera na kumweleza mambo saba ya kufanyiwa kazi kwa mustakabali wa demokrasia na utawala wa sheria nchini.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Chadema leo Aprili 16, 2026, Lissu alikutana na mwakilishi huyo wa Jumuiya ya Madola Aprili 15, 2026 ikiwa ni mwendelezo wa Chakwera kukutana na makundi mbalimbali ya wadau wa siasa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa chama hicho, Brenda Rupia, Lissu alimweleza Chakwera kuwa kesi ya uhaini inayomkabili inatokana na msimamo wake wa No Reforms, No Election, hivyo alisisitiza kufutwa kwa kesi zote zinazomkabili yeye na chama, pamoja na utayari wake wa kushiriki mazungumzo akiwa huru.
Jambo lingine, ni kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu matukio ya Oktoba 29, 2025, kupitia taasisi kama Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC).
Taarifa hiyo imetaja sharti lingine kuwa ni “uwepo wa mazingira wezeshi kwa mazungumzo ya kweli na utekelezaji wake. Pia, uwajibikaji wa kitaasisi kwa yaliyotokea Oktoba 2025, hususan kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.
Taasisi nyingine alizotaka ziwajibike katika matukio hayo ni Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), sambamba na kurejea ripoti ya Jaji Francis Nyalali (1992).
Jambo lingine ambalo Lissu alimweleza Chakwera, kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, ni kufanyika kwa mageuzi ya vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuzingatia Ripoti ya Jaji Chande (2023).
Vilevile, uwepo wa mabadiliko ya mfumo mzima wa uchaguzi, ikiwemo kuundwa kwa chombo kipya huru cha kusimamia uchaguzi, kwa kuzingatia ripoti mbalimbali za waangalizi wa uchaguzi 1995 – 2025), pamoja na ripoti za Jaji Warioba na Jaji Nyalali.
Katika hatua nyingine, taarifa hiyo imeeleza kwamba Lissu amepatiwa nakala ya uamuzi wa Mahakama ya Rufani uliotolewa Aprili 15, 2026 unaoruhusu chama hicho kuendelea na shughuli zake.
Chama hicho kimeeleza baada ya kuupitia uamuzi huo, wanatoa wito kwa wanachama na Watanzania kujiandaa kwa hatua zinazofuata za kisiasa, ikiwemo maandalizi ya mikutano ya hadhara.
“Chadema kinaendelea kusisitiza dhamira yake ya kupigania haki, demokrasia, utawala bora na masilahi ya wananchi kwa njia za amani na kisheria,” imeeleza taarifa hiyo.
Kupitia taarifa hiyo ya Chadema, Lissu alikutana na wakili wake, Paul Kisabo katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam na kupitia mazungumzo yao, wamejadili kwa kina mwenendo wa kesi mbalimbali zinazomkabili pamoja na zile zinazoendelea dhidi ya chama.
